Monday, October 20, 2014

Ndesamburo: CCM wataendelea kunisindikiza Moshi Mjini

Moshi.
Mbunge wa Moshi mjini, Philemon Ndesamburo ameapa kufanya kampeni angani na ardhini, kuhakikisha kuwa CCM inashindwa vibaya uchaguzi mkuu wa 2015.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana mjini Moshi, Ndesamburo aliahidi kutoa helikopta yake na kukodi nyingine kutoka nje ya nchi kuendesha kampeni hiyo ya nguvu.

Hata hivyo, Ndesamburo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, alikataa kutaja idadi ya helikopta zitakazokodishwa akisema kufanya hivyo ni kuwapa faida maadui kujipanga kukukabili.

“Nataka niwahakikishie helikopta itaruka katika kila kijiji cha mkoani Kilimanjaro kuhakikisha CCM hakipati jimbo hata moja. Uwezo huo ninao. Sababu ninazo na nia pia ninayo,” alisema na kuongeza:

“2015 Tutawapelekesha mchakamchaka ambao hawajawahi kuuona. Tunaomba wananchi watuunge mkono na tutaanzia kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa Desemba.”

Kwa mujibu wa Ndesamburo, helikopta hiyo na zingine zitakazokodishwa kama itabidi, zitatumika pia kumnadi mgombea urais atakayepeperusha bendera ya Ukawa katika uchaguzi huo.

Ndesamburo alisema kupitia mwongozo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), watateua wagombea wanaokubalika na wananchi na siyo wanaokubalika na viongozi kama wanavyofanya CCM.

“Safari hii hakuna mgombea kupita bila kupingwa. CCM wajiandae kwa maumivu na wajiandae kwa maumivu makubwa kuliko wanavyofikiri,”alisisitiza Ndesamburo na kuongeza:

“Tumejaribu kutafuta na kujenga uhusiano na vyama vingine vya siasa. Nchi itatikisika kwa matokeo ya uchaguzi huu.”

Alisema CCM walizoea siku zote kuwa harakati za Chadema zinapimwa kwa mikutano ya hadhara na maandamano, lakini Chadema kiliamua kwenda kimya kimya na kujikita kwa wananchi.

“Kitu ambacho hawakukijua ni kwamba tuliacha mikutano ya hadhara na maandamano tukaamua kushuka chini kuunda uongozi kitongoji kwa kitongoji Tanzania nzima,”alisema.

Amshangaa JK kuhusu Katiba

Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya, Ndesamburo alisema anachokiona sasa ni kwamba Rais Jakaya Kikwete hakuwa na dhamira ya dhati ya kuwapatia Watanzania Katiba Mpya wanayoitaka.

Ndesamburo alisema makubaliano kati ya Rais Kikwete na viongozi wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), yalikuwa ni kuahirisha kura ya maoni hadi baada ya uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, Ndesamburo alisema kinachoonekana ni kwamba Rais anatamani kura ya maoni ipigwe kabla hajaondoka madarakani na ndiyo maana ameanza kuipigia debe Katiba Inayopendekezwa.

“Nchi imegawanyika vipande vipande kutokana na ubabe uliotumika kupitisha Katiba. Leo Rais haoni hili naye anaendelea kuligawa taifa kwa kuipigia debe katiba ambayo haina maridhiano,” alisema.

“Mimi nawaambia Watanzania tusikate tamaa. Tulikuwa na Katiba ya 1977 ni mbaya ambayo tuliipigia kelele sana. Leo tunaletewa katiba isiyobeba maoni yetu. Tuikatae.”

Ndesamburo aliongeza kusema kuwa kilichofanywa na Bunge Maalumu, ndiyo kimechochea upya mapambano ya kudai Katiba Mpya inayotokana na wananchi.

“Mapambano ya kudai katiba mpya ndiyo yameanza upya na yataendelea. Mbinu chafu zimetumika kuipitisha, lakini Watanzania wanajua nini kimetokea,” alisisitiza Ndesamburo.

Aeleza siri ya ushindi wake

Ndesamburo ambaye amekuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa vipindi vitatu (2000-2015), alisema siri ya ushindi wake inatokana na yeye kutojikweza wala kuwa na dharau.

