TAARIFA
KWA UMMA
Rais Jakaya Kikwete
amwondoe Prof. Jumanne Maghembe nafasi
ya Waziri wa Maji kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka za kuongeza
upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es
Salaam na nchini kwa ujumla.
Rais Kikwete azingatie
kwamba tarehe 10 Januari 2014 nilimtumia ujumbe Waziri Maghembe kumshauri
ajiuzulu kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es
Salaam kinyume na maelezo yake ya uongo
aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.
Aidha, kufutia maelezo
yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es
Salaam (DAWASA) Hawa Sinare kuhusu sababu za kuchelewa kwa miradi ya maji
Jijini na majibu ya Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam
(DAWASCO) Jackson Midala kuhusu kujirudia kwa matatizo ya maji; Rais Kikwete
akumbuke ahadi yake ya kuitisha kikao Ikulu kujadili masuala maji mwezi Machi
2013 ambayo mpaka sasa hajaitekeleza.
Ikumbukwe kwamba mara
baada ya kujirudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam
niliwasiliana na mamlaka husika ziweze kuchukua hatua na pia nilitaka Wenyeviti
wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka zinazohusika na huduma ya maji jijini
(DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo kwa umma juu ya sababu za kweli za matatizo
za matatizo hayo.
Kwa nyakati mbalimbali
kati ya tarehe 10 na 14 Januari 2013 viongozi na watendaji mbalimbali wa DAWASA
na DAWASCO walitoa maelezo yenye kuonyesha kwamba matatizo ya maji Jijini Dar
Es Salaam yanayoendelea hivi sasa ni matokeo ya kudaiwa fedha za kulipia umeme
na TANESCO, uchakavu wa mitambo, kuchelewa kutekelezwa kwa miradi, wizi na
upotevu wa maji.
Rais Kikwete azingatie
kwamba maelezo yaliyotolewa yanadhihirisha kwamba Wizara ya Maji, DAWASA na
DAWASCO pekee hawawezi kukamilisha hatua za haraka hivyo mamlaka za juu
ziingilie kati kuepusha Serikali kuendelea kupata hasara, uchumi wa nchi
kuathirika na ugumu wa maisha kwa wananchi kuongezeka kwa kuzingatia kwamba
maji huduma ya msingi ya kijamii na malighafi muhimu katika uzalishaji.
Rais Kikwete arejee
hoja binafsi niliyowasilisha bungeni tarehe 4 Februari 2013 kuhusu hatua za
haraka za kuongeza upatikanaji wa maji safi na kuboresha ushughulikiaji wa maji
taka katika Jiji la Dar Es Salaam (Nimeambatanisha nakala ya sehemu ya hoja
hiyo inayohusu mapendekezo ya hatua nane za haraka).
Rais Kikwete atambue
kwamba ingejadiliwa na maazimio yote kutekelezwa matatizo ya maji katika Jiji
la Dar Es Salaam na nchini kwa ujumla mpaka hatua ya sasa yangekuwa yamepungua
katika maeneo mbalimbali kutokana na hatua ambazo nilipendekeza zichukuliwe.
Hata hivyo, badala ya
kuunga mkono hoja hiyo ambayo ingeisaidia Wizara yake na kurekebisha udhaifu uliokuwepo na hivyo
kumrejeshea imani kwa umma ambavyo ilikuwa imepungua; Waziri Maghembe akaamua
kinyume cha kanuni za Bunge kutoa hoja ya kuondoa hoja niliyowasilisha kwa
maelezo kuwa Serikali inaendelea vizuri na utekelezaji.
Kwa kuwa toka Februari
2013 mpaka Januari 2014 imebainika kwa nyakati mbalimbali kwamba utekelezaji
hauendi kama Serikali ilivyoahidi na kwamba kuna udhaifu wa usimamizi katika
ngazi mbalimbali ikiwemo wizarani, ni muhimu Rais amwondoe Prof. Maghembe kuwa
Waziri wa wizara hiyo.
Wenu katika uwakilishi
wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
14/01/2014
No comments:
Post a Comment