Wednesday, December 25, 2013

Bunge la Katiba laiva

Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limesema litaongoza mkutano wa kuchagua majina ya watu 20 kutoka katika taasisi zisizo za kiserikali katika makundi yaliyoainishwa kisheria, yatakayopelekwa kwa Rais ili ateue kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
 
Mkutano huo utafanyika mkoani Dodoma, Jumatano ijayo.
Hatua hiyo inafuatia taaarifa ya Ikulu wiki iliyopita iliyozitaka taasisi hizo kuwasilisha majina ya watu wanaowapendekeza awateue kuwa wajumbe wa Bunge hilo.
 
Kaimu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda, alisema jana kuwa mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe 200 kutoka katika mikoa na wilaya zote za Tanzania Bara na Zanzibar.
 
 Wajumbe hao wameteuliwa kutoka katika makundi ya taasisi zisizo za kiserikali, kidini, elimu ya juu, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wakulima na vyama vinavyowakilisha wavuvi na wafugaji. 
 
Alisema katika kuwapata wajumbe 20 wa Bunge hilo, vigezo vya uwakilishi wa kikanda na kisekta vimetumika.
 
Mwakagenda alisema uwakilishi wa wajumbe kijiografia ni kutoka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kusini, Magharibi, Kaskazini, Kati, Pwani, Nyanda za Juu Kusini, Unguja pamoja na Pemba.
 
Alisema kwa upande wa uwakilishi wa kisekta, ni katika maeneo yanayogusa jamii moja kwa moja.
 
Kwa mujibu wa Mwakagenda, pia kutakuwapo wajumbe watakaowakilisha uchumi na maendeleo ya jamii, wazee na vijana, jinsia na wanawake, sheria na haki za binadamu, uwajibikaji na utawala bora.
 
 Pia kutakuwapo uwakilishi katika haki za watoto, vyombo vya habari, ardhi, maliasili, elimu, afya, na na kwa watu wenye Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi pamoja na dawa ya kulevya.
 
“Tukishachagua majina 20 ya ‘wajumbe’ hao tutamwandikia barua Rais ili ateue wajumbe tisa kutoka kwenye uwakilishi wa kijiografia yaani kikanda na 11 kuwakilisha sekta mbalimbali,” alisema Mwakagenda.
 
Alisema kutokana na mchakato wa kuwapata wajumbe na kuchelewa kuanza kwa Bunge hilo, itakuwa ni miujiza kupatikana kwa katiba mpya ifikapo Aprili 26, mwakani.
 
 Mwakagenda alisema katika masuala ya kidemokrasia na sheria ni lazima yawepo makubaliano ya pamoja na kupendekekeza uitishwe mjadala wa kitaifa kabla wananchi hawajapiga kura ya maoni, kwani bila kufanya marekebisho hayo katiba ikikataliwa itakuwa ni hasara kwa Taifa kutokana na gharama kubwa zilizotumika kuendesha mchakato huo.
 
 Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa mwisho wa kupeleka majina ya wajumbe hao ni Januari 2, mwakani.
 
 Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013, Bunge Maalumu la Katiba litakuwa na jumla ya wajumbe 635.
 
 Kati ya wajumbe hao, wanaotoka katika mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini ni 201, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni 358 na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ni 76. 
 
Kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, kati ya wajumbe 201 kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini, nusu watakuwa wanawake na nusu nyingine watakuwa wanaume.
 
Waziri Chikawe aliliambia Bunge katika Mkutano wake wa 13 kuwa kati ya wateuliwa 201, wanawake watakuwa 101 na wanaume 100.

 Endelea.....
Bunge Maalumu la Katiba, ambalo litafanyika kwa siku zisizozidi 70, linatarajiwa kuanza rasmi Februari, mwakani, kwa ajili ya kujadili na kuipitisha rasimu ya pili ya katiba iliyopendekezwa.
 
Rasimu ya pili ya katiba itakabidhiwa kwa Rais na baadaye itachapishwa katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine ndani ya siku 31.
 
Katika kipindi hicho, Rais ataitisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kupitisha rasimu iliyopendekezwa. 
 
Tume itakabidhi rasimu ya pili ya katiba kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Desemba 30, mwaka huu. 
 
Rasimu hiyo ya pili inatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume hiyo ilipotoa rasimu ya kwanza ya ambayo ilijadiliwa katika Mabaraza ya Katiba yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2 mwaka huu.
Rasimu ya kwanza ilizinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Juni 4, mwaka huu.
 
Baada ya rasimu ya pili kupitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, itaitishwa kura ya maoni, ambayo itatoa fursa kwa wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa.
 
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, yenye wajumbe 30; wakiwamo 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar, ilitangazwa na Rais Jakaya Kikwete, Aprili 6 na kuapishwa Aprili 13, mwaka jana. 
 
Ilianza rasmi kazi ya kukusanya maoni ya wananchi Mei mosi, mwaka jana. Baada ya kukamilisha kazi hiyo, iliyachambua na kuandika Rasimu ya Katiba.
 
Kazi ya kukusanya maoni hayo iliwahusisha wananchi mmoja mmoja kupitia mikutano ya hadhara na ilikamilishwa na Tume Desemba, mwaka jana.
 
Baadaye Tume ilikutana na makundi maalumu na watu mashuhuri, wakiwamo viongozi wakuu wastaafu na waliopo madarakani Januari 7-28, mwaka huu.
 
 Baadaye, mabaraza ya katiba yaliipitia Rasimu ya Katiba kuanzia Julai 12 hadi Septemba 2, mwaka huu na kutoa mapendekezo yake, ambayo yaliwasilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
 
Tume inaendelea kuyachambua kabla ya kukabidhi rasimu ya pili ya katiba kwa Rais Kikwete na Rais Dk. Shein mwishoni mwa mwezi huu. 

No comments:

Post a Comment