“Siri ya ushindi ni kwamba mimi ni mtu wa kawaida, niko katika hali ya chini sijikwezi. Siwezi kuwa mbunge halafu nikaamua kukaa juu kama ndege. Mimi nakaa kwenye jimbo langu na wananchi wangu,” alisema.

“Najivunia kuwa mimi siyo mbunge anayekaa Dar es Salaam. Siku zote mchana na usiku niko na watu wangu. Ubaya wa wabunge wetu wengi wakishachaguliwa wanakwenda Dar es Salaam.”

Ndesamburo alisema kinachowafanya wabunge wengi kuwakimbia wapiga kura wao ni dhana iliyojengeka kuwa wapiga kura wanaomba sana pesa, jambo alilosema si la kweli.

“Kuna hisia kuwa mbunge ni mtu anayegawa pesa kwa hiyo wabunge wanayakimbia majimbo yao . Lakini dhana hii si ya kweli kwa sababu mimi nakaa hapa Moshi na naishi na watu wangu,” alisema.

“Wengine wanakimbia mahitaji ya wapiga kura wanaona hawayamudu. Lakini mimi nakaa nao wananijua hali yangu halisi kidogo ninachokuwa nacho natoa kama sina watu wangu wananielewa,” alisema.

“Na mimi nimeingia kwenye siasa siyo kama kutafuta ajira. Nina biashara zangu zinanipa pesa za kutosha. Pesa za ubunge nazitumia katika maendeleo ya jimbo langu.”

Atamba CCM kumpigia kura

Ndesamburo alisema baadhi ya kura zinazompa ushindi kila mara hutokea kwa wanachama wa CCM ambao hawachagui chama, bali wanatazama kiongozi bora.

“Watu wa Moshi wanatafuta kiongozi bora hawatafuti chama. Hata wanachama wa CCM siyo wajinga kwamba wachague tu mtu wa CCM wakati wanaona kabisa hafai,”alisema.

Ndesamburo alisema siku zote wanaCCM wamekuwa wakimuunga mkono kwa sababu wanaamini yeye ni kiongozi wa watu na asiye na makuu na si mbunge wa kuletewa na viongozi.

“Wanachagua mtu ambaye anawafanyia kazi. Kwa hiyo watu wa CCM wengi wa Moshi wananipigia kura na huo ndiyo ukweli. Wanajua pumba ni zipi na mchele ni upi”.

Ndesamburo alisema hata hasimu wake wa kisiasa, Elizabeth Minde akiamua kurudi tena katika kinyang’anyiro hicho mwaka 2015 hawezi kumshinda hata kama CCM yote itahamia Moshi Mjini.

Mbunge huyo amechuana na Minde (CCM) ambaye ni wakili wa kujitegemea mara mbili mwaka 2000 na 2005 na kumshinda.

Asita kusema atagombea tena au la

Ndesamburo alipoulizwa kuhusu uvumi kuwa hagombei tena ubunge 2015 alisema, “Tungojee muda ukifika nitatoa tamko.”

Kauli hii ya Ndesamburo ambayo amekuwa akiitoa kila mara anapoulizwa, inatafsiriwa na wengi kuwa hana mpango tena wa kugombea ubunge mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Ndesamburo, hata kama ataamua kutogombea uchaguzi mkuu wa 2015, bado CCM hawawezi kunyakua jimbo hilo kutokana na misingi aliyoiweka.

“Lakini nataka niwahakikishie CCM kwamba iwe isiwe jimbo la Moshi Mjini lazima libakie Chadema na hilo CCM wanalijua ila wanaleta kiburi tu,”alisema Ndesamburo.

Aeleza alivyotetereka kibiashara

Ndesamburo alidokeza kuwa alipojiunga na Chadema akiwa miongoni mwa waanzilishi 10 wa chama hicho mwaka 1992, akiwa na kadi namba 10, biashara zake ziliyumba sana wakati huo.

“Mimi ni mwanzilishi wa mageuzi katika Tanzania, wakati siasa za upinzani zilipoanza mwaka 1992 mimi nilikuwa mwanzilishi wa Chadema. Wale waanzilishi 10 kadi yangu mimi ni namba 10.”

