Wednesday, October 9, 2013

Waahirisha maandamano, mikutano nchi nzima

Vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, vimekubali kukutana na Rais Jakaya Kikwete, kwa ajili ya mazungumzo kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kutangaza kuahirisha maandamano yaliyokuwa yafanyike nchini kote kesho.



Maandamano hayo yalikuwa na lengo la kudai ushirikishwaji wa wananchi wa pande zote mbili za Muungano kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya nchi.

Uamuzi huo ulifikiwa na vyama hivyo ambavyo vipo kwenye ushirikiano wa kudai suala hilo na kupinga mchakato huo kuhodhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), siku moja baada ya Rais Kikwete kuanzisha mawasiliano na viongozi wa vyama hivyo, kwa nia ya kuandaa mkutano kati yake na wao.

Akisoma tamko la uamuzi huo kwa niaba ya wenyeviti wenzake wa Chadema (Freeman Mbowe) na NCCR-Mageuzi (James Mbatia) jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wamesitisha maandamano hayo baada ya kupata taarifa kuhusu Rais Kikwete kuwa tayari kukutana nao kwa mazungumzo.

“Jana (juzi), tumesoma kwenye vyombo vya habari kwamba Rais yuko tayari kukutana na sisi. Kwa kuwa ameafiki hilo, tumeamua kuahirisha maandamano na mikutano ya hadhara, badala yake tuzungumze na Rais,” alisema Profesa Lipumba.

Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema watayapima mazungumzo yao na Rais Kikwete kabla ya kuamua kuendelea na maandamano hayo au la.

Alipendekeza mkutano huo kati yao na Rais Kikwete upangwe mapema iwezekanavyo na kushauri ikiwezekana ufanyike Jumapili ya Oktoba 13, mwaka huu, kutokana na umuhimu wake.

Alisema baada ya Ikulu kutangaza uamuzi wa Rais Kikwete kuwasiliana nao, waliamini kwamba suala hilo ambalo ni kubwa lingekuwa limewekwa kwenye tovuti ya serikali.

Lakini akasema aliangalia kwenye tovuti hiyo ya serikali, ambayo hadi jana ilikuwa na taarifa ya tangu Juni 13, 2012 inayozungumzia Rais alikutana na wajumbe wa timu maalumu.

Rais Kikwete alianzisha mawasiliano na viongozi wa vyama vya siasa vyenye hoja kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa karibuni na Bunge kwa nia ya kuandaa mkutano kati yake na viongozi wa vyama hivyo.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari juzi ilisema kuwa mawasiliano hayo yalianza juzi kufuatia maelekezo ya Rais Kikwete kwa Ofisi ya Katibu wa Rais.

"Kwa mujibu wa maandalizi hayo, Ofisi ya Rais, Ikulu inaangalia uwezekano wa kuitisha mkutano huo Jumapili ya Oktoba 13 ama Jumanne ya Oktoba 15, mwaka huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu juzi.

Taarifa hiyo pia ilisema kufuatia matukio yaliyotokea bungeni wakati wa kujadiliwa na kupitishwa kwa muswada huo mwezi uliopita, na maneno na kauli mbalimbali, ambazo zimetolewa na wabunge wa vyama vya upinzani na wadau wengine kufuatia kupitishwa kwa Muswada huo na Bunge, Rais Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi Ijumaa iliyopita alisema hoja na kauli za wanaopinga Muswada huo zinazungumzika kwa nia njema ya kutafuta mwafaka katika mchakato wa kutafuta Katiba mpya.

Wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, walisusia na kutoka nje wakati wa kujadili na kupitishwa kwa muswada huo wakidai kuwa ulikuwa na kasoro kadhaa.

Kasoro hizo ni kutoshirikishwa kwa Zanzibar, madaraka ya Rais ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kuwasilisha Rasimu badala ya kuendelea kuwapo hadi kura ya maoni.

Vyama hivyo licha ya wabunge wake kususia Bunge, pia vimeunda ushirikiano wa kupinga mchakato wa Katiba kwa maelezo kuwa umehodhiwa na CCM.

Tayari wenyeviti wake, Profesa Lipumba, Mbowe na Mbatia wameshafanya mikutano ya hadhara jijiji Dar es Salaam na Zanzibar.

Awali, vyama hivyo viliandaa maadamano ya nchi nzima na baadaye kufanya mikutano mingine katika mikoa yote kuwashawishi wananchi waukatae mchakato huo.

Aidha, vyama hivyo na makundi ya wanaharakati wanamtaka Rais Kikwete asiusaini muswada huo kwa maelezo kuwa utaleta Katiba mbovu, ambayo haina maslahi kwa taifa.

WANAHARAKATI WAPIGA HODI IKULU
Makundi ya wanaharakati wamewasilisha hoja zao Ikulu wakimwomba Rais Kikwete asiusaini muswada huo.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba, alisema hoja za makundi hayo zimeandikwa katika kurasa 14.

Alisema baada ya kuwasilisha hoja hizo, walipangiwa muda wa kurudi Ikulu kufuata majibu na kupewa ahadi ya siku ya kuonana na Rais Kikwete kwa majadiliano zaidi.
Kibamba alisema walitakiwa kufika Ikulu jana au leo ili wapangiwe siku ya kwenda kuonana na Rais.

“Tumekwenda mara nyingi sana, lakini wanatuzungusha. Mwishowe wakatuambia tuandike hoja zetu tunazotaka kuzungumza na Rais. Tukaandika na kuwapelekea. Lakini wakatupangia tena tuje leo (jana) au kesho (leo) kupewa siku ya kuonana na Rais,” alisema Kibamba.

Alipoulizwa ni hoja gani walizoziorodhesha kwenye kurasa 14, Kibamba alisema hawezi kuzitaja kwa kuwa atakuwa amekwenda kinyume cha sheria na taratibu.

Alisema baada ya kuonana na Rais, wataitisha mkutano na waandishi wa habari kuwaeleza yaliyojiri.

Asasi zilizozoungana kwa pamoja na kupeleka hoja kwa Rais Ikulu ni pamoja na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), HakiElimu, Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT), Jukata, pamoja na Policy Forum.
NIPASHE

No comments:

Post a Comment