Sunday, September 21, 2014

TAMKO LA CHAMA JUU YA UTEKELEZAJI WA AZIMIO LA MKUTANO MKUU KUHUSU MIGOMO NA MAANDAMANO YA AMANI NCHI NZIMA

TAMKO LA CHAMA JUU YA UTEKELEZAJI WA AZIMIO LA MKUTANO MKUU KUHUSU MIGOMO NA MAANDAMANO YA AMANI NCHI NZIMA

Ndugu waandishi wa habari

Tunapenda kuanza mkutano huu kwa kutoa salaam za amani kwa Watanzania
wote, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Amani Kimataifa,
ambayo huadhimiswa Septemba 21, ya kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu
kama ilivyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ni
'The Right Of People's to Peace'.

Tumekutana nanyi hapa siku hii mahsusi ya kuazimisha amani kimataifa,
tukiwa na ujumbe maalum kwa Watanzania kuwaeleza namna ambavyo
watawala wa Serikali ya CCM, wanavyohatarisha amani ya nchi yetu kwa
kuvunja haki za msingi za Watanzania huku pia wakififisha matumaini ya
wananchi.

Tunataja maneno hayo mawili HAKI na MATUMAINI kwa makusudi kabisa kwa
sababu hayo ndiyo ndiyo msingi wa amani na utulivu wa kweli mahali
katika taifa ambalo linajali na kuzingatia maendeleo na ustawi wa
wananchi wake.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba zake kali
kuonesha namna ambavyo walioko madarakani wanahatarisha amani na
utulivu wan chi, aliwahi kusema kuwa ni hatari sana iwapo wananchi
wakipoteza matumaini kwa viongozi wao huku pia hawaoni haki
ikitendeka. Mwalimu alikwenda mbali na kusema Watanzania watakuwa
'wapumbavu' wakikubali viongozi waendelee kwenda kinyume na maslahi au
matakwa ya wananchi wao.

Kama wananchi hawapati haki na wanapoteza matumaini na viongozi wao,
hakuwezi kuwa na amani na utulivu. Itabaki amani inayoimbwa na CCM
majukwaani wakati haki za msingi ndani ya nchi zikiminywa na kukiukwa.

Ni vigumu kuwa na amani au utulivu wa dhati iwapo haki za kisiasa (mf;
kukutana, kuandamana n.k), haki za kiuchumi (kuwa na maisha bora) haki
za kijamii (kupata elimu bora na bure, matibabu bora na bure, maji
safi na salama), n,k, huku ufisadi na ubadhirifu wa mali na rasilimali
za umma, ukiongezeka na UWAJIBIKAJI ukiwekwa kapuni.

Ndugu waandisi wa habari, ninyi pia ni mashahidi wa namna ambavyo
utawala huu wa CCM ambao umeshapoteza kabisa ushawishi wa kisiasa kwa
wananchi, umezidi kuminya haki ya kupata taarifa huku pia ikiendelea
kutumia sheria za kikoloni kuminya uhuru wa habari nchini.

Hali hii imewafanya waandishi makini wanaozingatia miiko na maadili ya
taaluma yao, kuwa wahanga wa vitendo viovu vya watawala, wakiwemo
askari polisi kama ilivyodhihirika hivi karibuni mbele kabisa ya
milango ya wakubwa wa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Ikiwa ni mwendelezo wa matukio ya namna hiyo ambayo yalifikia hatua ya
juu pale askari walipomuua kikatili Mwandishi Daudi Mwangosi, Septemba
2, 2012, huko Nyololo, Iringa

Tungependa pia kutumia nafasi hii Siku ya Amani Kimataifa, kuwatia
moyo ninyi waandishi wa habari kuendelea kutekeleza wajibu wenu wa
kijamii (social responsible journalism) kwa kuzingatia maslahi na
matakwa ya wananchi, tukiungana na Watanzania wengine wanaothamini na
kutambua uhuru wa habari kama moja ya mihimili muhimu katika ujenzi wa
demokrasia na hatimaye maendeleo na ustawi wa wananchi wote.

