Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku amesema ipo haja kwa tume iwezeshwe kushiriki mchakato wa Katiba katika hatua zote zilizosalia, badala ya kubaki nje ya Bunge la Katiba kama washauri baada ya kukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba kwa Rais.
Butiku alisema licha ya umuhimu huo, tume haiwezi kulazimisha kushiriki kwake katika hatua za utunzi wa katiba zilizobaki na kwamba suala hilo linabaki mikononi mwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwapo litaifanyia marekebisho sheria husika.
Butiku ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, kuhusu mchakato wa uandikwaji wa Katiba Mpya, ambao umezua mivutano ya kimasilahi miongoni mwa makundi ya kisiasa.
Moja ya vipengele vya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa na Bunge Septemba, mwaka huu, kinaeleza kuwa baada ya kukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba kwa Rais, wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba hawatahusika tena na mchakato huo, badala yake watabaki kuwa washauri tu.
“Sisi (Tume) tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria, sheria kwanza ilisema tutafanya kazi mpaka mwisho, sheria ya sasa inasema tutaishia nje ya Bunge kama washauri. Sasa hayo ni mambo ya Bunge, lenyewe liamue wanayoyaamua, wakituhitaji kwenda (bungeni) kwa ushauri tutakwenda. Nadhani itakuwa vizuri hivyo, maana kazi hiyo siyo ya mmoja na inahitaji umakini mkubwa,” alisema Butiku na kusisitiza:
“Kama Bunge litaona inafaa hivyo, ndiyo kazi yetu hatuna kipingamizi, tutakwenda.”
Alitoa kauli hiyo baada ya kuhojiwa kuhusu kuwapo taarifa zilizodai kwamba wajumbe wote wa tume wamepanga kujiuzulu iwapo sheria iliyopitishwa na Bunge haitarekebishwa, ili kuwapa nafasi ya kisheria ya kufanyia kazi Rasimu ya Pili ya Katiba hatika hatua zote badala ya kubaki kuwa washauri.
“Na labda niseme tu kwamba tishio la wajumbe wa tume kutaka kujiuzulu halipo, tishio hilo halipo,” alisisitiza Butiku ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Aliongeza kuwa kilichoikasirisha tume ni mwelekeo wa makundi mbalimbali hasa ya kisiasa kuingilia mchakato wa Katiba, hali iliyoifanya tume kuamini kuwa vyama vilikuwa vimeanza kuvuruga mchakato huo.
Hata hivyo, alisema hivi sasa inaonekana kama kila mmoja amerejea kuheshimu sheria na kila mmoja anatimiza wajibu wake.
Mvutano wa kisiasa
Akizungumzia mvutano ulioibuka kati ya vyama vya upinzani na Serikali kuhusu baadhi ya marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria, Butiku alisema: “Mimi sitaki kusema kama huo ni mvutano, hiyo ni tofauti ya mawazo. Tusishangae, hamuwezi kufanya jambo kubwa namna hii la kujenga misingi ya taifa letu, kutazama Katiba yetu iweje, mwendesheje nchi yenu bila kutofautiana kimawazo.”
Mvutano wa kisiasa
Akizungumzia mvutano ulioibuka kati ya vyama vya upinzani na Serikali kuhusu baadhi ya marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria, Butiku alisema: “Mimi sitaki kusema kama huo ni mvutano, hiyo ni tofauti ya mawazo. Tusishangae, hamuwezi kufanya jambo kubwa namna hii la kujenga misingi ya taifa letu, kutazama Katiba yetu iweje, mwendesheje nchi yenu bila kutofautiana kimawazo.”
Aliongeza kuwa angeshangaa na kusikitika kama zisingekuwapo tofauti za mawazo kwa kuwa ndiyo afya ya mjadala wa Katiba Mpya, na kwamba ndiyo maana Rais Jakaya Kikwete ameamua kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani vinavyolalamika.
“Hiyo ndiyo afya ya mchakato, tofauti isionekane kama jambo la uhasama, nchi nyingine huwa na matendo mabaya zaidi, wanaweza kugombana hata kupigana, sisi hatujafanya hivyo, sisi tunajenga hoja. Kwa hiyo, hizo tofauti ni nzuri,” alisema Butiku.
Alisema hatua ya Rais Kikwete kuamua kukutana na viongozi wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF kuzungumzia mustakabali wa mambo yanayolalamikiwa na upinzani inafaa kupongezwa.
