Ikiwa imebaki siku moja kabla ya vyama vya siasa kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kujieleza kuhusiana na hesabu zao kutokukaguliwa, vyama hivyo vimesema havijapokea barua za wito.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alimuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuwaandikia barua ya kisheria viongozi wa vyama tisa vinavyopata ruzuku ya Serikali kuwaita mbele ya kamati hiyo kesho kujieleza kwa nini hawajawasilisha ripoti za ukaguzi kwa Msajili kwa miaka minne iliyopita.
Hadi kufikia jana, ni Chama cha Wananchi (CUF) pekee kilichopata barua kutoka kwa Msajili inayowataka kuhudhuria kikao hicho.
Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, alisema hawajapokea barua yoyote kutoka kwa Msajili.
Alisema endapo hawatapata barua yoyote ya kutakiwa kuhudhuria kikao hicho hawata kwenda.
Hata hivyo, alisema wamepata barua ya mwaliko wa kukutana na Msajili ofisini kwake leo kuzungumza masuala mengine yasiyohusu PAC.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, alisema hawajapata barua yoyote kutoka kwa Msajili kuhusu wito na kwamba jana alikuwa Dodoma katika mkutano.
Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia kwa Ofisa Habari wake, Tumaini Makene, kilisema hakijapokea barua ya wito na kuwa hawatakwenda kama hawatapata barua.
NIPASHE lilipomtafuta Jaji Francis Mutungi, kueleza juu ya kutovitumia barua vyama hivyo jana, alisema hawezi kuzungumza kwenye simu na kumtaka mwandishi afike ofisini kwake kwa mazungumzo zaidi.
“Mimi siwezi kuamini kama nazungumza na mwandishi, njoo ofisini kwangu nami nitakupa majibu ya maswali yako uliyoniuliza,” alisema Jaji Mutungi.
Zitto anasema kuwa miaka minne iliyopita hakuna chama chochote kilichowahi kuwasilisha ripoti zake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kama vinavyopaswa kufanya kisheria, na kutishia kuvinyima ruzuku ya mwezi huu kama havitatekeleza hayo.
No comments:
Post a Comment