CHADEMA inaungana na Watanzania wote ambao wako sambamba nanyi katika
kuheshimu wajibu, majukumu na taaluma yenu, hususan katika kipindi
hiki ambapo vyombo vya habari na waandishi wanaojipambanua kwa umakini
wa kuwatumikia Watanzania, kama ilivyo kwa watu wengine makini kwenye
makundi mbalimbali ya kijamii, wanalazimika kupitia kwenye 'bonde la
kifo' linalotengenezwa na watawala waliopoteza uhalali na ushawishi wa
kisiasa, wakikabiliwa na hofu ya anguko kubwa kutoka madarakani.

Katika siku hii ya leo, tukiunganisha na mfululizo wa matukio ya
vyombo vya dola kugeuka kuwa adui wa raia na mali zao, ikiwemo
kushambulia waandishi wakiwa kazini, tunao wajibu wa kuwataka watawala
kutambua wajibu wa kitaaluma na uhuru wa waandishi wa habari kwa ajili
ya kuweka misingi ya amani na utulivu unaotokana na haki na matumaini.
CHADEMA ni moja ya wadau wa habari ambao wameweka saini kukubaliana na
Azimio la Dar es Salaam Juu ya Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji
(DEFRI), ambalo iwapo Serikali ya CCM ingekuwa imelikubali,
kulithamini na kulizingatia, leo hii lingeweza kuwa moja ya nyaraka
zinazotutambulisha duniani kama taifa linalotukuza haki, matumaini,
uhuru na uwajibikaji kwa ajili ya wananchi.

Tumeomba kukutana nanyi leo ili tuweze kutoa kauli juu ya Siku ya
Amani Kimataifa, sambamba na yanayoendelea kuhusu Azimio la Mkutano
Mkuu wa Chama; kufanya maandamano na migomo ya amani nchi nzima isiyo
na ukomo kupinga ufisadi unaofanywa na Bunge Maalum la Katiba, kupinga
uchakachuaji wa maoni ya wananchi unaoendelea kufanyika mjini Dodoma
na uvunjifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Katika muktadha huo wa Siku ya Amani Kimataifa, tungependa kuelezea
uhalali wa maandamano na migomo hiyo ya amani kama ifuatavyo;

Maandamano; Haki na Wajibu wa kikatiba;

Kwanza kabisa, Watanzania wote wanawajibika kwa mujibu wa Katiba ya
Nchi, Ibara ya 27 (1)-(2), ambayo inasema;

"(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya
Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa
pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine. (2) Watu
wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya
pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha
uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya
baadaye ya taifa lao."

Azimio la Mkutano Mkuu wa Chama la kufanya maandamano na migomo ya
amani nchi nzima lilizingatia takwa hili la Katiba ya Nchi.
Kinachoendelea huko Dodoma ni uharibifu na ubadhirifu wa mali na
rasilimali za umma. Ule ni ufisadi. Kwa sababu Katiba Mpya
haitapatikana kwa namna ile bunge linavyoendelea Dodoma. Hata Rais
Jakaya Kikwete amekubali hilo mbele ya viongozi wenzake. Ni wajibu
wetu sote kupinga Bunge la Katiba kuendelea.

Pamoja na ubovu wake ilionao, Katiba ya Nchi, katika Ibara ya 20 (1),
imetoa haki kwa mtu au watu kuwa huru kukutana, kuchanganyika na
kushirikiana na watu wengine kutoa mawazo hadharani.

Mikutano ya hadhara, migomo na maandamano hayo ya amani ya CHADEMA ni
sehemu ya mikusanyiko, ambayo ni haki ya kikatiba ya kila mtu au
kikundi cha watu.

