Thursday, October 3, 2013

Lema kuongoza maandamano ya kudai maji kwa DC, RC

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amesema wakazi wa jiji hawapaswi kuiomba serikali huduma ya maji isipokuwa kuidai itekeleze wajibu wake na ili waweze kufanya hivyo, yupo tayari kuongoza maandamano ya amani kwa kwenda kwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa  wakiwa na ndoo tupu za maji.

“Nitaongoza maandamano baada ya maandamano ya kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Oktoba 10, mwaka huu, kudai maji…nimekuja kuwaelezeni kuwa hatuiombi serikali itupatie maji, tunaidai itupatie huduma hii ambayo ni haki yetu.

“Njooni na ndoo zenu tupu za maji ofisini kwangu, mimi najua wapi nitakakowapeleka kupata maji,” alisema na kuongeza, mtajaza maji ndoo zenu kutoka ofisi za watendaji wa serikali.

“Leo mnalalamika kutopata maji, shule na barabara, hii inatokana na woga, hampaswi kuiomba serikali huduma hizo, mnatakiwa kuidai, acheni woga,” alisema.

Alisema taasisi za serikali zinadaiwa na AUWSA Sh. milioni 346 deni ambalo linakwamisha usambazaji wa huduma za maji jijini Arusha.

Alisema serikali imeipandisha hadhi manispaa ya  Arusha na kuwa jiji, bila kupanua miundombinu ya maji na barabara ambayo ni ya zamani.

Lema alisema alishindwa kuonana nao kutokana na kupoteza muda mwingi mahakamani kwa kesi za kubambikiwa.

“Kwa zaidi ya miezi 18 nimepoteza muda mahakamani kushughulikia kesi za kubambikizwa, sijatumikia wananchi wangu kutokana na hila za watu,” alisema.

Hata hivyo, alisema, “ninachojivunia ni kuwajengea wakazi wa Arusha moyo wa ujasiri wa kudai haki zao.”

1 comment:

  1. kamandaa tuko pamopa,ngangamala mpaka kieleweke,

    ReplyDelete