Wednesday, December 18, 2013

Dk. Slaa: JK ni dhaifu

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu ndiyo maana anashindwa kufanya mabadiliko ya mawaziri wabovu ambao sasa wanaitwa ‘mizigo’.

Alisema mawaziri mizigo hao ni dalili za tatizo katika uteuzi unaofanyika, ambao unafanywa bila kufuata vigezo vya uwajibikaji, uzoefu na badala yake unaangaliwa uswahiba.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Uyui, mjini Tabora juzi jioni, Dk. Slaa alisema kuwa kinachoendelea ndani ya serikali hivi sasa sababu si mawaziri mizigo moja kwa moja, bali hao ni dalili ya tatizo kubwa hususan katika mamlaka ya uteuzi, akisema uongozi makini unapaswa kushughulikia kiini au chanzo cha tatizo.

“Hii ni dalili ya wazi kabisa kuwa tuna rais dhaifu. Sasa ni mara ya pili Rais Kikwete anashindwa kufanya mabadiliko ya mawaziri wake wabovu, badala yake anaanza kwa kuzunguka zunguka,” alisema.

Dk. Slaa aliongeza kuwa CCM wanapaswa kuwaambia wananchi ukweli juu ya chanzo cha ubovu wa serikali yao kuwa unatokana na kukosekana kwa uwajibikaji kuanzia ngazi ya juu hadi chini, ambao hatimaye umesababisha ufisadi unaoangamiza maisha ya Watanzania na kuongeza umaskini, ujinga na maradhi.

“Tatizo lililopo ni kwamba wote wameoza kwa ufisadi. Hakuna anayeweza kumwajibisha mwenzake moja kwa moja kwa sababu kila mmoja anamfahamu mwenzake. Hivyo dawa ukitaka kufanya maamuzi unazunguka zunguka ili wanaotakiwa kuondoka waone aliyewateua si yeye aliyewaondoa. Huu ni udhaifu.

“Tuna tatizo kubwa la serikali butu. Serikali butu haiwezi kufanya uamuzi sahihi, muhimu kwa wakati. Haiwezi hata kuchukulia hatua mawaziri wabovu, wazembe au wasiowajibika kwa wananchi ipasavyo. Badala yake chama ambacho kimeunda serikali kinakwenda kutangaza majukwaani, wakati mamlaka ya uteuzi ipo kimya.

“Tunataka kuwaambia CCM, kama wanaendelea kudanganya wananchi, wananchi hawa wanajua mamlaka iliyowateua inaweza kuwa mzigo pia. Kwanini inakaa kimya, wakati rais ndiye anakaa na hiyo mizigo kwenye Baraza la Mawaziri. Sasa kama rais anaongoza mawaziri mizigo na yuko kimya, wananchi wamweleweje?” alisema.

Alisema kuwa amewasikia CCM wakilalamika kuwa kwanini mawaziri hawafiki katika maeneo ya pembezoni mwa nchi wakati wananchi wanahitaji huduma za muhimu kutoka katika wizara husika.

“CCM wanalalamika eti kwanini waziri hajafika mahali fulani, sijui Namtumbo huko. Sisi tumewaambia siku zote, majibu yake ni kuwa na serikali za majimbo. Huwezi kutegemea katika nchi kubwa kama Tanzania Waziri wa Kilimo aliyeko Dar es Salaam ndiye anaamua kila kitu, hata kwa mwananchi aliyeko mbali huko.

“Waziri wa Elimu au Ajira ndiye anayetegemewa kuamua kila kitu cha kisera ndani ya nchi, yeye yuko Dar es Salaam anatakiwa kuwaamulia watu wa Namtumbo, watu wa Tunduru, watu wote wanasubiri Dar es Salaam inasemaje, CCM wanalalamika nini?” alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa CCM isiwahangaishe Watanzania kuwatajia majina ya mawaziri mizigo pekee, kwani suala la msingi ni namna ‘mizigo’ hiyo inavyopatikana hadi kufikia nafasi hizo nyeti za utumishi.

Alisema kwa muda mrefu sasa chini ya utawala wa CCM katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete, kumekuwa na hoja ya uteuzi wa mawaziri, ambapo Dk. Slaa amesema haufanyiki kwa umakini na hauzingatii vigezo, bali uswahiba.

Alisisitiza kuwa mamlaka ya uteuzi ikiwa makini inapaswa kuchukua uamuzi sahihi kwa wakati kwa wateuliwa iwapo wameonekana wamekosea au hawawajibiki ipasavyo badala ya kuwazunguka na kuishia kuwataja majukwaani ikiwa ni njia ya kusukuma ajenda ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Akifafanua zaidi, Dk. Slaa alisema kuwa Serikali ya Rais Kikwete iache ubutu linapofika suala la kuwachukulia hatua watendaji au viongozi wabovu, kwani suala la uwajibikaji likipuuzwa au kutiliwa mkazo ni moja ya masuala ambayo ama yamefanya nchi nyingi duniani zishindwe au zifaulu kuwapatia wananchi wake fursa za ustawi wa maendeleo.

Dk. Slaa ambaye anaendelea na ziara ya kuimarisha na kukagua uhai wa chama hicho mkoani Tabora ambapo juzi alikuwa maeneo ya Ugoweko, Kakola na Tabora mjini, alisema kuwa hata mabadiliko ya mara kwa mara ya Baraza la Mawaziri katika Serikali ya Rais Kikwete yamekuwa hayana tija kwa Watanzania, ni dalili za tatizo kubwa la ukosefu wa uwajibikaji.

Wiki iliyopita Kamati Kuu (CC) ya CCM ilikutana mkoani Dodoma na kuwahoji mawaziri saba kuhusu madai mbalimbali ambayo wizara zao zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi.

Baada ya kuwahoji na kusikiliza utetezi wao, CC ilitoa ushauri kwa Rais Jakaya Kikwete ambao unaweza kuwa ni kuwafukuza, kuwabakisha au kuwabadili wizara.

Mawaziri wanaotajwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi, Celina Kombani.

Wengine ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Dk. Mathayo David pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda.

No comments:

Post a Comment