“Nimekuwa ni mashabiki, nimekuwa mtetezi na kwa kweli niliingia katika siasa kwa kutaka kubadilisha maisha ya Watanzania. Ilikuwa ni kazi ngumu sana wakati ule,” alisema na kuongeza:

“Mimi nikiwa mfanyabiashara ilikuwa ngumu kuingia upinzani. Hali ya hewa ilikuwa siyo nzuri sana kwa mfanyabiashara kujiunga na upinzani ilikuwa ni vigumu kuonekana ni mtu wa upinzani uweze kufanya biashara Tanzania.”

“Kwa hiyo kimaendeleo biashara zangu ziliathirika sana, kwa mimi kuingia kwenye siasa. Sikufa moyo kwa sababu nilijua ukombozi una gharama zake,” alisema.

Ndesamburo alisema hadi sasa, wapo wafanyabiashara wanaoogopa kujiunga na vyama vya upinzani kwa kuogopa kufuatwafuatwa na wakati mwingine kuwekewa mizengwe hadi wafilisike.

Aeleza Mrema alivyomtibulia 1994

Ndesamburo alisema katika uchaguzi wa vyama vingi wa kwanza wa udiwani 1994, yeye aligombea udiwani wa Kata ya Kiborlon katika Manispaa ya Moshi.

Alisema pamoja na Naibu Waziri Mkuu wakati huo, Augustino Mrema kufanya mkutano wa mwisho wa kampeni katika kata hiyo ili kumvurugia, lakini anaamini alishinda uchaguzi huo.

“Mimi nilisimama Kata ya Kiborlon nilishinda, lakini kwa mbinu za CCM wakachakachua nikaambiwa nilishindwa. Sikukata tamaa.

“Uchaguzi mkuu wa 1995 nilisimama kugombea ubunge Jimbo la Moshi Mjini, lakini wakati ule Mrema alikuwa na nguvu sana akaniomba niingie NCCR-Mageuzi, nilikataa,”alisema na kuongeza:

“Baadaye nikashindwa na Joseph Mtui wa NCCR-Mageuzi kwa sababu watu walikuwa wanaamini Mrema angeshinda. Mwaka 2000 niligombea tena na nikashinda mpaka leo,” alisema Ndesamburo.

Ajivunia rekodi yake

Ndesamburo alisema tangu awe mbunge wa Moshi Mjini mwaka 2000, ameweza kutuliza hali ya kisiasa ya Moshi na ndiyo maana hakuna vurugu zozote za kisiasa katika kipindi chote cha miaka 15.

“Hakuna siku polisi wamepiga mtu, hakuna maandamano ambayo yameleta vurugu. Mimi nimekuwa balozi mzuri wa kuhubiri siasa ambazo siyo za vurugu,” alisema.

“Siwezi kusema nimefanya nini. Watu wa Moshi wanajua kazi nilizozifanya mimi kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani,”alisema na kuongeza:

“Leo Mji wa Moshi umeeneza barabara za lami ambazo tumezijenga wenyewe kutokana na uongozi makini na wa pamoja kati ya madiwani na wananchi.”

Ndesamburo alisema katika kipindi chake cha uongozi, Mji wa Moshi umeweza kushika nafasi ya kwanza kwa usafi nchini kwa miaka sita mfululizo, jambo alilosema ni la kujivunia.

“Yapo mengi tumeyafanya tunakarabati barabara za pembezoni tena kwa kutumia katapila nililonunua mwenyewe kwa ajili ya watu wangu. Tumejenga shule na kuongeza mapato ya halmashauri,” alisema.

“Wananchi wana macho, wanaona tofauti kati ya kipindi CCM iko madarakani na kipindi cha miaka 15 ambayo Chadema iko madarakani. Wamachinga wamefanya kazi zao kwa amani zaidi,” alisema.

Historia yake

Ndesamburo alizaliwa Februari 19, 1935 na kusoma Shule ya Msingi ya Matemboni kuanzia mwaka 1944 hadi 1950 na baadaye akajiunga na Government Commercial School mwaka 1954.

Akajiunga serikalini na kufanya kazi mpaka mwaka 1968 alipokwenda chuo cha Thurock cha nchini Uingereza na kupata Diploma ya juu katika masuala ya biashara.

Aliporejea nchini alifanya kazi serikalini kabla ya kuamua kujiajiri mwenyewe.

Ndesamburo anamiliki vitegauchumi kadhaa ukiwemo mtandao wa hoteli za Keys, kampuni ya utalii na vitegauchumi vingine nje ya nchi.


No comments:

Post a Comment