Sunday, September 15, 2013

Dk. Slaa aenda Mbeya kumsafisha Sugu

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, leo anatarajia kuongoza mapokezi makubwa ya kumpokea Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’. Mbunge huyo anafanyiwa mapokezi hayo, ikiwa ni siku tisa tangu kutokea kwa vurugu kubwa bungeni, baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kuamuru Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kutolewa ndani ya Bunge.

Hali hiyo ilisababisha mvutano mkali kiasi cha kusababisha Sugu kupigana ngumi na askari kabla na baada ya kutolewa kwa nguvu nje ya ukumbi wa Bunge.

Mbali na kushiriki mapokezi hayo ya Sugu ambaye suala lake hilo limefikishwa polisi mjini Dodoma, Dk. Slaa akiwa katika ziara ya chama mjini Mbeya, anatarajia kuzungumza mambo mazito juu ya ufisadi nchini, ikiwa ni kumbukizi ya tangu alipotangaza orodha ya aibu ‘list of shame’ ya ufisadi na mafisadi nchini.

Siku kama ya leo, Septemba 15, mwaka 2007, Dk. Slaa alitangaza orodha ya mafisadi 11 katika mkutano ulioitishwa na vyama vya upinzani kwenye viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema Dk. Slaa akiwa katika ziara hiyo, atazungumza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na tathimini ya matukio ya mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni.

Alisema pamoja na mambo mengine, leo atatumia kumbukizi hiyo kufunua uozo mwingine unaoendelea kufanywa na viongozi wa Serikali ya CCM.

Akizungumzia mapokezi ya Sugu, Makene alisema yataanzia Isanga hadi uwanja wa Dk. Slaa (zamani mama John), pia ataeleza namna ufisadi ulivyoongezeka lakini msingi wake ukiwa ni ile ile orodha ya aibu ya mafisadi aliyoitangaza hadharani Septemba 15, 2007.

Alisema katika ziara hiyo, Dk. Slaa ataambatana na watendaji kutoka makao makuu, viongozi wa chama pamoja na wabunge wa chama hicho.

2 comments:

  1. nikiwa kama mkazi wa jimbo la mbeya mjini ninaimani na mbunge wangu kwani kila afanyalo nikwahajiri ya wananchi wake.

    ReplyDelete
  2. nikiwa kama mkazi wa jimbo la mbeya mjini ninaimani na mbunge wangu kwani kila afanyalo nikwahajiri ya wananchi wake.

    ReplyDelete