Friday, April 4, 2014

Chadema walia kuhujumiwa

Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka wananchi wa Jimbo la Chalinze kutorubuniwa na chama chochote kuuza vitambulisho vyao vya kupigia kura kwa kuwa kufanya hivyo ni kujinyima haki zao za kidemokrasia na kuuza utu wao.

Aidha, chama hicho kimedai kubaini njama zilizopangwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuvuruga uchaguzi huo mdogo wa ubunge Jimbo la Chalinze ili kufanya wizi wa kura siku ya uchaguzi.

Hayo yalisemwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Issa Mohamed alipokuwa akimnadi mgombea wa chama hicho kwenye uchaguzi huo, Mathayo Torongey katika maeneo ya Msata, Chalinze Mzee na Miono.

Alidai kuna vyama ambavyo makada wake wanapita katika nyumba mbalimbali kuwarubuni na kuwalaghai wananchi kuuza shahada zao ili wasikichague Chadema siku ya uchaguzi.

Kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Chalinze ziko ukingoni huku vyama vya Chadema, CUF na CCM vikionekana kuchuana vikali katika kampeni za mikutano ya hadhara na nyumba kwa nyumba.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Chalinze, Said Bwana Mdogo kufariki dunia.

No comments:

Post a Comment