Friday, September 20, 2013

Marekebisho Sheria Vyama vya Siasa yapingwa

Mchakato wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa umekumbana na kizingiti baada ya viongozi wa vyama hivyo kuupinga wakidai kuna ajenda ya siri inayofaywa na serikali kutaka kuvikandamiza vyama vya upinzani na hivyo wametaka mpango huo usitishwe haraka kusubiri katiba mpya ipatikane.

Viongozi wa vyama vya siasa walitoa msimamo huo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kujadili namna marekebisho ya sheria hiyo kwa lengo la kuboresha utendaji wa vyama hivyo. 

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, alisema kitendo cha kuamua kufanya marekebisho ya sheria hiyo wakati mchakato wa katiba mpya unaendelea kinaleta mashaka.

Pia alisema hata katika mambo yanayotaka kurekebishwa mengi yanavikandamiza vyama vya upinzani.

Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema anafahamu marekebisho ya sheria hiyo yalianza baada ya Chadema kuanza operesheni zilizozua mapambano baina ya wafuasi wake na polisi na hivyo wabunge wa CCM kutaka kufanyike marekebisho ya vyama vya siasa. 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema serikali ina njama katika marekebisho ya sheria hiyo kwa sababu katiba mpya bado haijafahamika kama itaweka muundo gani wa vyama vya siasa.

Alisema hata mabadiliko yanayotaka kufanyika yanataka kumfanya msajili wa vyama vya siasa awe kiranja na polisi wa vyama hivyo jambo ambalo vyama haviwezi kukubaliana nalo katika kipindi hiki, ambacho demokrasia inaendelea kushika kasi duniani.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Mziray, alisema katika mkutano wa vyama vya siasa uliofanyika miezi kadhaa iliyopita walikubaliana kuwa marekebisho ya sheria hiyo yasiwapo kwa sasa hadi hapo katiba mpya itakapopatikana, lakini msimamo wa ofisi ya msajili ni kwamba, marekebisho hayo yataendelea kufanyika taratibu.

Katika mkutano huo uliokuwa na mvutano mkali, mambo ambayo yanayotaka kurekebishwa, ambayo yanapingwa na viongozi wa vyama vya siasa ni pamoja na kuweka ukomo wa viongozi wa vyama kukaa madarakani na adhabu kwa viongozi wa vyama wanaokiuka katiba ya vyama vyao. 

Mengine ni kuweka muda, ambao Jeshi la Polisi linatakiwa kuwasilisha pingamizi la mkutano wa chama cha siasa, kupanga vyama vya siasa katika madaraja, kuweka muda maalumu wa uchaguzi kwa viongozi wa vyama vya siasa na vigezo vya kutoa ruzuku vijumuishe wenyeviti wa serikali za mtaa.

No comments:

Post a Comment