Thursday, March 6, 2014

Chadema wamripoti polisi Katibu CCM kutishia kuua

Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefungua jalada dhidi ya Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, Hassan Mtenga kikimtuhumu kutishia kujeruhi na kuua kwa njia ya maneno.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa jana, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema Taifa, Benson Kigaila alisema Mtenga amefunguliwa jalada namba IR/RB/2014   katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Iringa.
"Leo (jana) tunakutana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi tukitaka kupata majibu ya lini Mtenga (Katibu wa CCM) atakamatwa, kuhojiwa na kisha kufikishwa mahakamani kwa kosa la kutishia kujeruhi na kuua kwa njia ya maneno," alisema na kuongeza:

“Kiongozi huyo ((anamtaja) alitoa vitisho hivyo kwa Ofisa wetu Mwandamizi wa Vikosi vya Ulinzi wa chama, Hemed Sabula na pia kiongozi huyo amekaririwa na vyombo vya habari akisema wanatuhumu na kazi iliyobaki kwa vijana wao baada ya kusema mkuu wao (anamtaja) ni kutekeleza tu." 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi alipotafutwa na NIPASHE ili kutoa ufafanuzi kuhusiana na madai hayo, alisema polisi inachunguza madai hayo na ikijiridhisha kwamba mlalamikiwa ametenda kosa hilo watamkamata na kumfikisha mahakamani.
Ni lazima kwanza tujiridhishe na kufanya uchambuzi wa kina katika hilo linalo lalamikiwa na Chadema lakini kimsingi vyama vyote vinatuhumiana na kutengeneza tetesi ambazo wanazisambaza. Ila tukiona yana ukweli mtu yeyote anayelalamikiwa na kufunguliwa mashitaka tutamkamata na kumpeleka mahakamani” alisema..
Kwa upande wake, Katibu wa CCM mkoani hapa, Hassan Mtenga alisema Chadema wanatapatapa kutokana na hofu ya kuanguka katika uchaguzi huo kwa vile walipotakiwa na polisi kupeleka ushahidi wa madai hayo hawajafanya hivyo.

No comments:

Post a Comment