Friday, October 11, 2013

Chadema wamjia juu Mangula

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Philip Mangula kutekeleza ahadi ya kuwashughulikia viongozi wa chama hicho walioingia madarakani kwa njia za rushwa badala ya kukibeza Chadema kuwa hakina anuani.

Chadema kimedai kuwa, Mangula muda mfupi baada ya kuanza ziara ya kichama jijini Dar es Salaam juzi, alianza kukibeza chama hicho ikiwamo kusema hajui anuani zao pamoja kuzungumzia ushindi wa Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Kwa mujibu wa Ofisa habari wa  Chadema, Tumain Makene, anuani yao siku zote ni nguvu ya umma inayotokana na uungwaji mkono ambao chama hicho kimeupata kutoka kwa Watanzania.

Alisema nguvu hiyo ya umma ndiyo inayowafanya wanachama na wapenzi wa Chadema wafungue ofisi na kujenga misingi na matawi ya chama katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam anakofanya ziara Mangula na nchi nzima.

Alisema kutokana na uungwaji mkono huo wa wananchi kwa chama hicho, ndiyo maana wananchi wa Jimbo la Kawe ambako Mangula anaishi na viongozi wengine waandamizi wa CCM na serikali wamemchagua kwa kishindo, Mdee kuwa mbunge wao.

No comments:

Post a Comment