Mbali ya haki hiyo kuwekwa bayana kwenye Katiba ya nchi, upo utaratibu
ambao umewekwa wa kuhakikisha haki hiyo inatekelezwa na wanayoitaka
katika kuhakikisha wanatoa mawazo yao kupitia mikusanyiko ya aina
mbalimbali.

Utaratibu ambao unavihusu vyama vya siasa mahsusi umefafanuliwa vizuri
kisheria, kupitia Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992, kifungu cha
11 ambacho kinasema hivi;

"11. --(1) Every party which has been provisionally or fully registered
shall be entitled-a) to hold and address public meetings in any area
in the United Republic after giving notification to the police officer
in-charge of the area concerned for purposes of publicizing itself and
soliciting for membership;"

"...(4) When a political party is desirous of holding a meeting or
procession in any open public place in any area it shall, not less
than forty eight hours before the meeting, submit a written
notification of its impending to the police officer in charge of the
area in which the meeting is to take place is situated.

(5) The written notification referred to in subsection (4) shall
specify--a) the name of the political party submitting the
notification; b) the place in and time at which the meeting is to take
place; c) the agenda or purpose in general of the meeting;".

Ndugu waandishi wa habari

Vipo vifungu vingine kwenye Police and Auxiliary Service Act ambavyo
navyo vinaweka utaratibu wa kisheria kwa makundi mbalimbali ya
kijamii, vikiwemo vyama vya siasa, kutekeleza haki hiyo, ambapo
kifungu cha 43 (1) kinasema;

"Any person who is desirous of convening, collecting, forming or
organizing any assembly or procession in any public place shall, not
less than forty eight hours before the time when the assembly or
procession is scheduled to take place, submit a written notification
of his impending assembly or procession to the police officer in
charge of the area specifying; (a) the place and time which the
meeting is to take place, (b) the purpose in general of the meeting;
and (c) such other particulars as the Minister may from time to time,
by notice published in the Gazette, specify."

Taarifa zote za CHADEMA ambazo zimetolewa kwa ajili ya mikutano,
migomo na maandamano ya amani kwa Jeshi la Polisi katika maeneo
mbalimbali kwenye ngazi za majimbo, wilaya na mikoa zimezingatia
wajibu wa kikatiba, matakwa ya kisheria.

Wakati watu wetu wakitimiza matakwa ya kisheria, Jeshi la Polisi
kupitia barua mbalimbali, mbali ya kukiri kuwa maandamano yetu ni ya
amani, limekuwa likitoa amri ambazo hazina msingi wa kisheria kuzuia
mikutano na maandamano hayo. Raia mtiifu kwa nchi yake hawezi kutii
amri isiyotokana na msingi wa kisheria. Kwa sababu ni batili.

Hivyo tunapenda kuwataarifu kuwa maandamano yetu ya kupinga ufisadi,
uchakachuaji kwenye mchakato wa Katiba na uvunjwaji wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba yako pale pale kuanzia kesho Jumatatu, Septemba
22 na kuendelea itakuwa ni wiki ya maandamano.

Ni vyema utaratibu huu tukaueleza na ueleweke vyema kwa sababu Jeshi
la Polisi nchini linatumia mamlaka lisilokuwa kikatiba wala kisheria,
kuzuia haki ya kikatiba ya wananchi kukusanyika na kuandamana dhidi ya
jambo ambalo linafanyika kinyume na maslahi au matakwa ya wananchi.

Wanachama wetu katika maeneo mbalimbali kama ambavyo tutawaonesha kwa
ushahidi hapa wa barua, wamefuata utaratibu huo wa kisheria ambao
unawataka kuwasilisha barua za TAARIFA kwa Jeshi la Polisi,
kuwataarifu polisi kuhusu kusudio la kufanya mkutano au kuandamana.

Tunaomba kusisitiza kuwa barua hizo ni za kutoa TAARIFA. Si kuomba KIBALI.

Pamoja na wanachama wetu katika maeneo mbalimbali ya nchi kutoa
taarifa kwa Jeshi la Polisi, bado wamekataliwa kutekeleza wajibu na
haki yao hiyo ya kikatiba kwa kisingizio cha kunyimwa KIBALI.

