Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, (pichani) amesema mapambano ya kudai katiba ya Watanzania yameanza upya hata kama Bunge Maalumu la Katiba litaamua vinginevyo.
Amesema uamuzi wowote utakaofanywa, hautakuwa na uhalali na hautaheshimiwa na mtu yeyote kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mawakala wao ndani ya Bunge wana shida ya akidi na ndiyo maana imewabidi wachakachue sheria na kanuni ili kuhakikisha wanaonekana wamekidhi matakwa ya akidi inayohitajika.
Lissu alisema hayo alipokuwa akihojiwa jana asubuhi na kituo kimoja cha runinga kuhusiana na upigaji wa kura ulioanza jana mjini Dodoma kwa ajili ya kupitisha rasimu ya katiba inayopendekezwa na Bunge hilo.
Alisema uhalali anaoutaja, unadhirishwa na namna CCM na mawakala wao walivyokosa maarifa hata ya kufunika mambo ili kuonyesha kwamba, yanayotafutwa na Watanzania yanakwenda kisheria.
Lissu alisema duniani kote, kura za mabunge huwa zinazopigwa bungeni, hazipigwi hospitalini, kanisani, msikitini, Makkah na kwamba, kama jambo linalopigiwa kura ni jambo muhimu sana kama, ambavyo suala la katiba ni muhimu, wagonjwa huchukuliwa hospitalini na kuingizwa bungeni ili wapige kura na baadaye hurejesha hospitalini.
Alisema msimamo wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uko pale pale kwamba, kinachoendelea Dodoma hivi sasa ni haramu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi.
Lissu alisema katika vitu vinavyothibitisha kwamba, kinachoendelea ni utaratibu wa kulazimisha rasimu ya katiba ya CCM ili katiba inayopendekezwa ionekane imebeba mawazo ya Watanzania wakati wakiwa wameua moyo wa rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba ni mfumo unaolazimisha kura nje ya Bunge.
“Sheria za nchi hii kama zilivyo sasa, haziruhusu kabisa kupiga kura za utaratibu huu na kwenye mchakato huu huu wa katiba, mwaka jana (2013) tulipitisha bungeni Sheria ya Kura ya Maoni,” alisema Lissu.
Aliongeza: “Katika muswada ulioletwa bungeni na serikali, kulikuwa na mapendekezo, ambayo kama yangekubaliwa, wangeorodheshwa Watanzania waliopo nje ya nchi, waliopo hospitalini, magerezani au kwa sababu nyingine yeyote ile hawako katika maeneo ya kupiga kura, wapige kura, lakini mapendekezo hayo yalikataliwa na wana CCM kata, kata, hili la kupiga kura kwa mtandao limetokea wapi.”
No comments:
Post a Comment