Monday, February 17, 2014

Katiba mpya shakani

WAKATI Bunge Maalumu la Katiba likitarajia kuanza vikao vyake keshokutwa mjini Dodoma, upatikanaji wa katiba mpya upo shakani, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.
Wasiwasi wa upatikanaji wa katiba mpya unatokana na uwepo wa idadi kubwa ya wajumbe kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliopenyezwa kupitia asasi mbalimbali, ambao tayari wameweka msimamo wa kuyakataa baadhi ya mambo yaliyopo kwenye rasimu ya katiba, huku wakielekeza lawama kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Wakati CCM ikitarajiwa kutumia wingi wa makada wake katika Bunge hilo kupinga muundo wa serikali tatu uliopendekezwa kwenye rasimu hiyo, vyama vya upinzani vimeamua kubadilisha mbinu ya kukabiliana nayo.
Upinzani sasa umeamua kuelekeza nguvu zake katika kura za maoni ambazo ndizo zitakazoamua kile kilichokubaliwa bungeni kipite au kisipite, na sasa msisitizo mkubwa wa vyama vya upinzani kuikabili CCM umeelekezwa katika maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura. Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesharidhia kuboresha daftari hilo ili liweze kutumika wakati wa kura za maoni.
Wapinzani wamelenga kuuhamasisha umma kukataa kupitisha katiba mpya iwapo wajumbe wa CCM watapinga baadhi ya mambo ya msingi kwa sababu ya kuhofia kwenda kinyume na msimamo wa chama chao watakapokuwa bungeni.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa mchakato huo unaweza kuvurugika kama NEC haitaboresha daftari la kudumu la wapiga kura.
Hata hivyo, ikitokea CCM watatumia wingi wao kupitisha mambo yao bungeni, halafu wapinzani wakahamasisha wananchi kukataa rasimu hiyo kwa kuwa imepitisha mambo kinyume, wimbo wa katiba mpya unaoimbwa sasa huenda usifanikiwe.
Inaaminika kuwa zaidi ya watu milioni 5, hasa vijana, hawapo kwenye daftari hilo lililoboreshwa mwaka 2010.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alishaweka wazi kuwa kama NEC hawataboresha daftari hilo kabla ya kura za maoni, watazunguka nchi nzima kuwahamasisha watu wasusie mchakato huo.
Akizungumzia Bunge la Katiba na idadi hiyo kubwa ya makada wa CCM, Mbowe amenukuliwa akisema kuwa wamepokea kwa masikitiko uteuzi uliofanywa na rais, na sasa ni dhahiri kuwa rais na chama chake hawana nia njema ya kutaka katiba mpya.
Mbowe alisema CCM wamelenga kupata katiba yenye mawazo ya ki-CCM kwani katika uteuzi huo Rais Kikwete ameteua wajumbe ambao ni makada wa CCM kwa asilimia 75-80.
Alisema CHADEMA wapo tayari kushirikiana na wajumbe wote bila shida, lakini ikitokea CCM wanatumia vibaya wingi wao bungeni ili kupitisha mambo kinyume na ilivyopendekezwa na tume, basi CHADEMA watasusia Bunge ili CCM ipitishe katiba yao ambayo itakuwa sio katiba ya wananchi.
Mbowe aliwataka wajumbe wote wa CCM wasitumie vibaya uwingi wao ila wazingatie matakwa ya wananchi na kuyaheshimu kama yalivyoratibiwa na Tume ya Jaji Warioba.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa CCM imekuwa ikitumia udhaifu wa uboreshaji wa daftari hilo kupata ushindi kwenye chaguzi mbalimbali.
Wamedokeza kuwa chama hicho tawala kinatarajia katika kura za maoni nako kitumie mwanya huo huo kama daftari lisipoboreshwa ndiyo maana maboresho ya daftari la wapiga kura sio kipaumbele kwa CCM hadi sasa.
Hoja wanayoijenga wapinzani ni kuwa idadi kubwa ya vijana wanaounga mkono mageuzi hawamo kwenye daftari hilo, hivyo hawatokuwa na fursa ya kupiga kura ya maoni au kushiriki kwenye uchaguzi mkuu, na jambo hilo litaisaidia CCM kuendelea kushinda.
Wakati hali ikianza kuonekana tete juu ya mijadala ya Bunge hilo itakavyoendeshwa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, katika vikao vya Halmashauri Kuu (NEC), aliwahi kukaririwa akiwataka makada wenzake wajiandae kisaikolojia na mfumo wa serikali tatu.
Kauli hiyo ilitafsiriwa chama hicho kujawa na hofu dhidi ya kura ya maoni itakayopigwa  na wananchi.
