Baraza la Vijana la Chama chama Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limesema litakilinda chama chao kwa nguvu na kwamba halitamvumilia atakayebainika kufanya vitendo vya kukihujumu.
Limesema kuwa uanachama ndani ya chama chao ni imani na siyo ushabiki, hivyo hawataruhusu mtu yeyote kuichezea hata kama mtu huyo atakuwa na umaarufu wa kupindukia.
Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Heche, alitoa kauli hiyo jijini Mbeya wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Chuo cha Uhasibu (TIA).
Alisema kutokana na imani hiyo, wapo watu ambao wamekipigania chama chao na kulazimika hata kufungwa gerezani huku wengine wakipoteza maisha ili kuhakikisha Chadema inajengeka na kuwa imara, hivyo kitendo cha aina yoyote kinachoonekana kukihujumu chama hicho ni sawa na usaliti kwa wale waliokipigania.
“Mpaka hapa Chadema ilipofika kuna watu wameumia sana, wapo waliofungwa gerezani, wapo waliopoteza mali na wapendwa wao na pia wapo walikufa kwa kuipigania Chadema iwe imara, chama hiki hivi sasa ni sawa na imani, haturuhusu mtu mmoja au kikundi cha watu wachache waichezee imani yetu, tutakilinda chama chetu kwa nguvu zote na tunawahakikishia kuwa tutawapoteza wachache, lakini meli yetu itavuka salama,” alisema Heche.
Alisema kuwa Chadema hakijajengwa kwa umaarufu wa mtu mmoja, bali kimejengwa na imani ya wananchi wote, hivyo hata kama kiongozi wao yeyote wa juu akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, wakionyesha usaliti nao watatemwa ili chama kisonge mbele.
Alisema mpaka sasa Chadema kimeonyesha njia ya kweli ya ukombozi, mwelekeo na tumaini kwa Watanzania na ndiyo maana kila uchaguzi unapofika lazima kiongeze idadi ya wabunge, madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa na Vijiji.
Aliongeza kuwa bila ya Chadema, uozo unaofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ufisadi unaofanywa na viongozi wa CCM usingejulikana na Watanzania wangeendelea kuwa masikini wa kutupwa huku rasilimali za nchi zikizidi kutanufunwa na kikundi cha watu wachache.
Alisema kuwa hata maamuzi yaliyochukuliwa na Kamati Kuu ya chama hicho ya kumvua nyadhifa zote Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, ni maamuzi magumu yenye kutaka kujenga imani ya chama hicho kwa Watanzania.
Alisema kuwa chadema kitaendelea kuchukua maamuzi kama hayo kwa kiongozi ama mwanachama yeyote atakayebainika kutaka kukiyumbisha kwa namna yoyote.
CHATO WAUNGA MKONO
Uongozi wa Chadema wilaya ya Chato, mkoani Geita, umesema unaunga mkono hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Chadema wilaya ya Chato, Mange Ludomya, alisema uamuzi wa viongozi hao kuvuliwa nyadhifa zao ni hatua madhubuti na ya kupongezwa.
Alisema viongozi hao kwa muda mrefu wamekuwa mzigo kwa chama hicho kutokana na kuendekeza siasa za kimakundi, hatua ambayo imekuwa ikisababisha mgawanyiko kwa baadhi ya viongozi na wanachama.
Ludomya alisema uamuzi huo ulifuata katiba ya Chadema Ibara ya 7:7.16 kifungu kidogo (v) Inayoeleza kuwa ina wajibu wa kumwachisha ujumbe wa Kamati Kuu mjumbe mteule ambaye atakwenda kinyume cha katiba, kanuni na maadili au kushindwa kukidhi matakwa ya kuteuliwa kwake.
Alisema maamuzi magumu yaliyochukuwa dhidi ya viongozi hao yataendelea kukiimalisha chama hicho kutokana na msimamo wake wa kusimamia ukweli badala ya kuendelea kuleana na kuoneana aibu.
KUSINI WAUNGA MKONO
Uongozi wa Chadema Kanda ya Kusini inayoundwa na mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi umeunga mkono maamuzi ya Kamati Kuu ya kuwavua uongozi Zitto, Dk. Kitila na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika soko kuu ya mjini Songea jana, Mwenyekiti wa Chadema wa Kanda hiyo, Matiko Matare, alisema maamuzi hayo wanayaunga mkono kwa kuwa ni sahihi.
Alisema Zitto awali alionekana mzuri, lakini baadaye ilibainika kwenda kinyume cha taratibu za chama na kupendekeza kwamba wanaomuunga mkono ikiwezekana waondolewe ndani ya chama kwa kwua wanaweza kukiteka.
WAZIRI AIPONGEZA CHADEMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, amekipongeza Chadema kwa utaratibu kilichoutumia kuwawajibisha viongozi wake kwamba ulikuwa ni mzuri na ulifuata taratibu za haki kwa pande zote.
Kombani alitoa kauli hiyo bungeni jana na kufafanua kuwa utaratibu wa kila upande kusikilizwa ni mzuri katika kutafuta makosa ya mtu.
Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) ambaye alitaka kujua kuhusiana na uamuzi wa serikali kuhamishwa kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kasulu (DMO), na kupelekwa mkoani Iringa huku akiacha tuhuma mbalimbali dhidi yake.
Aidha, katika swali lake la msingi mbunge huyo alitaka kujua ni sababu gani zinazoifanya Serikali kutowafukuza au kuwaachisha kazi watumishi wabadhilifu katika Halmashauri mbalimbali na badala yake baadhi wanahamishwa kutoka halmashauri moja kwenda nyingine.
