Thursday, September 19, 2013

Wanaharakati wamtega JK

WANAHARAKATI nchini wamekubaliana kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete kumtaka asitie saini muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba kuwa sheria, vinginevyo wametishia kwenda mahakamani.
Mratibu wa masuala ya mchakato wa katiba mpya kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alieleza hayo alipokuwa akitoa mada kuhusu mchakato wa katiba mpya kwenye mjadala wa wazi ulioandaliwa katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia (TGNP) jijini Dar es Salaam.
Henga alisema endapo Rais Kikwete hatawasikiliza, watakwenda mahakamani kuzuia mchakato huo usiendelee kwani kisheria wanaruhusiwa kusimamisha kwa miezi sita.
“Tutoke na tamko hapa, tutakwenda kwa rais, ikishindikana mahakama itakuwa ni tiba kusimamisha mchakato kwa miezi sita,” alisema.
Katika hatua nyingine, Henga alisema kuwa Bunge Maalumu la Katiba ni muhimu kwa kuwa linaweza kubadili rasimu ya katiba ikawa nyingine kuliko kura ya maoni. Kwamba hilo ni Bunge maalumu kwa ajili ya kuandika, kupitisha au kutunga katiba.
Naye Dk. Azavery Lwaitama ambaye ni mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema mchakato wa katiba umedhihirisha kuwa wananchi wana mawazo ya kikatiba, kisiasa, kiuchumi na kifalsafa.
Alisema kuwa wameonyesha uwezo wa kuizungumzia katiba bila kuhitaji wanasiasa wala wanasheria.
“Kumbe kuna watu wanataka kuharakisha huu mchakato kwa kuwa wananchi wanaendelea kuelimika,” alisema.
Kwa mujibu wa Lwaitama, tume ya rais ya mchakato wa katiba inaweza kutoa mapendekezo ya kimapinduzi, kufanya kazi na kutoa mabadiliko yatakayomshinikiza arudie mchakato huo.
Mwanaharakati Mpendwa Chihimba, alisema kuwa bado kuna nafasi na sauti ya kuzungumza kuhusu katiba japo muda ni mdogo, hivyo iangaliwe hatua gani ichukuliwe ili kipande kilichobakia kiwe cha wananchi si wanasiasa.
Wakati huo huo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisisitiza kuwa katiba ni mama wa mambo yote, na kwamba ikiwa mbaya itavuruga kila kitu.
Mnyika alichangia hoja kuwa wabunge hawakupaswa kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba, hivyo alisisitiza wanaharakati na wananchi kupiga kelele kuhusu hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Ussu Mallya alisema kuwa mchakato huo usiharakishwe ili hoja hiyo ipelekwe kwa rais.

No comments:

Post a Comment