MWENYEKITI wa Kamati ya Maliasili na Mazingira, James Lembeli, amesema wanaokamatwa na kuhusishwa na utoroshwaji wa nyara za serikali nje ya nchi ni vidagaa huku makambare yakiachwa.
Lembeli alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana na kupongeza juhudi za Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kwa kufanikisha kukamatwa kwa majangili hao.
“Waliokamatwa na wanaoendelea kukamatwa ni vidagaa, lakini makambare wameachwa, ingawa wanajulikana sasa ni vema wakakamatwa wahusika wenyewe na sio hao watumwaji,” alisema Lembeli.
Lembeli ambaye pia ni mbunge wa Kahama, alishauri ni vema operesheni ya Tokomeza Majangiri ikaendelea baada ya wao kumaliza uchunguzi na kubaini kasoro zilizojitokeza katika operesheni hiyo.
Alisema dunia nzima kwa sasa inapingana na kitendo cha ujangili na wanaiunga mkono operesheni iliyoanzishwa nchini hivyo ni vema pia serikali na wadau wengine mbalimbali wakaunga mkono juhudi hizo.
Hivi karibuni shehena yenye urefu wa futi 40 ilinaswa Zanzibar ikiwa na nyara za serikali ambapo hadi sasa watuhumiwa watano wamekamatwa huku uchunguzi ukiwa unaendelea kubaini wengine.
No comments:
Post a Comment