WAKATI Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ikiendelea na kikao chake jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, amekacha.
Zitto ambaye katika siku za hivi karibuni aliibua mjadala kwenye vyombo vya habari, hasa alipoingia kwenye malumbano na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amekacha kikao hicho na badala yake ametoa taarifa ya kusafiri nje ya nchi.
Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa iliyotolewa kwa wajumbe wa mkutano huo na Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe, ilisema kuwa Zitto yuko safarini nchini Sudan, lakini anatarajia kuhudhuria mkutano huo wakati wowote.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kinachofanyika kwenye Hoteli ya Blue Pearl, jijini Dar es Salaam zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe wameonyesha dhahiri kukerwa na hatua ya naibu katibu mkuu huyo kutoshiriki.
Waliolalamikia hatua hiyo walisema kuwa limekuwa jambo la kawaida kwa Zitto kutohudhuria vikao muhimu vya chama huku akijua fika kwamba yeye ndiye msaidizi mkuu wa katibu mkuu wa chama taifa.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho aliliambia gazeti hili kuwa moja ya ajenda zilizowasilishwa jana na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi ni kuhusu mapato na matumizi ya chama ambayo alidai ingefaa Zitto awepo kuisikiliza.
Mjumbe huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema ajenda hiyo ilikuwa muhimu kwa Zitto kuwepo kwani akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), amekuwa akidai kwamba CHADEMA na vyama vingine hawana hesabu za mapato na matumizi ya fedha za ruzuku wanazopata kila mwezi. Mkutano huo unaendelea leo.
No comments:
Post a Comment