Wednesday, September 25, 2013

Tamwa wapendekeza umiliki ardhi uwe kwa Watanzania pekee

Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimependekeza Katiba ijayo itamke wazi kuwa mmiliki wa ardhi ni Mtanzania na ardhi isiuzwe bila ridhaa ya familia.

Mapendekezo hayo yalitolewa jijini Dar es Salaam na wakufunzi wa mafunzo ya Rasimu ya Katiba mpya watakaotoa elimu kwa wanawake juu ya namna ya kushiriki kuchangia mawazo yao katika mchakato wa kuandaa Katiba mpya unaoendelea.

Walipendekeza endapo mzawa ataolewa au kuoana na mgeni kutoka nje mmiliki wa ardhi au rasilimali atakuwa ni mzawa kwenye hiyo familia ili kuondokana na tatizo lililopo la ardhi kumilikiwa na wageni.

“Sheria itamke kuwa ardhi imilikiwe na mzawa peke yake na kila Mtanzania awe na haki ya kumiliki zaidi ya heka tano kwa ajili ya kuzalisha chakula kwani asilimia 65 ya chakula kinazalishwa na wanawake hivyo ni vyema wakapatiwa fursa za kumiliki ardhi,” alisema mmoja wa washiriki. 

Pia waliitaka Katiba itamke kuwa taarifa za uwekezaji ziwe wazi ili kuwafikia wazawa hasa wanawake kwani zimekuwa hazitolewi kwa wote.

“Watu wote wapewe haki ya kupata taarifa ambayo inawalenga wakiwamo walemavu kama viziwi, lengo ni Watanzania wote wapate taarifa ili kuzifikia fursa mbalimbali zinazotokea ,” alisema Valeria Msoka ambaye ni Mkurugenzi wa Tamwa.

Pia waliitaka serikali izingatie kutoa elimu ya jamii na ambayo itamuwezesha mtu kujitegemea pindi anapomaliza masomo na kuzingatia kikomo cha elimu ya sekondari badala ya shule ya msingi kama sasa.

“Katiba itamke kumpatia mtoto elimu hadi Sekondari na ambayo itamuwezesha kijitegemea na kuanzisha shughuli za maendeleo, sambamba na kuondoa mfumo wa uzoefu kazini kwani unawanyima vijana wengi fursa za ajira pindi wanapomaliza masomo,” alisema Gemma Akilimali.

No comments:

Post a Comment