Thursday, November 7, 2013

Mnyika ahoji ukusanyaji wa kodi za majengo Dar

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika (pichani), amesema uhalali wa ukusanyaji wa kodi ya majengo unaoendelea jijini Dar es Salaam unatia mashaka kwa kuwa muda wa awali, ambao Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliruhusiwa kutekeleza jukumu hilo kufikia ukomo.

Mnyika alisema hayo wakati akiwasilisha maelezo binafsi juzi, kuhusu ukomo na udhaifu katika ukusanyaji wa kodi ya majengo jijini humo, bungeni juzi.

Alisema sheria iliiruhusu TRA kukusanya kodi ya majengo kwa niaba ya serikali za mitaa kwa muda wa miaka mitano, kuanzia Julai 2008 hadi Juni 2013.

Alisema pia waziri mwenye dhamana alizitangaza manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke jijini humo kuwa maeneo, ambayo TRA wangefanya kazi kwa kuanzia.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya uwakala, waziri mwenye dhamana anaweza kuongeza muda wa TRA kufanya kazi na pia kusitishwa kwa muda kunaweza kutokea tu iwapo halmashauri husika imejengewa uwezo wa kutosha katika ukusanyaji wa kodi. 

 “Muda wa awali ulifika ukomo wake bila ya Bunge na wananchi kupewa taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa kuziba ombwe hilo na hivyo kuweka mashakani uhalali wa ukusanyaji wa kodi unaoendelea katika Jiji la Dar es Salaam,” alisema Mnyika.

Alisema pia sheria ilimpa waziri mwenye dhamana kuandaa kanuni ambazo zingeongoza mwenendo wa TRA kwa upande mmoja na halmashauri zinzohusika kwa upande wa pili.  Kwa mujibu wa Mnyika, kanuni hizo ziliandaliwa na wataalamu na kuwasilishwa kwa waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa kwa hatua zaidi.

Lakini akasema hadi Juni, mwaka jana, ikiwa ni miaka minne tangu kukasimiwa kwa ukusanyaji wa kodi, mchakato wa kuidhinisha kanunihizo bado ulikuwa haujakamilika ikiwa ni pamoja na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.

Alisema kukosekana kwa kanuni hizo kumechangia udhaifu wa TRA na halmashauri katika kutekeleza majukumu yao yanayohusu ukusanyaji wa kodi za majengo katika jiji la Dar es Salaam. 

Mnyika alisema ingawaje uthamini wa mwisho wa majengo katika manispaa zote tatu ulifanyika mwaka 2006, mengi kuanzia kipindi hicho hayakuingizwa katika uthamini wa jumla, hivyo kukosekana kwa kumbukumbu na kusababisha wamiliki wake kulipa Sh. 10,000 kwa jengo kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment