MCHAKATO wa uundwaji wa Katiba mpya uliotarajiwa kuleta umoja, amani na utulivu sasa umegeuka shubiri, baada ya kukithiri kwa mpasuko baina ya njia zinazotumika kuelekea upatikanaji wake.
Mnyukano wa kisiasa ulioanza kuonekana hivi sasa unalifanya taifa lipite kwenye hali tete ambayo wachambuzi wa masuala ya siasa wanalidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa busara na hekima isipotumika kuna hatari taifa likashuhudia vurugu kubwa.
Wakati hofu hiyo ikianza kujitokeza, viongozi wa vyama vya CHADEMA,NCCR-Mageuzi na CUF, jana walikwenda katika Ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kumueleza sababu za kupinga muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba na kumtaka Rais Kikwete asisaini muswada huo.
Tanzania Daima Jumapili imedokezwa kuwa mchakato huo umekiweka njia panda Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa Rais Jakaya Kikwete anayekabiliwa na shinikizo kubwa ndani na nje ya chama chake.
Uamuzi wowote atakaouchukua Rais Kikwete unadaiwa utakuwa na athari kwa chama chake ambacho hivi sasa wabunge wake wanasubiri iwapo hatausaini na kuurejesha bungeni ili ufanyiwe marekebisho yanayodaiwa na wapinzani.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili, tangu kupitishwa kwa muswada huo bila ridhaa ya wabunge wa upinzani umebaini kuwa kwa sasa CCM ni lazima iamue kuchukiwa na wananchi kama muswada huo utasainiwa na Rais Kikwete bila mabadiliko au kuondoka madarakani endapo rais akiurejesha muswada huo bungeni ufanyiwe marekebisho na wabunge wakigoma kufanya hivyo.
Kigogo mmoja wa CCM, amelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa hivi sasa chama chao kipo tayari kuchukiwa na wananchi kwa suala la muswada huo kuliko kuondoka madarakani kabla ya muda, ikiwa rais atalazimika kulivunja Bunge.
Inadaiwa kuwa kutokana na kasi ya upingaji wa muswada huo, Rais Kikwete atakuwa kwenye wakati mgumu ambapo kama atausaini ataweza kutoa maagizo ya kurekebishwa kwa vipengele vinavyolalamikiwa kama alivyofanya siku za nyuma.
Hofu kubwa imetanda kwa CCM baada ya tamko la hivi karibuni lililotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba akiwatuhumu wabunge wa CCM ingawa hakuwataja aliposema: “Sheria iliyounda tume hii inasema wazi kwamba ukomo wa tume ni baada ya wajumbe wa tume hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu kura ya maoni na mchakato wa kupiga kura hiyo utakapokamilika, lakini wao hawaoni sababu ya sisi kuendelea kuwapo hapa, nawaomba watafakari kipengele hicho”.
Kauli ya Warioba inafuatia muswada uliopitishwa hivi karibuni na wabunge wa chama hicho bila kuwapo wapinzani, kuwepo na kipengele kinachoivunja tume ya mabadiliko ya Katiba wakati rasimu itakapokuwa inajadiliwa na Bunge maalumu la Katiba, hivyo kusababisha rasimu ya Katiba kukosa watu watakaotetea mawazo ya wananchi yaliyoandikwa na kupitishwa na tume kabla ya kura ya maoni.
Wadau wa siasa wanasema endapo muswada huu utasainiwa na kuwa sheria bila kufanyiwa mabadiliko kuna uwezekano wa kikundi cha watu wachache kuweza kutumia mwanya huo kuingiza mambo ambayo hayajawekwa na tume ya mabadiliko ya Katiba kwa masilahi yao binafsi kwa kuwa tume itakuwa imevunjwa kwa kutumia udhaifu wa muswada unaoleta utata sasa kote nchini.
Hayo yote mawili yanazidi kukiweka Chama Cha Mapinduzi katika njia panda kwa kuwa kama rais atasaini muswada huo, CCM italazimika kuzunguka nchi nzima kutafuta ushawishi kwa Watanzania wengi wanaoonekana kuchukizwa na muswada huo uliopitishwa na wabunge wa chama hicho ukiwa na mapungufu ambayo hata Jaji Warioba tayari ameukosoa.
Pamoja na Jaji Warioba, viongozi wengine wa CCM waliotoa msimamo wao hadharani kusema kuwa wapinzani wapo sahihi katika hoja ya kutoivunja tume ili iweze kusimamia maoni ya wananchi wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, ni Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, ambaye amenukuliwa akisema anaona hatari mbele ya Tanzania ijayo.
“Naona hatari mbele ya Tanzania ijayo, suala la Katiba si la kufikiria walio wengi bungeni wanaweza kupitisha kwa wingi wao, na kama rais atasaini pasipo mambo ya msingi kushughulikiwa, basi aviandae vyombo mbalimbali viwe tayari kukabiliana na matokeo yatakayojitokeza.”
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alikaririwa wiki iliyopita akisema kuwa ni vema pande zinazopingana zikasikilizwa hoja zao ili kuepuka kuwaburuza wananchi katika suala la mchakato wa Katiba.
Kufuatia misimamo hiyo ya Jaji Warioba, Samuel Sitta, Kangi Lugola na baadhi ya asasi za kiraia kuhusu suala la kasoro ya muswada huo wa mabadiliko ya Katiba, endapo Rais atasaini muswada huo Chama hicho kitalazimika kujisafisha mbele ya wananchi kwa kutumia nguvu kubwa kwa kupitisha muswada wenye kasoro unaotia doa zoezi la mchakato wa madiliko ya Katiba.
