Wednesday, September 25, 2013

Lukuvi, Lissu kuumana

MNADHIMU wa Serikali Bungeni, William Lukuvi, ataumana na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, katika mdahalo wa kujadili ‘Bunge tulitakalo dhidi ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba’ uliopitishwa hivi karibuni.
Mdahalo huo utakaofanyika Ijumaa wiki hii katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, umeandaliwa na asasi ya kiraia ya kufuatilia mwenendo wa Bunge.
Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa asasi hiyo, Marcus Albany, alisema mdahalo huo umewekwa ili kuikutanisha mihimili ya Bunge na Serikali ili wananchi waweze kubaini nini hasa kinachobishaniwa katika muswada huo.
“Kumekuwapo na mvutano, kumekuwapo na sintofahamu, kule bungeni wabunge wanabanwa na kanuni, akilazimishwa kukaa anatii mamlaka ya kiti.
“Hapa tunataka tuwape uwanja mpana ili kila upande usikilizwe vya kutosha na wananchi, kwa kuwa suala la Katiba ni suala la wananchi, wabunge ni wawakilishi wa wananchi, hivyo tunataka tuje tujadili tuone wapi tumekosea na nini kifanyike kwa masilahi ya nchi,” alisema.
Albany alisema wazungumzaji wakuu katika mdahalo huo watakuwa ni Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) na Lukuvi, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge).
Wengine ni aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk. Charles Kitima, na profesa mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye bado walikuwa katika majadiliano naye.
Albany alibainisha kuwa katika mdahalo huo asasi mbalimbali za kiraia, vyama vya siasa, taasisi za elimu ya juu nchini, viongozi mbalimbali wa dini na wadau wanaopenda kuchangia mawazo yao kuhusu muswada huo wanaalikwa.
Tangu kupitishwa kibabe kwa muswada huo wenye kasoro nyingi, vyama vitatu vya siasa vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi vimeunganisha nguvu vikizunguka sehemu mbalimbali nchini kushawishi makundi mbalimbali na wananchi wamshinikize Rais Jakaya Kikwete asiusaini.

No comments:

Post a Comment