MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa chanzo cha Katiba mpya ni wapinzani, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mbowe alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Morogoro, ukiwa ni mwendelezo wa mikutano ya Operesheni ya M4C, iliyopewa jina la ‘Pamoja Daima’.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara mjini hapa, alisema kuwa ingawa mchakato wa Katiba ulianza muda mrefu kuanzia miaka ya 1992, lakini kasi ya kudai Katiba mpya ilikolezwa na CHADEMA mara baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
“Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, tuliahidi tukiingia madarakani tutaitisha mchakato wa Katiba ndani ya siku 100 ya utawala wetu. CCM walipoiba kura na kushinda, ndani ya Bunge tulisusia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete na kilio chetu kilikuwa mabadiliko ya Katiba,” alisema Mbowe.
Kwa mujibu wa Mbowe, baada ya CHADEMA kususia hotuba ya rais bungeni, kukawa na presha kubwa kutoka ndani na nje ya nchi kutaka Katiba mpya ndipo Rais Kikwete akakubali kuanzisha mchakato huo.
Alisema kuwa ameamua kueleza hayo kutokana na kuwapo kwa upotoshaji mkubwa kuhusu Katiba, ambapo baadhi wanasema ni CCM, wengine wanadai ni serikali na wapo wanaosema Rais Kikwete.
Kutokana na umuhimu wa Katiba, Mbowe alisisitiza kuwa kamwe CHADEMA haitakubali kuona mchakato huo unaishia njiani na Watanzania kulazimika kurudi kwenye Katiba ya sasa ambayo alisema imekosa uhalali wa kuongoza nchi.
Daftari la kupiga kura lina kasoro, Jeshi la Polisi la mauaji, polisi walitoka Moro kwenda kudhoofisha CHADEMA.
Makombora CHADEMA yaizindua NEC
Katika hatua nyingine kauli za kutishia kususia mchakato wa Katiba Mpya kama Daftari la Kudumu la Wapiga Kura halitaboreshwa, zimeizindua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na sasa imetangaza kuboresha daftari hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva, alisema jana kuwa NEC imeshaanza mchakato wa kuboresha daftari hilo baada ya kupata fedha kutoka serikalini.
Jaji Lubuva alisema kazi ya kuhakiki vituo vyote vya uandikishaji wa wapiga kura na vile vitakavyoongezeka kwa lengo la kuviweka karibu zaidi na wananchi, inaendelea.
“Tume inawaomba wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya suala hili, jukumu la kusimamia na kuendesha mchakato wa kuandikisha wapiga kura kisheria na kikatiba ni la Tume ya Taifa ya Uchaguzi vyombo vingine visiingilie shughuli zisizowahusu,” alisema.
Hata hivyo Lubuva alisema, kura ya maoni ya Katiba na Uchaguzi Mkuu ujao vitafanywa kwa kutumia daftari lililoboreshwa, hivyo wapiga kura wote wenye sifa ya kupiga kura pamoja na wale ambao watakuwa wamefikisha umri wa miaka 18 wataandikishwa kwenye daftari hilo litakaloboreshwa.
Lubuva alisema katika kuboresha daftari la wapiga kura, wale wote ambao wamefariki dunia wataondolewa kwenye daftari hilo.
Aidha, Jaji Lubuva alitoa ushauri kwa viongozi wa nyama vya siasa nchini kutowababaisha wananchi juu ya uboreshwaji wa daftari, badala yake wawahamasishe kuwa tayari kushiriki katika kura ya maoni na uchaguzi ujao.
“Kama tulivyoafikiana na viongozi wa vyama vya siasa Januari 9 ufanisi wa uchaguzi wowote katika nchi yetu unategemea ushirikiano wa wadau kwa kuzingatia katiba, sheria na kanuni za uchaguzi,” alisema.
Lubuva aliongeza kwa kutoa wito kwa wananchi kujitokeza na kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kujitokeza kupiga kura ya maoni kwa ajili ya katiba mpya na Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Uamuzi huo wa NEC umekuja baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Katibu wake Mkuu, Dk. Willbrod Slaa, kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiitisha NEC kwamba kama daftari hilo halitaboreshwa kwa ajili ya kura za maoni za Katiba Mpya, CHADEMA itafanya ziara nchi kuzuia wananchi wasishiriki kwenye mchakato huo.
CHADEMA ilisema kama daftari hilo halitaboreshwa vijana milioni nne wangekosa fursa ya kupiga kura.
No comments:
Post a Comment