Nape aeleza hofu ya CCM
Tanzania Daima Jumapili lilimtafuta Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kujua msimamo wa chama katika suala hili, Nape alisema: “Hofu yangu ni kuwa rais asiposaini muswada huo, ataingia katika mgogoro kikatiba, itabidi arejeshe muswada bungeni aeleze kwanini hajasaini, na muswada ukishakaa miezi sita wabunge wakaurejesha tena kwake atalazimika kuvunja Bunge. Mimi ninaona afadhali rais asaini muswada huu ili kama kuna upungufu uwekwe mezani kama ilivyokuwa mwanzo, ila nakubali kabisa mzee Warioba ana hoja katika suala la kutovunjwa tume ya mabadiliko ya Katiba kabla ya kutetea rasimu mbele ya Bunge Maalumu la Katiba”.
Alisema wabunge wa Chama Cha Mapinduzi ni asilimia 74 ya wabunge wote, hivyo wakishikilia hoja ya kutobadilisha jambo lolote katika muswada huo baada ya kurejeshewa na rais, matokeo yake ni kuvunjwa kwa Bunge na nchi kuingia kwenye uchaguzi kabla ya 2015.
Nape alisema CCM haiko tayari kuingia kwenye uchaguzi kabla ya 2015, hivyo akawataka wanaopinga na kuunga mkono hoja hizo watumie busara na hekima kufikia maridhiano yatakayolijenga taifa.
Kada mmoja wa CCM amelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa muswada wa mabadiliko ya sheria wa mwanzo nao ulipitishwa ukiwa na kasoro lakini Chama cha Demokrasia na Maendeleo walienda kwa rais wakajadiliana wakakubaliwa viongozi wa CCM walilazimika kwenda Dodoma kuwaeleza wabunge msimamo wa Rais Kikwete na kuwashawishi waukubali.
“Tulipoona kuna hoja tulilazimika kwenda Dodoma kuwaomba wabunge wetu wakubali hoja za CHADEMA ili marekebisho yafanyike ingawa suala hilo lilifanyika kwa taabu sana, sasa zamu hii wabunge wa CCM wanaweza wasikubali hoja za wapinzani, na likiendelea vile rais atalazimika kuvunja Bunge, hili suala limetuweka pabaya sana CCM sijui hatima yetu,” alisema.
Lipumba, Mnyika wafunguka
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemshauri Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu, Joseph Warioba, kuacha kuzungumzia uchakachuaji wa ukomo wa tume yake pekee bali kwenda mbele zaidi na kujadili upungufu uliopo katika muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko Katiba wa mwaka 2013.
Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya kikao cha pamoja na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mnyika, alisema kuwa Jaji Warioba alipaswa kwenda mbele zaidi na kutakiwa kujadili namna uchakachuaji wa vifungu mbalimbali vya sheria katika muswada huo ulivyofanyika.
Mnyika alisema kuwa wananchi na makundi mbalimbali yameporwa haki yao kwa kuwa uteuzi wa wajumbe 166 watakaochaguliwa na Rais Jakaya Kikwete ndio watakaoweza kuingia katika Bunge la Katiba.
“Wananchi wamechakachuliwa mamlaka ya Rais Kikwete ya kuteua wajumbe hao ilipaswa kufanywa na wananchi na si rais kama ambavyo muswada huo unavyosema, yote hiyo ni kupora haki za Watanzania,” alisema.
Pia mbunge huyo alisema kuwa kauli ya Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, haitawarudisha nyuma wala kuwafanya wasiendelea na mchakato wa kuwaeleza Watanzania juu ya uchakachuaji uliofanywa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kupitisha muswada huo.
“Tumemsikia Chikawe akisema kuwa Zanzibar pia haikushirikishwa, tuliamini kuwa kwa kauli hiyo angeweza kumshauri Rais Kikwete asisaini muswada huo lakini kwa vile amelewa madaraka hataki kufanya hivyo,” alisema.
Alisema kuwa upinzani wamedhamiria kwenda kwa wananchi kuwapa elimu juu ya muswada huo na kuwa uamuzi huo hautakoma.
Naye Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa wamekutana na Jaji Francis Mutungi na kumueleza juu ya ushirikiano wao na uchakachuaji uliofanywa na wabunge wa CCM juu ya muswada huo na sababu za kumuomba Rais Kikwete asisaini muswada huo.
Alisema kuwa walimjulisha Mutungi sababu ya kuwa na msimamo katika suala hilo na kutaka mwafaka ili kuweza kupata Katiba inayotokana na Watanzania.
Prof. Lipumba alisema kuwa hakuna sababu ya kuendelea na mchakato kwa kuwa kuna uwezekano wa Katiba hiyo kuwa ya chama kimoja.
Alisema ni vema kupata maridhiano katika suala hilo ili Katiba itakayopatikana itokane na Watanzania. “Kama Rais akisaini ina maana Katiba ya Watanzania itakuwa imekwama,” alisema.
Hata hivyo Prof. Lipumba aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 10, mwaka huu katika viwanja vya Jangwani ili kuwa na ushiriki wa kitaifa katika suala hilo.
“Tutafanya maandamano na mikutano ya amani na tutafuata taratibu zote za kisheria na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi,” alisema.
No comments:
Post a Comment