Saturday, September 6, 2014

Chadema: Hatutarudia makosa 2010 Ukonga

 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa makosa yaliyofanyika mwaka 2010 katika Jimbo la Ukonga na kuchukuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), hayatajirudia tena.


Chama hicho kimesema hiyo inatokana na kujipanga hivi sasa kuhakikisha nafasi za serikali za mtaa mwaka huu na ubunge mwakani, zinachukuliwa na chama hicho.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Jimbo hilo, Juma Mwaipopo, baada ya kufanikiwa kuitetea nafasi hiyo kwa mara ya pili.

“Kutokana na kuipata tena hii nafasi kwa mara ya pili, sasa tutahakikisha CCM haishindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na ubunge mwakani baada ya kuyagundua makosa ya mwaka 2010," alisema.

Alisema Chadema ikiingia madarakani itahakikisha inasimamia mapato yanayopatikana na kwamba kwa sasa hakuna mwananchi anayejua mapato ya jimbo hilo.

Aliwataka wananchi kuachana na tabia ya mazoea na kinachotakiwa ni kufanya uamuzi ili Chadema iingie madarakani na watafanikiwa kuwa wanajua mapato ya Jimbo.

Alisema kuwa watendaji wa serikali za mitaa watakuwa wakitoa huduma bure kwa wananchi na siyo kama ilivyo sasa.

Alisema atatumia nafasi aliyonayo kwa kuhakikisha panakuwa na umoja ndani ya Chama na hali hiyo itasaidia kuiondoa CCM madarakani.

Naye Mwenyekiti wa Jimbo hilo, Thomas Nyahenge, alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa, jimbo hilowatashinda kwa asilimia 80.

Hata hivyo, aliwataka wana-Chadema kuvunja makundi yao ili chama chao kizidi kwenda mbele.

No comments:

Post a Comment