Thursday, April 3, 2014

Moto wa Wenje wawababua wajumbe wanaodaiwa kuhongwa

Katibu  wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti (Raawu), mkoani hapa, Ramadhan Mwendwa, amewaandama baadhi ya wajumbe 201 wa Bunge Maalum la Katiba walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wanaotuhumiwa kutoa rushwa kwa wajumbe hao. 

Kwa mujibu wa Mwendwa, mawaziri na wajumbe hao wanatakiwa kuwaomba radhi wananchi kutokana na kitendo cha kukubali kutoa hongo kwa wajumbe na wajumbe hao kuikubali.

 “Baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 wametia aibu zaidi kwa kukubali kulishwa vyakula na kupewa pombe kwa lengo la kukubaliana na misimamo ya serikali mbili kutokana na msimamo wa chama tawala,” alisema.

Alisema kitendo cha mawaziri kuwaita baadhi ya  wajumbe hao na kukutana nao nyumbani kwao na kuwapatia vyakula ni dalili tosha kuwa walikuwa wakiwahonga. 

Alisema wajumbe hao hawajawatendea haki wananchi kwani kutokana na tamaa yao tayari wameishaonyesha udhaifu mkubwa na kuwasaliti wananchi.

 Mjumbe wa Bunge hilo, Ezekia Wenje, alidai Ijumaa iliyopita kuwa kuna baadhi ya Mawaziri ambao waliwaita wajumbe wa kundi la 201 majumbani na kuwapa chakula, pombe, maji na soda.  

“Nataka kuwauliza wajumbe wa kundi la 201 wao wana tofauti gani na wajumbe wengine, ikumbukwe kuwa mawaziri katika bunge hili ni sawa na wajumbe wengine, ni kwanini wawaite wakati huu ambao wanajua kuwa kuna jambo muhimu la mjadala wa kujadili Rasimu ya Katiba mpya?” alihoji.

 “Kitendo cha mawaziri kuwaita wajumbe majumbani kwao na kuwapatia vyakula na vinywaji ni kuwarubuni na kuwabadilisha mawazo, ikumbukwe kuwa inafahamika kuwa mawaziri wanatokana na chama tawala na chama hicho kina msimamo wa kupinga mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na serikali tatu,” alisema.

“Mbaya zaidi Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, ametoa msimamo wakati wa kulihutubia bunge kuwa kamwe msimamo wa chama ni serikali mbili, kwa mtaji huo ni wazi kuwa walikwenda kuongwa hata kama hawakupewa fedha, lakini kitendo cha kupewa chakula na vinywaji ni kuhongwa,” alisema

No comments:

Post a Comment