JIBU LA SWALI LA MBUNGE MUHAMBWE
MBUNGE wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) amemshambulia mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema, kwa madai kuwa anajikomba kwa serikali ili apatiwe mafao makubwa ya uzeeni kutokana na wadhifa wake aliokuwa nao serikalini wakati huo.
Mkosamali alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa kuitaka serikali ieleze ni kwa nini inatoa mafao makubwa kwa viongozi wastaafu kama vile mawaziri wastaafu na marais wastaafu wakati wastaafu wa ngazi ya chini pensheni yao ni kidogo.
Mkosamali alitoa mfano huo wa Mrema kutokana na kuwa Naibu Waziri Mkuu, cheo ambacho alikipata wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, japo cheo hicho hakipo kikatiba.
Wakati Mkosamali akiuliza swali hilo, mwenyekiti wa kikao cha Bunge, Jenister Mhagama, alimtaka mbunge huyo afute kauli yake dhidi ya Mrema kwa madai kuwa si sahihi kumtaja mbunge aliyeko ndani na badala yake ajielekeze katika kuuliza swali analotaka.
Katika swali la msingi, mbunge wa Viti Maalum, Felister Bura (CCM), alitaka kujua kama kuna utaratibu wowote unaoandaliwa na serikali kuhakikisha kuwa ukokotoaji wa hesabu za wastaafu hautofautiani kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, alisema kinachosababisha wastaafu kwa ngazi ya Rais na mawaziri wakuu wastaafu kulipwa mafao makubwa ni kutokana na nafasi zao na kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja.
Alisema wastaafu hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira hatarishi na nyingi, ikiwa ni pamoja na heshima kubwa waliyonayo katika kulitumikia taifa.
“ Hatuwezi wastaafu wote tukawalipa viwango sawa na viongozi wastaafu kwa sababu serikali haina fedha za kutimiza hilo, na pia tunatakiwa kukubaliana kuwa lazima kuna matabaka,” alisema.
Naibu waziri alisema serikali imeunda Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambayo mbali na jukumu la usimamizi, pia hufanya kazi ya uhuishaji wa uwiano wa ukokotaji wa hesabu za mafao.
Alisema mifuko inayohusika na ukokotoaji wa hesabu za wastaafu ni Mifuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Pensheni wa mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa Serikali (GEPF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
No comments:
Post a Comment