Wenyeviti wa vyama hivyo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Freeman Mbowe (Chadema) jana walifika katika ofisi za Jukwaa la Katiba jijini Dar es Salaam na kujifungia kwa zaidi ya saa nne kwa mashauriano na viongozi wa Jukwaa hilo.
Viongozi hao walifika katika ofisi za Jukwaa la Katiba saa 4:15 asubuhi na kufanya kikao na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba, hadi walipomaliza saa 8:15 na baadaye kuzungumza na waandishi wa habari.
Wenyeviti hao katika tamko lao lililosomwa na Profesa Lipumba, walisema kuwa vyama hivyo vimeazimia kwa pamoja kuupinga Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba na wameanzisha utaratibu wa kuwatembelea wadau ili kujadiliana nao.
Profesa Lipumba alisema kuwa uamuzi wao wa kuungana ni kuhakikisha katiba haitekwi nyara na chama tawala ili Watanzania waweze kupata katiba mpya na nzuri ambayo imewashirikisha wadau wote.
Profesa Lipumba alisema ili kuhakikisha wanapata nguvu ya kupinga katiba hiyo, vyama hivyo vitatoa elimu ya uraia kwa wananchi wote ili kuhakikisha inapatikana katiba bora na yenye maslahi kwa wananchi wote na Taifa kwa ujumla.
“Tumeanzia kutembelea Jukwaa la Katiba kwa sababu jukwaa hilo limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Tanzania inapata katiba mpya iliyowashirikisha wanancho wote na baada ya hapa tutatembelea katika taasisi nyingine,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, wananchi lazima watambue kuwa suala la Katiba Mpya siyo la Chadema, CUF wala NCCR- Mageuzi, bali ni la Watanzania wote, hivyo wanatakiwa kuunga mkono ili kupata katiba nzuri.
Alitaja maeneo mengine watakayotembelea kuwa ni taasisi ya Walemavu ambayo wataitembelea kesho na kwamba Ijumaa watatembelea Ofisi za Shura ya Maimamu na Baraza la Waislamu Tanzania ( Bakwata) pamoja na Taasisi na Asasi nyingine.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba, alisema kuwa mchakato wa Katiba Mpya upo njia panda na kwamba na viongozi hao pamoja na mambo mengine wamepata fursa ya kuyaelewa vizuri matukio yaliyotokea Bungeni wakati wa Mkutano wa 12 ikiwa ni pamoja na hoja aliyotaka kuitoa Kiongozi Rasmi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, lakini alizuiwa na Naibu Spika, Job Ndugai.
“Wameanzisha mchakato wa kutoa elimu ya uraia na tutaendelea kufanya hivyo ili wananchi wajue, kwani mchakato wa sasa hauko sawa kwa kuwa pamoja na mambo mengine, Wazanzibari hawakushirikishwa,” alisema Kibamba.
Wabunge wa vyama hivyo walilazimika kutoka nje ya ukumbi wa Bunge Septemba 4, 5, na 6 wakipinga kuendeshwa kibabe na sheria na kanuni za Bunge kwa kuunyima upande wa Zanzibar haki ya kushiriki katika mchakato wa Katiba Mpya.
Jumapili iliyopita, vyama hivyo vilikutana na kutoa tamko la pamoja ikiwa ni pamoja na maazimio ili kuunusuru mchakato huo kuendelea kutekwa na kuhodhiwa na CCM kwa kuzingatia kwamba madaraka na mamlaka yote ya wananchi na serikali inapaswa kuwajibika kwa serikali.
Aidha, vyama hivyo viliazimia kuwa Septemba 21, mwaka huu vitaitisha mkutano wa hadhara wa pamoja kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam kuzungumza na wananchi sababu za kuupinga mchakato wa Katiba Mpya.
Kadhalika, vyama hivyo vilikubaliana kuwa baada ya mkutano wa Jangwani vitakwenda nchi nzima kuwaelimisha wananchi na kuwashawishi kuupinga mchakato huo.
Vilevile, vyama hivyo vinamuomba Rais Jakaya Kikwete kutousaini muswada huo uli kumwepusha kuwa sehemu ya kuandika katiba isiyo na maslahi kwa Watanzania wote.
No comments:
Post a Comment