Friday, October 4, 2013

Sugu awataka Kigoda, Mgimwa Mbeya

WAKATI Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, akifanya jitihada za kuwapoza wafanyabiashara, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu, amesema mgogoro huo utaisha endapo serikali kupitia Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdalah Kigoda na Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, watakapokwenda kuwasikiliza wafanyabiashara hao.
Jana ikiwa ni siku ya pili ya mgomo wa wafanyabiashara hao, wakifungua maduka na kuishinikiza serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) igharamie mashine za kukatia stakabadhi, Kandoro alilazimika kukutana na viongozi wao na kuwataka waendelee na biashara zao wakati serikali ikitafuta ufumbuzi wa malalamiko yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalamu ya mkoa kukutana na viongozi wa wafanyabiashara hao na kujadili vurugu zilizotokea kwa siku mbili katika Soko la Sido-Mwanjelwa, Kandoro alisema kuwa wamekubaliana kwa kauli moja kuendelea na kazi na maduka kufunguliwa kuanzia leo huku mazungumzo yakiendelea kati yao na serikali.
“Madai yao ni ya msingi na ndiyo maana nilikutana nao siku tatu zilizopita, hivyo serikali imeyapokea na inayafanyia kazi.
“Hata mimi nafahamu kabisa kuna mambo mengine wanaonewa lakini licha ya hivyo, isiwe sababu ya wao kufanya mgomo na vurugu ambazo zinahatarisha usalama wa mkoa pamoja na mali zao,” alisema.
Kandoro alisema ni vema wafanyabiashara hao wakajenga desturi ya kufanya mazungumzo badala ya kugoma na kufanya vurugu ambazo zinahatarisha usalama wa mkoa.
Aliwataka kuwa na subira wakati wote huu ambao serikali inafanya mazungumzo na TRA, kwamba hali ya utulivu ikipotea hakuna atakayepona.
Kwa mujibu wa Kandoro, hadi kufikia Novemba 15 tarehe ambayo ilipangwa na TRA kuwa ya mwisho kila mfanyabiashara kuwa na mashine hiyo ya risiti za kielektroniki, muafaka utakuwa umepatikana.
Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Charles Syonga, alisema kuwa wamepokea kwa mikono miwili mazungumzo hayo na kwamba atafikisha taarifa hiyo kwa wenzake kuhakikisha wanafungua maduka na kuendelea na utaratibu kama kawaida.
Kuhusu vurugu za uchomaji matairi na kuzuia barabara kwa kupanga mawe, Syonga alisema kuwa suala hilo halijafanywa na wafanyabiashara bali watu ambao ni wapenda vurugu.
“Kimsingi sisi wenyewe hatupendi vurugu na ninaamini hazifanywi na mfanyabiashara yeyote, kwani katika mazingira ya kawaida tunapenda kufanya kazi zetu katika mazingira ya amani na utulivu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alisema kuwa tangu juzi jeshi hilo lilikuwa linawashikilia watu 105, lakini walifanya uchunguzi na kubaini kuwa 59 hawakuwa na hatia, hivyo kuwaachia huru huku watu 46 wakipandishwa kizimbani.
Tanzania Daima ilishuhudia polisi wakiendesha msako mkali katika eneo la soko la Sido wakiwa na gari lenye maji ya kuwasha huku wakiwataka watu wote waliokuwa ndani kutoka nje na kurejea makwao.



Sugu ang’aka
Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, ameitaka serikali ifanye haraka kuuingilia na kuumaliza mgogoro kati ya wafanyabiashara wa mkoani humo na TRA.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Sugu alisema mgogoro huo utaisha endapo serikali kupitia mawaziri wake, Kigoda na Mgimwa, wataenda kuwasikiliza wafanyabiashara hao.
Sugu alisema ameamua kutoa ushauri huo kwa serikali baada ya kuzungumza na viongozi wa wafanyabiashara hao ambao alidai pamoja na mambo mengine walimueleza kuwa wanataka kuonana na mawaziri hao.
“Nafikiri itakuwa busara kama serikali itawapeleka mawaziri hao ili waweze kuzungumza na wafanyabiashara hao ili kuupatia ufumbuzi mgogoro huu ambao sasa umechukua siku nyingi,” alisema.
Alisema hili la wafanyabiashara kutuma ujumbe kwa serikali kwa kufunga maduka ni ishara mbaya kwao na jamii nzima, kwani wanaoathirika zaidi ni wananchi wa mkoa huo ambao wanataka kununua mahitaji.
Aliongeza kuwa mawaziri hao watapaswa kuutatua kwa kina mgogoro huo kwa kuwa umeanza miaka mingi, hata hivyo sasa umeibuliwa na ununuaji wa mashine hizo za kielektroniki.
Aidha Sugu alilaani kitendo cha Mkuu wa Mkoa, Kandoro, kuzuia mkutano wa wafanyabiashara hao ambao ulikuwa ufanyike katika uwanja wa Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe juzi.
Mbunge huyo alisema serikali ya mkoa kupitia kwa Kandoro na polisi hawakuwa na sababu ya kuzuia mkutano huo ambao awali walikubaliwa ili waweze kujadili mambo yao.

No comments:

Post a Comment