Wednesday, October 29, 2014

Mbowe: Ukawa sasa ni mbele kwa mbele

Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kamwe hautarudi nyuma katika makubaliano yaliyofikiwa juzi, likiwamo la kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Kauli ya Mbowe ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa imekuja huku kukiwa na maoni kutoka kwa watu mbalimbali wakiukosoa ushirikiano huo na kwamba hautadumu kutokana na viongozi wengi wa kisiasa nchini kuwa na tabia za kutanguliza masilahi binafsi.
Miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa kikwazo kwa viongozi hao ni suala la ruzuku ambayo hutolewa kwa kuzingatia wingi wa wabunge na idadi ya kura za mgombea urais pamoja na suala la mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi hasa katika maeneo ambayo chama zaidi ya kimoja vina nguvu.
Hata hivyo, jana Mbowe alipuuza dhana hiyo kwa kusema: “Historia ya upinzani nchini imetufundisha mengi na tutakuwa wajinga kama muda wote hatukuweza kujifunza.
“Tunafahamu na tunatambua wapo watu ambao walijitahidi sana kutugawa na kutugombanisha, lakini naomba Watanzania watambue kwamba katika hatua hii hatutakubali kugawanyika tena wala kugombana tena.”
Juzi, vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, NCCR Mageuzi, CUF na NLD vilisaini makubaliano ya kushirikiana ikiwa ni pamoja na kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zote zijazo tukio lililofanyika kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Akizungumzia suala la ruzuku, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema: “Tuna uzoefu wa miaka 24 sasa katika siasa za vyama vingi na siasa za ushindani, kwa hiyo suala la ruzuku haliwezi kutugombanisha kwa sababu tumeamua kwa dhati kuweka mbele masilahi ya nchi.
“Hilo linawezekana kabisa, tumeonyesha mfano kwa sababu pamoja na umaskini wetu, tulisusia Bunge la Katiba na tukakosa zaidi ya Sh3 bilioni. Hii haimaanishi kwamba watu wetu hawakuwa wakihitaji hizo fedha, lakini ni suala la msimamo tu kuhusu masilahi mapana ya nchi.”
Alisema mambo yote yanayofanyika ndani ya ushirikiano huo yamekuwa yakiratibiwa na timu za wataalamu wakiwamo wanasheria kisha mapendekezo husika kuridhiwa na viongozi wakuu, hivyo hakuna shaka kwamba kila jambo litafuata utaratibu huo.
“Tunao wataalamu wengi wakiwamo wanasheria, kwa hiyo hakuna kitakachoshindikana maana sisi hatuongozwi na matakwa ya ruzuku, tunaongozwa na dhamira safi za kutanguliza masilahi mapana ya nchi,” alisisitiza.
Muungano wa Ukawa dhidi ya CCM, ni matokeo ya misuguano iliyojiri wakati wa mchakato wa Katiba. Hatua ya kwanza ilianza kwa Mbowe kuunda Baraza la Mawaziri Kivuli, likiwashirikisha wabunge kutoka vyama hivyo isipokuwa NLD ambacho hakina mwakilishi bungeni.

Wakosoaji
Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), Kapteni John Komba alisema ushirikiano huo ni feki na unalenga katika masilahi binafsi na kwamba hauwezi kukiyumbisha chama chake. Pia alisema kukosekana kwa wanawake wa kutosha kwenye mkutano huo wa juzi ni dalili tosha ya anguko la Ukawa.
“Ukiona wapinzani wanaungana ujue wamegundua nguvu ya kila mmoja wao haitoshi kuing’oa CCM, lakini swali la msingi kujiuliza ni je, muungano huo utaleta tija inayokusudiwa? Watasambaratika baada ya muda mfupi na masilahi binafsi pamoja na itikadi tofauti ndizo zitakazochangia,” alisema Komba.
Komba alisema aliangalia mkutano huo kupitia runinga lakini alishangazwa na idadi ndogo ya wanawake waliohudhuria na kusema kuwa hiyo ni ishara kuwa kinamama hawaukubali umoja huo.
Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray alisema: “Hili si jambo jipya kwa kuwa lilishawahi kutokea lakini baada ya kuona halina maana wengine tuliamua kujitoa… tumekaa pembeni tuone watakapofika.
“Huko mbele ni lazima watakorofishana hasa litakapokuja suala la masilahi. Inaeleweka wazi kuwa chama chenye wawakilishi wengi ndicho kinapata ruzuku. Kusimamisha mgombea wa urais pekee ina maana kubwa kwa kila chama, sijui kama wameweka wazi utaratibu wa kugawana ruzuku itakayopatikana kwa chama kitakachostahili.”
Mziray alibainisha kuwa anakumbuka vizuri ushirikiano uliokuwapo kati ya Chadema na Mchungaji Christopher Mtikila ambaye baada ya kukiunga mkono chama hicho hakuambulia chochote.
Kwa upande wake, Mtikila ambaye ni Mwenyekiti wa DP aliuponda muungano huo akisema: “Nililetewa mwaliko wa kuhudhuria mkutano uliofanyika juzi kutoka kwa mratibu wa Ukawa, ambaye simjui. Siwezi kwenda huko kwa sababu wakati wanaanzisha Ukawa ilikuwa ni Umoja wa Katiba ya Watanganyika na si kama wanavyoieleza.”
Alidai kwamba ndiye aliyeanzisha mchakato wa kudai Katiba ya Watanganyika baada ya Rais Jakaya Kikwete kulihutubia Bunge Maalumu la Katiba lakini baada ya Chadema kuchukua hatamu za kuongoza harakati hizo alijiweka pembeni.

