Wednesday, December 18, 2013

Chadema yawashauri wasomi waache woga

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  kimetoa changamoto kwa wasomi kama wana nia ya dhati ya kulisogeza taifa mbele kimaendeleo, waache  woga badala yake wachukue hatua pale wanapoona wanasiasa wanalikwamisha taifa.

Changamoto hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi wa Manispaa ya Tabora wakiwamo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Uyui mjini hapa.

Dk. Slaa alisema wasomi wa vyuo vikuu wanatakiwa  kuwa chemchem ya fikra, kuwa watoa dira wa taifa, kuipeleka taifa mbele pale ambapo taifa linakwamishwa na wanasiasa.

Dk.Slaa ambaye anaendelea na ziara yake ya siku 20 katika Mkoa wa Tabora baada ya kumaliza mikoa ya Kigoma na Shinyanga, alisema wasomi wanatakiwa kuwa watu wasiokuwa na woga kwani hata nchi zote za Ulaya zilizoendelea ni kwasababu ya wasomi wao hawakuwa waoga.

Alisema hivi sasa tatizo lililopo vijana wanakwenda haraka haraka wakitaka mabadiliko kuliko wazee ambao wanakwenda pole pole, hivyo ni lazima vijana na wazee ifike mahali wakutane katikati ili nchi isonge mbele kimaendeleo.

 "Nchi isiyokuwa na wazee haina baraka, nyumba isiyo na mzee na baba itavunjika, lakini pia nyumba isiyokuwa na mtoto itavunjika sababu mtoto ndiyo kiungo kati ya baba na mama," alisema.

Dk. Slaa alisema kumekuwa na ufisadi mkubwa ndani ya serikali na ndiyo maana taifa linarudi nyuma kimaendeleo badala ya kusonga mbele kama zilivyo nchi nyingine duniani.

Alitoa mfano katika bajeti iliyopita kuwa serikali ilitenga Shilingi bilioni moja kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa kitaifa, lakini hadi sasa hakuna kiongozi hata mmoja aliyekufa.

Kwa msingi huo alisema ni vizuri Watanzania wakajulishwa fedha hizo ziko wapi.

Dk. Slaa akizungujmzia kuhusu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), alisema hapa Tanzania hauwezi kufanikiwa kwa sababu nchi kama Malaysia ambayo inaendesha mpango kama huo imefanikiwa kwa sababu imewekeza katika elimu tofauti na hapa nchini.

No comments:

Post a Comment