Kombani alisema nidhamu katika utumishi wa umma iimewekwa kwa mujibu wa kisheria, kanuni na taratibu hivyo kama kuna ukiukwaji ni makosa na kuongeza kuwa mtu anapoachishwa kazi lazima taratibu husika zinafuatwe.
DK. SLAA ASUBIRIWA KIGOMA
Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Willibrod Slaa, ataanza ziara ya siku 20 katika mikoa ya Shinyanga na Kigoma, kuanzia leo hadi Desemba 23, mwaka huu.
Taarifa ya Chadema imesema lengo la ziara hiyo ambayo imetokana na maombi ya muda mrefu ya viongozi wa chama katika maeneo husika, ni kuimarisha na kukagua uhai wa chama katika majimbo ya mikoa hiyo.
Katika ziara hiyo, Dk. Slaa atakutana na wananchi katika mikutano ya hadhara ambapo atazungumzia masuala ya kitaifa na eneo husika, kisha atafanya vikao vya ndani na viongozi pamoja na wanachama.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, leo atakuwa Wilaya ya Kahama, kesho atakuwa Wilaya ya Kakonko, Jimbo la Buyungu na keshokutwa, atakuwa Jimbo la Muhambwe.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kibondo, Clavery Ntindyicha, alisema maandalizi ya kumpokea Dk. Slaa yanaendelea na kwamba, wananchi wamejipanga vizuri kwa mapokezi hayo wilayani humo.
Alisema wananchi wana hamu kubwa ya kumsikiliza Dk. Slaa kwa kuwa tangu afike wilayani humo katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hadi sasa hawajawahi kupata fursa hiyo.
Ntindyicha alithibitisha kuwa Dk. Slaa anatarajia kutembelea Jimbo la Buyungu kesho wakati katika Jimbo la Muhambwe atakuwa keshokutwa na kuongeza kuwa maeneo yote ni tulivu.
MWENYEKITI SINGIDA AJIUZULU
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, Wilfred Kitundu, ametangaza kujiuzulu akipinga uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwavua uongozi Zitto na wenzake.
Katika barua yake kwenda kwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Singida, Kitundu alisema jana kuwa: “Ninapenda kukuarifu kuwa nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya uenyekiti wa mkoa ambayo nimekuwa nikiitumikia kwa kipindi kirefu sasa kama kielelezo cha kuamini na kudai demokrasia ya kweli ndani ya chama.”
Aliongeza: “Ikumbukwe kwamba mimi ndiye mwanachama wa kwanza kujiunga na Chadema mkoa wa Singida na ni mwanachama wa 300 kitaifa, hiyo ni heshima kubwa sana kwangu na sipo tayari kuipoteza kwa kukubali kuwa sehemu ya udharirishaji huu wa demokrasia uliopitiliza.”
“Kwa barua hii basi, nimeonelea bora upate ufahamu huo kuwa si vema mimi kuendelea kupingana na dhamira yangu inayonituma kuwa mwanademokrasia wa kweli,” alisema.
KATIBU: CHAMA KIKO IMARA
Naye Katibu wa Chadema Mkoa wa Singida, Patrick Msuta, alisema hajapata taarifa rasmi za kujiuzulu kwa Kitundu, lakini amezipata kupitia kwa waandishi wa habari.
“Kimsingi alitakiwa aniandikie barua kuniarifu mimi, lakini hajafanya hivyo, badala yake, taarifa za kujiuzulu kwake nimezipata kwa waandishi wa habari, lakini taarifa kamili bado hajaniletea,” alisema Msuta.
Hata hivyo, alisema pamoja na Kitundu nafasi hiyo, chama bado kiko imara na kwamba, sababu za kujiuzulu alizozitoa ni zake binafsi.
OFISI YANUSURIKA KUCHOMWA ARUSHA
Watu wasiojulikana wamevamia ofisi ya Chadema mkoa wa Arusha na kuchoma moto dari na kuteketea vyumba viwili.
Tukio hilo limethibitishwa na Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini na Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa.
Alisema kuwa tukio hilo la kusilitisha lilitokea jana saa 12: asubuhi, baada ya mlinzi wao kuondoka, ndipo wahalifu hao walipoingia kwa uani na kutoboa dari na kuingia ndani.
“Lakini inaonekana alipopanda ndani alikata mawasiliano ya kengele (alarm system) na hili linafanywa na mtaalamu, hivyo huyu alikuwa
mtaalamu wa umeme, kisha akapanda chumba kinachofuata na aliposhindwa namna ya kupenya ndani, aliamua kuchoma moto,” alisema Golugwa.
Golugwa alisema kuwa baada ya kuchoma moto huo chumba hicho, dari yote iliteketea kuingia bafuni ambako uliteketeza dari yote na kuanguka chini, kisha moto kuzimika bila kuendelea vyumba vyenye mali za ofisi.
“Sisi tulipofika tukashuhudia maajabu ya Mungu, moto ulizimika bafuni na kompyuta na tarifa zetu muhimu zilikuwapo bila kuthirika na moto huo,” alisema.
Golugwa alisema kutokana na hali hiyo walilazimika kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi cha Ngarenaro na askari walifika.
Alipoulizwa sababu za mlinzi kuondoka bila ofisi kufunguliwa, alisema kwa kawaida mlinzi huondoka mapema baada ya kupandisha bendera ya chama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alipotafutwa kwa njia ya simu ya kiganjani, hakupatikana kupatikana kutokana na kuwapo kwenye kikao.
No comments:
Post a Comment