Makada wenzake  waliweka wazi kuwa anaonekana kutishwa na upepo uliopo nje ya chama chao hali itakayoathiri msimamo wao ambao ni muundo wa serikali mbili.
Msimamo wa CCM wa kung’ang’ania serikali mbili, licha ya kupingwa na wengi, lakini pia unapingana pia na Katiba ya Zanzibar inayoitambua Zanzibar kama nchi, msimamo unaolazimisha wanasiasa wa upinzani kudai zaidi Tanganyika nayo itambuliwe.
Hoja ya kutaka Tanganyika nayo itambuliwe, inaungwa mkono na wanaCCM kwa siri, kwa kuhofia msimamo wa chama chao, na kama kura zitakazopigwa bungeni zitakuwa za siri, basi uwezekano wa kulazimisha serikali mbili hautapita.
Profesa Abdallah Safari alipoulizwa juu ya hali ya sasa na mustakabali wa katiba mpya, alisema anapata shaka na upatikanaji wake.
Alisema kwa hali ilivyo hadi sasa ni vigumu kusema moja kwa moja kama itapatikana katiba mpya kwa sababu ya muundo wa Bunge lenyewe ulio na asilimia 80 ya wabunge na makada wa CCM wasiotaka mabadiliko.
“CCM wanaweza kutumia wingi wao kupitisha mambo mengi bungeni, lakini daftari la kudumu la wapiga kura likiboreshwa wapiga kura wengi watakuwa ni vijana ambao wengi wao hawakubaliani na hoja za CCM, bali wanaunga mkono maoni yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba,” alisema.
Aliongeza kuwa uteuzi ungefanyika vema watu wangeanza kuwa na imani na Bunge, lakini umefanywa kiitikadi zaidi kwa wajumbe wake wanaotoka CCM kupitishiwa mlango wa uani kwa kutumia taasisi mbalimbali zikiwemo za dini.
Profesa Safari alibainisha kuwa utaratibu wa bungeni ukiwa wa kupiga kura za siri, suala la serikali mbili halitapita hata kwa wanaCCM wenyewe, lakini kura zikipigwa za wazi basi wajumbe wengi wataogopa msimamo wa chama chao.
Aliongeza kuwa kuna wasiwasi watapitisha kila kitu kinachotakiwa na chama chao, lakini wapinzani wakienda mtaani kwa wananchi watakataa tena kwa kura, maana kati ya kitu ambacho sisi tunataka sasa ni Tume Huru ya Uchaguzi itakayosimamia kura ya maoni.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema atakwenda bungeni kusimamia maslahi ya kitaifa kwa kujenga hoja.
Alisema majadiliano yote yatakayofanyika ndani ya Bunge yatasimama katika rasimu hiyo pamoja na muongozo wa tume, na kwamba kuna uwezekano wa kuongeza au kupunguza baadhi ya mambo yaliyo nje ya rasimu hiyo.
Alisema ndani ya Bunge siyo kila kitu kitakubaliwa. Yale yatakayokataliwa yataondolewa na yatakaoyoonekana yana msingi yataongezwa huku msingi mkuu ukiwa ni muongozo wa rasimu ya katiba.
“Tunaweza kufanya yote mawili huku tukiwa tunafuata muongozo wa rasimu ya katiba,” alisema Lipumba.
Akihutubia mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wa tafakuri na maridhiano kuelekea katiba mpya wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Tume ya Mbadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema kazi ya Bunge sio kwenda kubadili rasimu.
“Madaraka ya Bunge Maalumu yamekuwa yanabadilika kwa kutegemea aina ya mchakato unaotumika.
“Afrika Kusini, Namibia na Cambodia, Bunge Maalumu lenyewe ndilo lilipewa jukumu la kuandika rasimu ya katiba. Katika mazingira haya, Bunge Maalumu lilikuwa na madaraka ya kubadilisha mambo mengi katika rasimu ya katiba… lilikuwa na madaraka ya kuachana na rasimu ya katiba na kuandika rasimu mbadala.
“Madaraka ya Bunge Maalumu yanakuwa na mipaka endapo rasimu ya katiba imeandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au chombo cha aina hiyo.
“Bunge Maalumu linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya masharti yaliyomo kwenye rasimu ya katiba, lakini si suala la kawaida Bunge Maalumu kubadili hoja ya msingi. Jinsi ushirikishaji wa wananchi unavyokuwa wa wazi na mpana, ndivyo madaraka ya Bunge Maalumu yanavyopungua.
“Mantiki ni kuzuia Bunge Maalumu kunyang’anya madaraka ya wananchi, yaani “act of popular sovereignty,” alisema.

No comments:

Post a Comment