KATIBU MKUU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ameibua madudu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwamba vijana milioni nne watakosa fursa ya kupiga kura baada ya tume hiyo kushindwa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja kati ya NEC na viongozi wa vyama vya siasa nchini, Dk. Slaa alisema wamekuwa na mgogoro wa suala hilo kwa muda mrefu huku serikali na NEC ikishindwa kuboresha daftari hilo.
Alisema hadi sasa vijana zaidi ya milioni 2.5 waliofikisha umri wa miaka 18 wamenyimwa fursa ya kushiriki katika uchaguzi wa madiwani unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao huku serikali ikishindwa kuonyesha nia ya dhati ya kuwaingiza vijana hao kwenye orodha ya wapiga kura.
Alisema hakuna sababu ya msingi inayoelezwa na serikali na NEC kushindwa kuboresha daftari hilo kwani hivi sasa teknolojia imekua, hivyo kazi ya maboresho ya daftari hilo inaweza kufanyika kwa gharama nafuu na muda mfupi zaidi.
“Kama kuna nia ya dhati serikali inaweza kuboresha daftari hilo kila siku kuanzia ngazi ya chini hadi taifa…kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa vijana waliotimiza miaka 18 wamenyimwa haki yao ya kikatiba ya kupiga kura,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema inashangaza kwani hata tovuti ya NEC inaonyesha kuwa maboresho ya daftari hilo mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2007/2008, jambo ambalo si sahihi.
Alisema kutokana na hali hiyo ni wazi kwamba vijana wa kata 27 zitakazoshiriki uchaguzi wa madiwani hivi karibuni, hawajaandikishwa katika daftari hilo.
Profesa Lipumba naye alisisitiza kuwa vijana zaidi ya milioni nne ambao wametimiza umri wa miaka 18 hadi sasa, hawajaingizwa katika daftari hilo.
“Sheria inaitaka NEC iandikishe majina ya watu wasioingizwa katika daftari hilo kila siku lakini hadi sasa inashindwa kutimiza wajibu wake hata katika tovuti ya tume hakuna chochote kinachoonyesha juu ya daftari hilo,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo hata kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba vitambulisho vya uraia vitatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao haina ukweli wowote.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa tume haijaeleza wala kufafanua lolote kuhusiana na suala hilo na hata zoezi la vitambulisho hivyo kwa Jiji la Dar es Salaam halijakamilika hadi sasa.
“Rais Kikwete alitueleza kuwa Februari 11 Bunge la Katiba litakaa, Mei 10 kuna uwezekano wa kupitishwa kwa Katiba au kutopitishwa na ndani ya siku 74, yaani Julai 23 ni kura za maoni, je, NEC itaweza kuandaa utaratibu wa kuandikisha vijana huku wengi wakiwa wamepoteza vitambulisho vya kupigia kura?” alihoji.
Alisema kutokana na kukosekana kwa utaratibu makini ndiyo maana zoezi la uchaguzi linashindwa kufanyika ipasavyo.
Profesa Lipumba alisema kuwa demokrasia haiwezi kukuzwa ikiwa hakuna tume ya kuandikisha wapiga kura.
Aidha, Rais Mtendaji wa Chama cha APPT-Maendeleo, Peter Mziray, alisema kuwa suala la kuboresha daftari linapoteza muda na kupendekeza vitumike vitambulisho vya uraia katika kupigia kura kwani vitarahisisha mchakato wa Uchaguzi Mkuu mwakani.
“Kampeni zinazopigwa kabla ya wakati zitasabibisha ugomvi kwa kuwa kuna baadhi ya viongozi wameshaanza harakati za kujipigia kampeni mapema, hivyo tume iangalie suala hilo kwani kila chama kikianza mapema italeta shida,” alisema.
Aidha, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema kuwa daftari hilo liliboreshwa kwa mara ya mwisho kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010.
Alisema kuwa kutokana na ukosefu wa fedha NEC imeshindwa kufanya maboresho hayo katika uchaguzi huo na watakaoshiriki ni wale walioandikishwa awali.
“Watakaoshiriki ni wale walioandikishwa katika daftrai wakati wa uchaguzi mwaka 2010, hivyo wapiga kura waliohamia katika maeneo yenye uchaguzi na wale waliopoteza kadi zao hawatapata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi huo mdogo wa madiwani wa Februari,” alisema.
Alisema kuwa hivi sasa wapo katika mchakato wa kuboresha daftari hilo kwa uchaguzi ujao.
Mwenyekiti huyo alisema uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata hizo 27 unafanyika baada ya nafasi hizo kuachwa wazi kutokana na vifo, kujiuzulu na kuhama chama, zinazotoka katika halmashauri 23 za Tanzania Bara.
“Tume imeshatoa ratiba ya uchaguzi huo kuanzia siku wagombea watakapochukua fomu za uteuzi hadi siku ya kupiga kura hivyo vyama na wadau watazingatia ratiba hiyo na kuifuata kwa umakini ili kuepuka kupoteza muda na usumbufu,” alisema.
Alisema kuwa ni muhimu vyama vikazingatia maadili ili kuepusha vurugu, malumbano na matusi wakati wa kampeni.
No comments:
Post a Comment