UMOJA
WA KATIBA YA WANANCHI
(UKAWA)
TAMKO
LA UKAWA JUU YA AMRI YA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KUHUSU MAMLAKA YA BUNGE MAALUM
&
RASIMU
YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA ILIYOWASILISHWA KWENYE BUNGE MAALUM NA MWENYEKITI WA
KAMATI YA UANDISHI YA BUNGE MAALUM
Dar
es Salaam, 26 Septemba 2014:
Hapo jana tarehe 25
Septemba, 2014, Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa amri kuhusu maombi
yaliyofunguliwa na Bwana Saed Kubenea, mwandishi habari mwandamizi na mhariri
wa gazeti la Mwanahalisi kutaka Mahakama Kuu itoe ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge
Maalum kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya
83 ya Sheria za nchi yetu. Katika amri yake hiyo, Mahakama Kuu imesema
yafuatayo kuhusu mamlaka ya Bunge Maalum:
(a)
“Kwamba kuna mgongano katika maana
ya maneno yaliyotumika kwenye kifungu cha 25 cha Sheria hiyo kwenye toleo la
Kiingereza la Sheria hiyo. Hata hivyo, licha ya mgongano huo, tafsiri sahihi ya
maneno ya kifungu hicho ni kwamba:
(i)
“Mamlaka ya ‘kujadili na kupitisha
masharti ya Katiba inayopendekezwa’ maana yake ni mamlaka ya kutunga na
kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupelekwa kwa wananchi wa
Tanzania ili kupigiwa kura ya maoni;
(ii)
“Mamlaka hayo yatatekelezwa kwa
kutumia Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalum na Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Katika kufanya hivyo, Bunge Maalum linaweza
kuboresha na/au kurekebisha Rasimu ya Katiba. Mamlaka hayo yanamewekewa mipaka,
kama ilivyokuwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na tunu na maadili ya taifa
yaliyopo kwenye kifungu cha 9(2) cha Sheria;
(b)
“Mahakama haina mamlaka ya kuamua
aina na upeo wa maboresho na/au marekebisho ambayo Bunge Maalum linaweza
kuyafanya kwenye Rasimu ya Katiba kwa sababu hilo ni suala la kisiasa na wala
siyo la kisheria, ilimradi maboresho na/au marekebisho hayo hayaendi kinyume na
matakwa ya kifungu cha 9(2) cha Sheria.”
Uamuzi huu ni
muhimu kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu zifuatazo:
(1)
Tangu kuanza kwa Bunge Maalum mwezi
Februari mwaka huu, kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya wajumbe wa UKAWA na
wajumbe wa CCM na mawakala wao katika Bunge Maalum kuhusu mamlaka ya Bunge
Maalum kama yalivyoainishwa kwenye kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba. Wakati UKAWA imeshikilia msimamo kwamba mamlaka ya Bunge Maalum yana
mipaka kisheria na Bunge hilo halina mamlaka ya kubadilisha misingi mikuu ya
Rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi, CCM na mawakala wake imeshikilia
msimamo kwamba mamlaka ya Bunge Maalum hayana mipaka na Bunge Maalum lina uwezo
wa kufanya marekebisho au mabadiliko yoyote kwenye Rasimu ya Katiba. Uamuzi wa
Mahakama Kuu unathibitisha usahihi wa hoja ya UKAWA kwamba mamlaka ya Bunge
Bunge Maalum yana mipaka kisheria;
(2)
Kwa kusema kwamba Bunge Maalum lina
mamlaka ya kufanya maboresho na/au marekebisho kwenye Rasimu ya Katiba,
Mahakama Kuu imekataa dhana ya CCM na mawakala wake kwamba Bunge Maalum lina
mamlaka ya kubadilisha Rasimu ya Katiba. Amri ya Mahakama Kuu haijataja kabisa
neno ‘kubadilisha’ ambalo liliingizwa kwa nguvu kwenye Kanuni za Bunge Maalum.
