Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amevunja uongozi mzima wa chama hicho wilayani Kyela kwa madai kuwa viongozi hao hawakuwa waadilifu.
Badala yake, Dk. Slaa amekabidhi ofisi na mali za chama kwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Peter Mwamboneke, ambaye pia amepewa siku saba kuhakikisha anaandaa uchaguzi wa kujaza nafasi za viongozi hao.
Uamuzi huo ulitangazwa na Dk. Slaa kwenye mkutano wa hadhara mjini Kyela ulioandaliwa na chama hicho kwa ajili ya kutoa elimu ya umuhimu wa kushiriki kwenye mchakato wa upatikanaji wa Katiba iliyo bora kwa maisha ya Watanzania.
Alisema Chadema kwa sasa ni chama imara kilichokomaa na kuwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuwaongoza wananchi kupitia chama hicho, kamwe hawawezi kufanya kazi kwa kushurutishwa kwa namna yoyote na chama kingine cha siasa nchini.
Aidha, alikemea vikali vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi utakaoandaliwa, huku akionya kuwa yeyote atakayebainika ameingia madarakani kwa kutoa rushwa, ataenguliwa mara moja. Kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, Dk. Slaa alisema kinachoonekana hivi sasa ni kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeanza kufanya mizengwe ya kuharibu mchakato huo ili Katiba hiyo isipite.
Alisema CCM inatambua kuwa rasimu ya Katiba ikipitishwa kama ilivyoandaliwa na Tume ya Jaji Warioba, utakuwa ni mwisho wa utawala wake na kuwa hivi sasa inatumia kila mbinu kujinusuru na ndiyo sababu ilipitisha kinyemela Muswada wa Sheria wa Mabadiliko ya Sheria ya Katiba bungeni.
Dk. Slaa alisema hivi sasa vyama vya upinzani vimeungana kupinga muswada huo kusainiwa na Rais na kuwaomba wananchi kuwaunga mkono kwenye mapambano hayo.
No comments:
Post a Comment