Sunday, September 29, 2013

Kamati ya Moyo yatoa masharti Katiba Mpya

Kamati ya Maridhiano Zanzibar imetangaza maazimio sita inayotaka yazingatiwe katika mchakato wa Katiba Mpya kabla ya Bunge la Katiba kujadili rasimu ya mwisho na kupigwa kwa kura ya maoni mwakani.
Maazimio hayo yametangazwa na kamati hiyo pamoja na Baraza la Katiba Zanzibar (Bakaza) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika huko Shangani mjini Zanzibar jana.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hassan Nassor Moyo, alisema kwamba marekebisho ya sheria hiyo yaliyofanywa na Serikali na kupitishwa na Bunge kibabe yana upungufu mkubwa katika utaratibu wa kuandaa muswada huo na uchukuaji wa maoni yake.
Alisema kuwa kabla Rais Kikwete hajasaini muswada huo, wadau kutoka Zanzibar wapewe nafasi ya kutoa maoni yao kisha urudishwe upya bungeni ili kujadiliwa na kupitishwa kwa manufaa ya pande mbili za Muungano – Tanganyika na Zanzibar.
Alifafanua kuwa kifungu kinachotoa nafasi kwa wabunge wa Bunge la Katiba kupitisha Katiba kwa wingi wa kura ikiwapo theluthi mbili zitashindikana kupatikana mara mbili, kifutwe, badala yake utaratibu wa awali wa kupitisha kwa kupata theluthi mbili kila upande utumike.
Mambo mengine yaliyopendekezwa na kamati hiyo, ni Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wawe idadi sawa baina ya Zanzibar na Tanzania Bara kwa sababu Katiba Mpya inayoandaliwa ni ya Jamhuri ya Muungano unaotokana na washirika hao wawili, ambao walikuwa na sifa sawa kabla ya muungano huo mwaka 1964.
Moyo alisema pia kuwa wajumbe 166 wa Bunge la Katiba kutoka makundi mbalimbali ya kijamii na asasi za kiraia wachaguliwe na makundi na Taasisi zenyewe, badala ya kazi hiyo kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kuwa Kamati yake inaunga mkono ushauri wa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wa kutaka viongozi wa kisiasa na makundi ya kijamii kukaa pamoja kuzungumzia mvutano uliojitokeza baada ya kufanyika kwa marekebisho ya muswada huo.
Upande wake Mwenyekiti wa Bakaza, Profesa Abdul Shariff alisema kuwa muundo wa Bunge la Katiba una walakini na kutaka uangaliwe upya kutokana na chama kimoja cha siasa kuwa na uwakilishi wa asilimia 72 katika Bunge la Katiba, jambo alilosema linaweza kuathiri upatikanaji wa Katiba inayozingatia matakwa ya masilahi ya wananchi.
“Bakaza tunapendekeza wabunge wa Bunge Maalumu wangechaguliwa na wananchi kwa kazi maalumu ya kuandika katiba tu ili kupata ridhaa ya wananchi kuhusu aina ya Katiba wanayoitaka wakati huu,” alisisitiza Profesa Shariff.
Alisema kuwa haikuwa sahihi kwa Zanzibar kunufaika na theluthi moja kati ya wajumbe 166 ambao watateuliwa kutoka katika makundi ya kijamii na asasi za kiraia, akitaka kila upande wa Muungano utoe idadi sawa bila ya kuzingatia udogo wa ardhi, uchumi au idadi ya watu baina ya pande mbili za Muungano.
Mkutano huo uliudhuriwa na Katibu Mtendaji wa Kamati ya Maridhiano, Ismail Jussa Ladhu, ambaye alisisitiza umuhimu wa amani na umoja wa kitaifa wakati huu wa mjadala wa kupata Katiba Mpya kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment