WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kujali itikadi za vyama vyao, jana waliweka kando tofauti zao na kuunga mkono mapendekezo ya serikali kwenye muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba mpya uliorejeshwa bungeni.
Muswada huo, ndio uliibua vurugu bungeni hadi kufikia hatua ya wabunge wa vyama vikubwa vya upinzani vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kususia mjadala na kupeleka hoja nje ya Bunge, wakimshinikiza Rais Jakaya Kikwete asiusaini kutokana na kasoro.
Rais Kikwete aliiona hoja ya wapinzani na hivyo aliwaita Ikulu kuzungumza nao pamoja na CCM, kisha akausaini muswada huo na kuafiki kasoro hizo zirejeshwe bungeni tena.
Akiwasilisha mapendekezo ya muswada huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisema serikali ilikubali kuongeza mambo matano.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, alitaja mapendekezo hayo kuwa ni kuongeza idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka 166 hadi 201.
Pendekezo jingine ni kuweka kiwango cha chini na cha juu cha idadi ya watu wanaopendekezwa kwa ajili ya kuteuliwa na rais.
Chana alisema mapendekezo mengine ni kutoa ruhusa kwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawawakilishi kufanya maandalizi yote muhimu kwa ufanisi wa Bunge Maalumu.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (CHADEMA), aliwataka wabunge kuhakikisha wanajenga umoja na mshikamano katika kujadili suala la katiba mpya.
Mbowe alisema suala hilo lisiwe jambo la ubinafsi wala la ukubwa au udogo wa chama.
Alisema awali jinsi muswada ulivyokuwa umeletwa bungeni, haukuwa na hali njema na ndiyo maana hata Bunge halikuweza kumalizika kwa mtazamo mmoja.
Mbowe alitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba isibezwe hata kidogo kwani kazi waliyoifanya ni kubwa kuliko kikundi chochote kilichohusika katika mchakato huo.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), aliitaka serikali kutoona hofu ya kuwa na wadau wengi katika kujadili katika Bunge la Katiba.
Mnyika alisema kwa pamoja wanakubaliana na muswada huo kutokana na mazungumzo na Rais Kikwete, na serikali kukubali kuongeza mapendekezo matano ambayo wapinzani walikuwa wakiyataka.
Tofauti na ilivyokuwa awali kwa wabunge wa CCM waliopitisha muswada huo wenyewe bila kuuchambua kwa vifungu, jana waliopata nafasi ya kuzungumza walitoa mapendekezo ya kuboresha huku wakiwapongeza viongozi wa vyama vya upinzani kwa kazi nzuri waliyofanya.
Wabunge hao, Rosemary Makilagi (Viti Maalumu), Magreth Mkanga (Viti Maalumu), Jenista Muhagama (Peramiho), Christopher ole Sendeka (Simanjiro) na William Ngeleja (Sengerema), walimpongeza rais pamoja na wenzao wa upinzani huku wakiunga mkono mapendekeo hayo ya serikali na kuleta nyongeza ya mapendekezo yao.
Hata hivyo wabunge hao, walipingana na wazo la kambi ya upinzani la kutaka idadi ya wajumbe iongezeke zaidi ya 201 wanaopendekezwa na serikali.
Nao wabunge wengine wa upinzani, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Mohamed Habib Mnyaa (CUF) na Kombo Khaji Kombo (CUF) waliwataka wenzao kutumia busara katika kujadili muswada huo ili kufikia muafaka.
Walisema kuwa hatua iliyofikiwa sasa ni nzuri, hivyo pale watakapotofautiana, kuna haja ya kutumia demokrasia ya wengi kwani mapendekezo takribani yote ya upinzani ni kama yamekubaliwa.
No comments:
Post a Comment