MBUNGE wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), ameituhumu serikali kuwa inaongoza nchi kwa kaulimbiu na si mipango endelevu.
Wenje alitoa kauli hiyo bungeni juzi alipokuwa akichangia hoja ya mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2014/15 wakati Bunge lilipokaa kama kamati ya mpango huo.
“Hii ni serikali pekee duniani ambayo inafanya kazi zake kinyume, kutokana na mipango mibovu ambayo kila kukicha ni kaulimbiu na si mipango kabambe,” alisema Wenje.
Alisema Serikali ya Tanzania imekosa hata huruma ya kurudisha madaraka kwa wananchi na matokeo yake imebaki kung’ang’ania kila kitu yenyewe, jambo ambalo limesababisha malalamiko makubwa katika maeneo mengi.
Alitolea mfano wa kupanda kwa gharama za maisha ambako kunasababishwa na upandishaji holela wa bei za mafuta pamoja na hali ya kulindana kwa viongozi katika ununuzi wa vifaa vya kufanyia kazi.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema Tanzania ina mkosi na viongozi, kwani imekuwa ikipata viongozi ambao ni mabingwa wa kusafiri lakini wanachokwenda kufanya huko hawakijui.
Alisema baadhi ya viongozi walioko madarakani wamejaa kiburi na jeuri wakidhani hawatatoka madarakani.
Mbali na hilo, alisema ufuatiliaji wa utendaji kazi serikalini ni tatizo kwa kuwa wengi wa wafanyakazi wanatumia muda wa asilimia 20 kwa kazi za serikali wakati muda wa asilimia 80 wanafanya mambo yao.
No comments:
Post a Comment