MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemoni Ndesamburo (CHADEMA), amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Mhongo kuacha kuwakebehi Watanzania wanaoonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika sekta ya gesi.
Badala yake, amemtaka waziri huyo kufikiria namna ya kuwajengea uwezo kwa kuwatafutia mitaji kuliko kufikiria wawekezaji wa nje.
Ndesamburo ambaye pia anatajwa kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa nchini, alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wa hadhara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wenye lengo la kukijenga chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Kata ya Majengo, mjini hapa.
Alisema baadhi ya mawaziri wa Rais Jakaya Kikwete wameonyesha kupwaya katika utendaji kazi wao na kushindwa kusimamia maslahi ya Watanzania, na badala yake wamekuwa wakifanya kazi kwa kufikiria wageni wa nje kutokana na kile kinachodaiwa kupatiwa asilimia 10 katika uwekezaji.
“Hatupaswi kuwa na waziri anayewatusi Watanzania, kwamba hawana uwezo wa kuwekeza kwenye sekta ya mafuta na gesi. Waziri huyu anashindwa kuelewa kuwa baadhi ya wawekezaji hawa hawa watatumia ardhi hii hii kutafuta mitaji,” alisema Ndesamburo.
Alisema wapo Watanzania wenye uwezo wa kuwekeza katika vitalu vya gesi huku akiwataja Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi na Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji kwamba ni baadhi ya wafanyabiashara ambao wana uwezo wa kuweka mitaji yao katika sekta ya gesi.
“Hoja ya Regnald Mengi kutaka wazawa wapewe kipaumbele ni msingi wa mawazo unaoakisi mahitaji ya Watanzania wa kawaida. Hawa wamekuwa wakiwekeza hapa hapa nyumbani na faida yake tunaiona kwa sababu matunda yao yanaliwa na Watanzania wote,” alisema Ndesamburo.
Alisema hatua ya serikali kuwataka kwenda kujiunga na kisha kuingia mkataba na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ni porojo, na
kwamba lengo lake ni kutaka kuwabana mbavu wazawa ambao serikali haitaki wapewe vitalu vya uvunaji wa gesi na mafuta.
“Mengi anakuwa mtetezi wa Watanzania kuliko mwanasiasa Mhongo ambaye ndiye alipaswa kuwa na jukumu hilo. Tunasema kuna watu kama
Mengi, kuna watu kama Dewji, hawa wote wana uwezo wa kuwekeza kwenye gesi, eti tunaambiwa tujiunge TPDC kwenye shirika la umma, ni lipi shirika la umma Tanzania limekwishafanya kazi kwa faida?
“Tunajua mashirika mengi yamekufa, tunaona mengi ya mashirika ya umma yamekufa, eti leo wanatuambia tukatumbukie kule. Sisi tunaweza
kuungana na kina Mengi tukachanga thumni thumni zetu tukachimba gesi na faida ikabaki hapa hapa kwetu Tanzania kuliko kufikiria kuwatajirisha mataifa mengine.
“Badala ya kuwabeza, serikali ilitakiwa kukaa na wawekezaji hawa wa kizalendo na kujua uwezo wao, na kisha kufanya tathmini kama
hawawezi kuwekeza kwa asilimia 100 basi pajengwe mazingira ya kuwawezesha kuwekeza,” alisema Ndesamburo.
Alisema wazawa wanaweza kuzalisha kwa tija zaidi, kupunguza matumizi ya nishati ya kuni, mkaa na umeme kwa kuegemea gesi ambayo tunaizalisha wenyewe kulingana na mahitaji yetu.
Ndesamburo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, alisema wananchi ni mashahidi kwa baadhi ya viongozi waliopo
madarakani, kwamba kabla ya kushika madaraka ya umma wanakuwa watu wa kipato cha kawaida, lakini katika kipindi kifupi wanakuwa na utajiri wa kutisha.
Kwa kweli Muhongo anaonesha dhahiri kukosa upeo wa kifikra. Hafai. Ajiuzulu.
ReplyDelete