Neno KIBALI, limekuwa likitumiwa na Jeshi la Polisi katika hali ile
ile ya matumizi mabovu ya madaraka na mamlaka wasiyokuwa nayo kisheria
wala kikatiba. Hakuna mahali popote kisheria ambapo wananchi au chama
cha siasa kinatakiwa kuomba kibali ili waweze kukusanyika au
kuandamana.

Jambo la pili ambalo tungependa kuzungumza hapa ni kusisitiza kuwa
tunaendelea na uratibu wa maandamano ya nchi nzima, ambayo sasa
tumepanga yaendelee kuanzia kesho Jumatatu.

Tunafanya hivyo kwa sababu ni wajibu na haki yetu ya kikatiba, baada
ya kuwa tumefuata utaratibu wa kisheria ambao ni kutoa taarifa kwa
mamlaka husika. Tunapenda kuwaambia Jeshi la Polisi kuwa matumizi ya
neon hilo 'kibali' ni ubatili kisheria na si sahihi kutii amri
isiyokuwa na msingi katika sheria.

Kulaani kupigwa waandishi wa habari

Tunatumia fursa hii, kwa mara nyingine tena, kutoa kauli ya chama
kulaani kwa nguvu zote kitendo cha Jeshi la Polisi kupiga waandishi wa
habari waliokuwa wakitimiza wajibu wao siku ya Alhamis wakati
Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe alipoitikia wito wa jeshi
hilo.

Kitendo hicho cha askari wa Jeshi la Polisi kuwashushia kipigo
waandishi wa habari mbele ya macho, masikio na milango ya wakubwa wa
jeshi hilo na Wizara ya Mambo ya Ndani, ni wazi kimetupeleka hata
nyingine katika kutaka mabadiliko makubwa ya kimfumo na kisheria
kuhusu utendaji na usimamizi wa Jeshi la Polisi nchini.

Kitendo hicho kinachopaswa kulaaniwa na kila mpenda demokrasia na
maendeleo, anayeamini katika uhuru wa maoni na fikra mbadala,
kilitokea siku moja tu baada ya Makamu wa Rais (mkuu wa nchi kwa
wakati huu) kuwa amekutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini
pamoja na Vyombo vya Dola, akitoa wito kuwepo na maelewano kati ya
pande hizo mbili wakati wa utekelezajiwa majukumu yao.

Tangu juzi tumemtaka Makamu wa Rais kujitokeza hadharani kuuambia umma
wa Watanzania kama alitoa maelekezo mengine baada ya kuachana na
wanahabari, ambayo ndiyo yaliyotekelezwa na askari siku iliyofuata!

Tumemtaka pia IGP Ernest Mangu kutoa kauli ya hatua zipi amechukua
hadi sasa dhidi ya matukio mbalimbali ya askari polisi kushambulia
waandishi wakiwa kazini, huku tukimkumbusha tukio la kuuwawa kikatili
kwa Daudi Mwangosi katika mazingira yale yale kama ya juzi Makao Makuu
ya Polisi.

Ikiwa ni sehemu ya hatua za haraka, tunawashauri vyombo vya habari
nchini vikiwa kama mhimili wa nne, kuchukua hatua zifuatazo katika
kuupigania mhimili huo upate hadhi na heshima unayostahili;

1. Kufuatilia na kuhakikisha kwa hatua za kinidhamu zimechukuliwa
dhidi ya wale wote waliohusika katika kuwashambulia na kuwapiga
waandishi wa habari walipokuwa kazini wakitimiza wajibu wao.

2. Kufungua mashtaka; private prosecution kama sheria inavyoelekeza.

3. Kukusanya ushahidi wa wazi uliopo na kufungua kesi za madai, kudai fidia.

Imetolewa leo Septemba 21, 2014 na;
Kigaila Singo Benson
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda

No comments:

Post a Comment