Wednesday, March 12, 2014

Chadema yamtangaza mgombea ubunge Chalinze

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtangaza Mathayo Torongey, kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo Jimbo la Chalinze mkoani  Pwani.
Mchakato huo ulihusisha wagombea wanne waliojitokeza kuwania nafasi ya ubunge kupitia tiketi ya Chadema.

Torongey alipitshwa kwa kura 280 za maoni kati ya kura 485 zilizopigwa.

Mkurugenzi wa  Bunge na Halmashauri wa Chadema ambaye ni Mkuu wa Operesheni wa Jimbo la Chalinze, John Mrema, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana.
Alisema uchaguzi wa Jimbo la Chalinze ni muhimu kwa kuwa lina historia ya kuongozwa na Rais Jakaya Kikwete, kwa muda wa miaka 15.

"Hivyo Chadema imadhamiria kulichukua jimbo hilo ili  kutafuta changamoto zilizopo," alisema.

Aliongeza: “Leo (jana), tunakwenda wilayani Bagamoyo kuchukua fomu kwa ajili ya mgombea wetu wa ubunge Chalinze, ambaye ametoka katika familia maskini anayefahamu changamoto zinazowakabili,” alisema.

Kwa upande wake, Torongey alisema kuwa yeye ni mkazi wa Chalinze katika kijiji cha Ubena na ametokea katika familia maskini ya jamii ya wafugaji.

Aliongeza: “Zipo changamoto nyingi katika elimu na maji, lakini nitajitahidi kwa pamoja kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo,” alisema.

No comments:

Post a Comment