Friday, December 27, 2013

Operesheni Tokomeza: Serikali kuwafukuza mawaziri wanne kazi haitoshi

Uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuwaachisha kazi mawaziri wanne Ijumaa, juma lililopita, umemsaidia kuiokoa serikali yake dhidi ya kupigiwa kura na wabunge ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wake.
Kama asingechukua hatua hiyo, Rais angekabiliwa na tatizo la au kuvunja serikali yake au yeye mwenyewe kupigiwa kura hiyo na hivyo kulipeleka taifa katika uchaguzi mkuu wa kuchagua serikali nyingine.

Mawaziri ambao Rais alitengua kuendelea kusimamia wizara zao ni aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, bwana David Mathayo, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, bwana Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, bwana Emmanuel Nchimbi na aliyekuwa Waziri wa Mali asili na Utalii, Balozi Hamisi Kagasheki.
Hata hivyo bwana Kagasheki ambaye ni mwanadiplomasia kwa taaluma, anaelekea ‘alitonywa’ na Rais kuwa ataondolewa hivyo akatumia mahusiano yake hayo ya karibu na Rais kutangaza kujiuzulu kwake bungeni kabla Rais hajatangaza uamuzi wake wa kuwaondoa mawaziri wengine watatu Ijumaa hiyo.
Pengine jambo la kusikitisha ni utetezi uliofanywa bungeni na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, bwana Mathayo ambaye alidiriki kudai kuwa anaonewa!
Huyu ni Waziri ambaye alipewa maagizo tisa na rais mwaka 2006, lakini mpaka alipoachishwa kazi Ijumaa alikuwa hajatekeleza hata agizo moja!

Kwa kujitetea kwake bungeni, Waziri huyo ameonyesha bayana kwanini hakupaswa kupewa kazi ya uwaziri! Katika utetezi wake bungeni, bwana Mathayo, alidai kuwa Wizara yake kuanzia mwaka 2006 imekuwa ikipewa fedha kidogo tofauti na zile ambazo ilikuwa ikiomba.

Lakini kwa bahati mbaya hakuonesha ni kwa namna gani amekuwa akitumia fedha hizo kidogo katika kutatua moja ya maagizo hayo tisa aliyopewa na rais! Hata hivyo, uamuzi wa Rais kuwaondoa mawaziri hao wanne hautakuwa na tija kama hatawaondoa pia viongozi wa Vyombo vya Dola ambavyo vimelaumiwa Ijumaa na wabunge kwa kuhusisha uvunjaji wa haki za binadamu; vitendo ambavyo vinafanana na vile ambavyo vilikuwa vikifanywa na makaburu wa serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini!

Viongozi wa Taasisi hizo wanaopaswa pia kufutwa kazi ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Wananchi na Jeshi la Kujenga Taifa, Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Mkugurugenzi wa Usalama wa Taifa na Kamanda wa Askari wa Wanyamapori.
Viongozi hao toka Taasisi nne nilizotaja, wanapaswa pia kuwajibishwa kutokana na usimamizi wao mbaya wa Vyombo vya Dola vilivyohusika moja kwa moja na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
Serikali pia inapaswa kuwashughulikia Makatibu Wakuu wote na wakurugenzi wao wa Wizara nne husika, pamoja na ile inayosimamia Utawala Bora, Wizara ambayo pia inasimamia Usalama wa Taifa.
Hata hivyo serikali pia inapaswa kuchunguza kwa kina yale ambayo yamekuwa yakiendelea, hususan katika Wizara ya Mali asili na Utalii, hasa katika eneo la vitalu vya uwindaji na kadhalika. Kumekuwa na madai lukuki ya rushwa katika eneo hili!

Ikumbukwe pia kuwa ni viongozi waandamizi wa wizara hiyo hiyo waliodaiwa kuhuhusika na utoroshaji wa wanyamapori kwenda Jamhuri ya Kifalme ya Uarabuni, UAE, mwezi Septemba, mwaka 2010 wakati umakini wa viongozi wa nchi ulikuwa umemezwa na shughuli za uchaguzi mkuu!
Kadhalika ni viongozi hao hao wambao walidaiwa kuhusika, kwa namna moja au nyingine na kashifa ya kuitenga Loliondo na kakabidhi sehemu nyeti ya eneo hilo kwa waarabu chini ya mkataba tata!
Suala la Liliondo linalokaliwa na mtoto wa mfalme wa UAE linapaswa kutafutiwa ufumbuzi sasa kwani wakati utakuja wakati Rais wa Tanzania wakati huo atapaswa kuwajibika!

Swali ambalo tunapaswa kujiuliza ni; Kwanini viongozi waandamizi katika wizara hii wana kiburi cha kutisha cha hata kutompa ushirikiano aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Balozi Kagasheki?

Wabunge siku ya Ijumaa walihoji Usalama wa Taifa walikuwa wapi wakati yote haya yalikuwa yakitokea. Mimi nauliza, Waandishi wa Habari na Vyombo vya Habari walikuwa wapi? Tutafakari!

No comments:

Post a Comment