“Ni jambo zuri, ni vizuri tumpongeze Rais, anapenda mjadala kufikia mwafaka. Hii siyo kazi ya kikundi ni kazi ya Watanzania wote…; Siyo jambo ya mtu mmoja, ni jambo la mwafaka. Mwafaka unatokana na mazungumzo na Rais anakaribisha mazungumzo,” alisema Butiku lakini akatahadharisha:
“Ni vizuri wanaokwenda kuzungumza naye wazungumze vizuri, wajiandae vizuri kumsaidia Rais...Wazungumze na Rais wetu kwa hoja, wamsaidie na yeye awasaidie, wote tusaidiane.”
Kasoro kwenye muswada
Baadhi ya wanasheria wasomi wamesisitiza kuwa malalamiko ya wapinzani yana mashiko kwani ni dhahiri kwamba muswada uliopitishwa na Bunge ulikuwa na kasoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utafiti wa Mambo ya Uchumi na Umaskini (Repoa), Profesa Samwel Wangwe alirejea hoja ya kutoshirikishwa kwa wadau wa Zanzibar na kusema: “Katiba siyo mali ya chama cha siasa, Katiba ni mali ya Watanzania, hivyo ni lazima washirikishwe.”
Alisema kabla ya kuanza kutumia sheria ya mabadiliko ya Katiba, lazima upatikane mwafaka wa kitaifa na kusisitiza: “Katiba siyo mapambano na haitakiwi katika uandikwaji wake upande mmoja ujione uko sahihi kuliko mwingine. Tujenge mwafaka wa pamoja.”
Naye wakili maarufu nchini, Peter Kibatara alisema ili azma ya kuandika Katiba Mpya isiyokuwa na malalamiko itimie ni lazima viongozi wawe na utashi, maono, kuacha ubinafsi, kuweka masilahi ya wananchi mbele na kutafuta mwafaka wa pamoja.
“Wanasiasa wanatakiwa kuvua kofia zao za kisiasa na kuzingatia hayo niliyoyataja. Wakifuata hayo mchakato utakwenda vizuri na hakutakuwa na malalamiko,” alisema Kibatara.
Kwa upande wa mwanasheria wa Kampuni ya Uwakili ya Rwelu ya jijini Mwanza, Alfred Sotoka alisema Rais ameona kuwa wapinzani wana hoja za msingi na kukubali kwake kukaa nao meza moja ni jambo la busara.
“Hii siyo mara ya kwanza kwa Rais kukaa nao meza moja, hii ni mara ya pili toka mchato huu kuanza na tukumbuke kuwa mazungumzo ya awali yalileta mafanikio na kupatikana makundi ya kijamii ambapo walipata nafasi na kuunda Mabaraza ya Katiba na kupata fursa ya kutoa maoni yao,” alisema Sotoka.
Baadhi ya wasomi wanasema kuwa hatua ya Rais Kikwete kuamua kukutana na wapinzani inathibitisha kwamba Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba , utarejeshwa bungeni kwa ajili ya marekebisho, hata kabla ya kuanza kutumika.
Wakili Charles Semgalawe pia wa Dar es Salaam alisema alichofanya Rais Kikwete ni kukwepa kuvunja bunge na Serikali yake, hatua ambayo angelazimika kuichukua endapo asingesaini muswada huo.
Hata hivyo hadi sasa hakuna taarifa zozote kuhusu kusainiwa au kutosainiwa kwa muswada huo.
“Muswada wa sheria yoyote ukipitishwa na Bunge endapo Rais atakataa kuutia saini, maana yake lazima aivunje Serikali yake na uchaguzi uitishwe upya kwa hiyo alichofanya ni ujanja tu,” alisema Semgalawe na kuongeza:
“Ameamua kuwarudishia wabunge kile walichopitisha ili warekebishe, ukijaribu kuangalia ni sawa na amewarudishia matapishi yao wayale tena.”
Hata hivyo, alisema kuwa, hatua hiyo ya Rais Kikwete ni nzuri kwani angeweza kuamua kung’ang’ania kile walichopitisha wabunge wa chama chake hata kama hakina manufaa kwa taifa.
Vyama vya upinzani vilikuwa vimepanga kufanya maandamano Alhamisi wiki hii kushinikiza Rais kutosaini muswada huo, lakini vikaamua kuyasitisha baada ya Rais Kikwete kuwaalika kwenye meza ya mazungumzo.
Mbali na hoja ya ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, mambo mengine yanayolalamikiwa katika sheria iliyopitishwa ni nguvu ya Rais katika kuteua wabunge wa nyongeza 166 wa Bunge Maalumu la Katiba, idadi ya kura zinazohitajika kupitisha uamuzi katika Bunge hilo na suala kwamba Zanzibar haikushirikishwa.
No comments:
Post a Comment