Kwa maana hiyo, kanuni ya 3 ya Kanuni za Bunge Maalum inayotafsiri neno ‘hoja’
kuwa ni pamoja na mamlaka ya Bunge Maalum kubadilisha Rasimu ya Rasimu
inakwenda kinyume na matakwa ya kifungu cha 25 cha Sheria na kwa hiyo tafsiri
hiyo ni batili;
(3)
Kama ilivyokuwa kwa Mahakama ya
Rufani ya Tanzania katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya
Mwanasheria Mkuu iliyokuwa inahusu suala la mgombea binafsi, Mahakama Kuu ya
Tanzania imekwepa kutekeleza wajibu wake wa kutenda haki kwa kufuata Katiba na
Sheria za nchi kwa kujificha nyuma ya kichaka cha ‘maamuzi ya kisiasa.’ Mamlaka
ya Bunge Maalum yamewekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mipaka yake
imewekwa na Sheria hiyo pia. Mahakama Kuu, kama ilivyo kwa Mahakama nyingine
zote, ilikuwa na wajibu wa kutafsiri Sheria hiyo kwa kutamka bayana aina na
upeo wa mamlaka ya kisheria ya Bunge Maalum kufanya maboresho na/au marekebisho
ya Rasimu ya Katiba. Badala ya kutekeleza wajibu wake huo, Mahakama Kuu
imekwepa lawama za CCM na mawakala wake kwa kusema kwamba aina na upeo wa
maboresho na/au marekebisho ya Rasimu ya Katiba utategemea matakwa ya kisiasa,
yaani ya CCM na mawakala wake, badala ya kutegemea lugha ya Sheria yenyewe.
Aidha, Mahakama Kuu imekwepa lawama za UKAWA kwa kukubali hoja kwamba mamlaka
ya Bunge Maalum yana mipaka, hata hivyo bila kuifafanua mipaka hiyo;
KATIBA MPYA INATENGENEZWA KWA
MTUTU WA BUNDUKI!!!
Hali ya kisiasa katika nchi yetu kwa
sasa ni tete kwa kiasi kikubwa. Nchi yetu sasa iko chini ya utawala wa kijeshi
usiokuwa rasmi. Kila mahali katika makao makuu ya mikoa, wilaya na majimbo,
askari wa Jeshi la Polisi wakiwa na mabomu na risasi za moto, magari ya deraya,
farasi na mbwa wametanda kila mahali ili kujaribu kuzuia maandamano na mikutano
ya wananchi wanaopinga mchakato wa Katiba unaoendelea.
Mjini Dodoma, Jengo la Bunge la
Jamhuri ya Muungano ambalo linatumiwa na Bunge Maalum limezingirwa na vikosi
hivyo vya Jeshi la Polisi. Katika hali hii, ni wazi kwamba mchakato wa Katiba
umekuwa mateka wa Jeshi la Polisi, Bunge Maalum lenyewe ni mateka na Watanzania
wote ni mateka wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya mabavu. Katiba mpya
inatengenezwa kwa mtutu wa bunduki. Katika hali tete kama hii, kitu cha ajabu
kabisa ni kwamba Rais Jakaya Kikwete – kama ambavyo imekuwa kawaida yake sasa –
amekimbia nchi na kwenda Marekani kwa ziara ya wiki mbili.
Kama ambavyo UKAWA imesema katika
kipindi chote hiki, chochote kitakachotokana na mchakato huu wa kimabavu
hakitakuwa na uhalali wowote wa kisiasa. Sasa, baada ya mabadiliko mbali mbali
ya Kanuni za Bunge Maalum kuruhusu uchakachuaji sio tu wa Rasimu ya Katiba bali
pia uchakachuaji wa maamuzi ya wajumbe waliobakia wa Bunge Maalum, ni wazi pia
kwamba chochote kitakachotolewa na Bunge Maalum kwa sura ya Katiba
inayopendekezwa kitakuwa batili kisheria vile vile.
Kwa sababu hizo, tunawaomba
Watanzania wote wenye nia njema na nchi yao kupinga nchi yetu kugeuzwa kuwa
dola ya kipolisi na nchi ili chini ya utawala wa kijeshi usio rasmi. Tunawaomba
wanachama na viongozi wote wa vyama vya UKAWA kufanya maandalizi ya kupinga
vitendo hivi kwa njia mbali mbali za kidemokrasia. Aidha, wanachama na viongozi
wetu wafanye maandalizi kwa pamoja kwa ajili ya Uchaguzi wa Mitaa, Vijiji na
Vitongoji uliotangazwa kufanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Uchaguzi huo uwe ni
fursa ya kwanza ya kuiondoa CCM katika utawala wa nchi yetu kabla ya kuiondoa
kabisa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
-----------------------------------------------------------
Mh. Freeman Aikaeli Mbowe
MWENYEKITI MWENZA
Mh. Profesa Ibrahim Haruna
Lipumba
MWENYEKITI MWENZA
--------------------------------------------------------------------
Mh. James Francis Mbatia
MWENYEKITI MWENZA
No comments:
Post a Comment