Sunday, October 20, 2013

CCM wamsaliti Kikwete

WABUNGE WAVIMBIA MAREKEBISHO YA KATIBA
HOFU kubwa imetanda ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), juu ya upatikanaji wa katiba mpya, hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kusaini muswada ambao sasa ni Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba.
Mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni uliofanyika Ikulu Oktoba 15, 2013 umeongeza mpasuko ulioanza kujitokeza baina ya makada wa CCM na wapinzani.
Katika mkutano huo, rais na viongozi wa upinzani waliafikiana vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo.
Walikubaliana kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa katiba mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato huo kwa masilahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa.
Awali kabla ya mkutano huo, makada wa CCM wakiwamo mawaziri kadhaa waliweka wazi kuwa milango ya Ikulu imeshafungwa kwa wapinzani kuzungumzia suala hilo, lakini Rais Kikwete alipotangaza kukutana nao iliwaweka njia panda.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa baadhi ya makada wa CCM wamekuwa wakimshutumu Rais Kikwete kwa kuwabembeleza wapinzani huku akikiumiza chama chake.
Hoja wanayoijenga ni kuwa Rais Kikwete anataka kujijengea kitu cha kukumbukwa, hasa katika suala la katiba mpya bila kujali athari zinazokipata chama chake.
Makada hao wanaweka bayana kuwa hali hiyo itakiacha chama katika wakati mgumu wa kukabiliana na wapinzani wanaoonekana kuimarika kadiri siku zinavyoyoyoma.
Baadhi ya wabunge wa CCM wanamuona Kikwete kama msaliti kwa wabunge wake waliopitisha muswada huo, ambao sasa ni Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba, ukiwa na upungufu ulioainishwa na wapinzani.
Mmoja wa watu waliohudhuria mazungumzo ya Ikulu anasema rais aliridhia marekebisho hayo na alibainisha kuwa yajikite katika masuala kadhaa, likiwamo suala la Tume ya Warioba kuwapo kwenye Bunge Maalumu la Katiba, marekebisho katika suala la uteuzi wa wajumbe 166 ili idadi iongezeke na hoja ya Zanzibar kushirikishwa kabla ya muswada wa sheria ya kura za maoni kuanza.
Tayari Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, alishatoa tamko kuwashangaa wabunge wa CCM kwa kupotosha kifungu kilichokuwa kinasema Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa na rais mara tu baada ya kuwasilisha rasimu kwenye Bunge Maalumu la Katiba, msimamo ambao unaungwa mkono na Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala (CCM).
Mbunge huyo katika andiko lake alilolisambaza katika vyombo vya habari, anakiri kuwa moja ya upungufu alioubaini katika muswada ule ambao sasa ni sheria, ni kuiua Tume ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya mchakato kufikia mwisho.
“Kiukweli, lina mantiki ndani yake. Tukiwa kwenye Bunge la Katiba hakutakuwa na serikali, sasa ni nani atakayejibu na kuweka sawa hoja za wabunge? Hili kwa kweli wabunge tuliopitisha muswada ule hatukuliona vizuri,” alisema Kigwangala.
Wakati Kigwangala akiona upungufu huo, Naibu Spika Job Ndugai, aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa haoni udharura wa suala hilo kurejeshwa bungeni.
Ndugai amebeza suala la urejeshwaji wa sheria hiyo bungeni, akihoji kuwa suala hilo halina udharura.
“Ni ishu gani hasa ambayo wapinzani walienda kumwona rais ambayo inahitaji udharura huo? Je, kanuni za Bunge zinaruhusu suala hilo?” alihoji Ndugai.
Akizungumza na gazeti hili wiki hii, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema Bunge ni muhimili tofauti. Wabunge kama wataona kuna kitu cha kubadilisha watabadilisha, lakini wakiona hakuna cha kubadilisha itabaki ilivyo.
Kauli hiyo imeungwa mkono jana na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, ambaye alinukuliwa na gazeti moja nchini (si Tanzania Daima), akisema: “Serikali haikusudii kufanya marekebisho yoyote kwenye Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba iliyosainiwa na Rais Kikwete hivi karibuni.”
Mmoja wa wabunge wa CCM aliyehojiwa na gazeti hili na kutoa msimamo wake baada ya rais kusaini muswada kuwa sheria ni aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Hamad Yusuf Massauni, ambaye sasa ni Mbunge wa Kikwajuni.
“Mimi ningekuwa rais nisingepoteza muda kuongea na wapinzani, na hata kama sheria hii itarejeshwa bungeni, sioni sehemu yoyote ya kufanyia marekebisho, iwe ya kuondoa koma wala kuweka nukta,” alisema.
Kabla ya muswada huo kusainiwa kuwa sheria, Nape alinukuliwa na gazeti hili akisema: “Hofu yangu ni kuwa rais asiposaini muswada huo, ataingia katika mgogoro kikatiba, itabidi arejeshe muswada bungeni aeleze kwanini hajasaini, na ukirejeshwa bungeni wabunge wa CCM wakakataa kufanya mabadiliko, rais angelazimika kuvunja Bunge.”
Aliongeza kuwa: “Mimi ninaona afadhali rais asaini muswada huu ili kama kuna upungufu uwekwe mezani kama ilivyokuwa mwanzo, ila nakubali kabisa mzee Warioba ana hoja katika suala la kutovunjwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya kutetea rasimu mbele ya Bunge Maalumu la Katiba.”
Alisema wabunge wa CCM ni asilimia 74 ya wabunge wote, hivyo wakishikilia hoja ya kutobadilisha jambo lolote katika muswada huo baada ya kurejeshewa na rais, matokeo yake ni kuvunjwa kwa Bunge na nchi kuingia kwenye uchaguzi kabla ya 2015.
Nape alisema CCM haiko tayari kuingia kwenye uchaguzi kabla ya 2015, hivyo akawataka wanaopinga na kuunga mkono hoja hizo watumie busara na hekima kufikia maridhiano yatakayolijenga taifa.
Alisema kuwa muswada wa mabadiliko ya sheria wa mwanzo nao ulipitishwa ukiwa na kasoro mwaka 2011, lakini Chama cha Demokrasia na Maendeleo walienda kwa rais wakajadiliana wakakubaliwa, na kwamba viongozi wa CCM walilazimika kwenda Dodoma kuwaeleza wabunge msimamo wa Rais Kikwete na kuwashawishi waukubali.
“Tulipoona kuna hoja tulilazimika kwenda Dodoma kuwaomba wabunge wetu wakubali hoja za CHADEMA ili marekebisho yafanyike, ingawa suala hilo lilifanyika kwa taabu sana, sasa zamu hii wabunge wa CCM wanaweza wasikubali hoja za wapinzani, na likiendelea vile rais atalazimika kuvunja Bunge, hili suala limetuweka pabaya sana CCM, sijui hatima yetu,” alisema.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa iwapo serikali itaridhia marekebisho yaliyotajwa na wapinzani, mvutano mkubwa utazuka bungeni kati ya washindi na washindwa.
Jambo hilo linadaiwa halitakubaliwa na wabunge wa CCM ambao mara kwa mara wamekuwa wakishutumiwa kupitisha mambo kwa kuangalia zaidi masilahi ya chama kuliko taifa.
Kumekuwa na mipango ya CCM kumuandaa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, kuwa Spika wa Bunge la Katiba.
Inadaiwa Chenge ndiye atakayebeba jukumu la kudhibiti baadhi ya hoja zinazopingwa na CCM zilizotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.
Miongoni mwa mambo yaliyomo ndani ya rasimu ya katiba ni serikali tatu.

No comments:

Post a Comment