Wabunge wa upinzani
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa alisema nafasi za uongozi katika ushirikiano wa Ukawa zipo wazi kwa kila mwanachama, hivyo ushindani utahusisha wote walio tayari kushindana.
“Jimbo si mali ya mbunge aliyepo, kitakachoendelea kumweka madarakani ni uchapakazi wake licha ya kuungwa mkono na Ukawa. Yapo maeneo yanatambulika kuwa ni ngome za vyama fulani vya upinzani huko, tutaunga mkono ili kupata ushindi mkubwa zaidi. Katika maeneo ambayo CCM wanaongoza juhudi binafsi ndizo zitakazotumika kumpata mpinzani atakayeungwa mkono na wote.”
Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Barwan Salum alisema historia inaonyesha kuwa vyama vya upinzani vinaongoza katika maeneo tofauti na kwamba juhudi hizi zinalenga kuwanufaisha wananchi.
“Chadema ina nguvu kubwa Kaskazini mwa nchi wakati NCCR-Mageuzi ikiongoza Magharibi na CUF wanafanya vizuri Visiwani. Katika chaguzi zilizopita, takwimu zinaonyesha kuwa vyama vya upinzani kwa jumla wake vilikuwa vinapata asilimia 40 ya nafasi zote. Umoja huu unamaanisha makubwa katika siasa za nchi hii.”

Wananchi
Mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam, Hamis Suleiman (72), alisema muungano huo ni mwamko mpya wa siasa nchini kwani hakuwahi kufikiria kuwa kuna siku wapinzani watakuja kuonyesha mshikamano mkubwa kiasi hicho katika kupigania masilahi ya taifa.
“Ni kitu kipya katika historia ya Taifa letu. Wakati tunadai uhuru iliwezekana kuona mambo haya lakini kwa sasa naona harakati hizo zinafanywa kudai utawala bora na usawa kwa wananchi wote,” alisema Suleiman.
Mkazi mwingine, Deogratius Bikongoro alisema hakuamini kama wapinzani wanaweza wakafanya kitu kikubwa kama hicho, tena hadharani na kwamba alishawishika kwenda kwenye mkutano huo ili aweze kujiridhisha.
“Nimejifunza elimu ya uraia katika tukio hili. Kumsikiliza Tundu Lissu na Ismail Jussa Ladhu wakifafanua Katiba Inayopendekezwa pamoja na sheria za nchi kwa jumla, imenipa ufahamu wa mambo mengi niliyokuwa siyajui lakini nimeona dhamira ya wapinzani sambamba na mwitikio wa wananchi. Mkutano huu unatoa picha kuwa hata huko mikoani kuna watu ambao hawajaridhika na jinsi mchakato wa Katiba ulivyokwenda,” alisema.
Mmoja wa waasisi wa Chadema, Victor Kimesela alisema mchakato wa kuunganisha vyama vya upinzani ulianza siku nyingi kutokana na mahitaji ya wananchi... “Wananchi watanufaika kutokana na muungano huu ambao unaunganisha juhudi tofauti zinazoletwa na itikadi mtambuka.”
Alisema juhudi za kuunganisha vyama zimepitia hatua nyingi na kuzitaja kuwa ni pamoja na kuundwa kwa Umoja wa Demokrasia Tanzania (Udata) na Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (Kamaka) na kusisitiza kuwa Ukawa ndiyo hitimisho la juhudi hizo.
Mkurugenzi wa Fedha wa CUF, Joran Bashange alisema:
“Masilahi ya Taifa ndiyo kitu cha msingi kinachotuunganisha pamoja na tunawaomba wote walio tayari kushirikiana nasi watuunge mkono katika kutekeleza azma hii muhimu kwa wananchi na nchi kwa ujumla. Masilahi binafsi siyo hoja yetu kwa kuwa wapo watu wengi wasio wafuasi wa siasa hapa nchini lakini wanaovutiwa na haja ya kuwa na maendeleo sawa kulingana na rasilimali zilizopo.”
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa NCCR-Mageuzi, Mohamed Tibanyendera alisema kitendo cha CCM kutunga Katiba yenye mapendekezo yake pekee na kuyatupia kisogo maoni ya wananchi, kimepokewa vibaya na Watanzania wengi ambao wanataka mabadiliko kupitia umoja huu.
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa alisema: “Historia inaonyesha kuwa ni vigumu kwa vyama vya upinzani kukiondoa madarakani chama tawala pasipo ushirikiano wa vyama hivyo. Tuliona yaliyotokea Afrika Kusini na hata jirani zetu Kenya… muungano huu utaleta mapinduzi kama yaliyotokea Kenya.”


No comments:

Post a Comment