NI KWA KURIDHIA TOZO ZA SIMU ILIZOZIPINGA
HATUA ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuziba masikio na kupuuza kilio cha wananchi, badala yake kuridhia kampuni za simu ziwakate kodi ya sh 1,000 kwa laini (sim card) watumiaji, inakiweka njia panda chama hicho.
Uamuzi huo unaonesha kutokuwapo mawasiliano kati ya chama na serikali, kwani pamoja na wabunge wa CCM kupitisha bajeti hiyo bungeni, viongozi wa chama waligeuka na kuitaka serikali itafute kodi mbadala ya kuziba pengo hilo.
Tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeziandikia kampuni za simu waraka wa kuzitaka zianze kukata kodi mpya ya laini za simu mara moja kuanzia Julai 30, 2013.
Watumiaji wa simu zaidi ya milioni nane watakuwa hatarini kufungiwa simu zao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, kwa vile kodi hiyo itakayotozwa mwezi huu, itajumuisha miezi ya Julai, Agosti na Septemba.
Hatua hiyo inatokana na serikali kushindwa kufuta kodi hiyo ya sh 1,000 iliyopitishwa na Bunge kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete baada ya kukutana na wadau wa sekta ya mawasiliano.
Kwa maana hiyo, kila anayemiliki laini moja ya simu atakatwa sh 3,000; anayemiliki laini mbili sh 6,000 na anayemiliki laini tatu sh 12,000, lengo ni kuhakikisha serikali inakusanya sh bilioni 178 zitakazopelekwa kwenye bajeti kuu.
Kwa uamuzi huo wa serikali, ni wazi CCM ilikuwa ikifanya kiini macho kwa wananchi kujifanya inapinga kodi hiyo wakati wabunge wake ndio waliishabikia bungeni.
Tozo hiyo haikuwa bahati mbaya bali ilipangwa na kupata baraka za vikao vya juu vya CCM na Baraza la Mawaziri kabla ya bajeti hiyo kusomwa bungeni.
Hata kauli za Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu wake, Mizengo Pinda na viongozi wengine wa CCM akiwamo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ni wazi kuwa zilikuwa za kujaribu kupunguza jazba za wananchi, lakini hazikuwa na nia ya kuifuta kodi hiyo.
Katika kuthibitisha kuwa CCM walifahamu mapema tozo hiyo ni mwiba kwao, siku ya kusomwa kwa bajeti kuu ya serikali, Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, alilazimika kufuta pendekezo la awali katika kifungu (C) (viii) cha marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa, sura 147, akisema kimefanyiwa marekebisho.
Kabla ya marekebisho hayo kipengele hicho kilisomeka kuwa serikali ilikuwa inapendekeza kuanzisha ushuru wa bidhaa kwa laini za simu kwa kiwango cha sh 1,450 kwa mwezi, ambapo ushuru huo utakusanywa na kampuni za simu.
Hata hivyo, Waziri Mgimwa hakusema kuwa fedha hiyo itakayokusanywa itapelekwa kwenye Mfuko wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini kama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alivyonukuliwa baadaye.
Mbali na tozo hiyo kwenye laini za simu, serikali pia inatoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 14.5 kwenye huduma zote za simu za kiganjani badala ya muda wa maongezi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Uchumi, katika ushuru huo asilimia 2.5 zinatumika kugharamia elimu nchini.
Suala ambalo wananchi wengi hawakugundua mapema, ni kodi ya zuio ya asilimia 10 ya kamisheni ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mkononi, yaani M-Pesa, Tigo-Pesa, Aitel Money na Easy Pesa.
Licha ya Waziri Mgimwa kusema ushuru wa bidhaa kwenye simu hautatozwa kwenye huduma za kutuma na kupokea fedha, tayari makali hayo yameelekezwa kwa watumiaji, kwani kampuni hizo zimeongeza tozo kwenye huduma hizo za kutuma na kupokea fedha.
Kwa mkanganyiko huo wa kauli za Rais Kikwete, Waziri Mkuu Pinda na Nape, ni wazi kuwa uamuzi huo wa kubariki tozo hizo haukuwa shirikishi kwa serikali ya CCM na ndiyo sababu wameridhia kodi itozwe licha ya kuahidi kurudisha suala hilo bungeni.
Wakati Nape akisema kuwa CCM inataka serikali ifute kodi hiyo kwa madai kuwa ni mzigo kwa walalahoi, Pinda alidai fedha hizo zitakazokusanywa zilipangwa kuingizwa REA ili kusambaza umeme vijijini.
Bonyeza Read More kuendelea
Kauli ya Pinda inakinzana na maelezo ya Waziri wa Fedha bungeni, aliyesema kuwa fedha zitakazopelekwa REA ni zile za tozo mpya ya mafuta ya petroli (petroleum levy) ya sh 50 kwa lita, ambayo itakusanywa na TRA.
CCM na serikali walianza kujichanganya kwa kauli baada ya wamiliki wa kampuni za simu kutikisa kiberiti wakiipinga kodi hiyo kuwa inawaumiza watumiaji wa simu.
Waziri Mgimwa alijaribu kuzima upepo huo akisema kuwa watakaa na wadau hao kuona jinsi watakavyoweza kumaliza sakata hilo ambalo wanasiasa wa upinzani wamelibebea bango wakitaka lirudishwe upya bungeni.
Naye Pinda alidai kuwa kama wanasiasa wataendelea kuipinga dhamira njema ya serikali, itabidi serikali ipunguze idadi ya vijiji vilivyokuwa vimeingizwa kwenye orodha ya kupatiwa umeme na REA.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ambayo Kamati Kuu yake ndiyo iliishauri serikali katika kuandaa bajeti hiyo, aliitisha mkutano na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa kampuni za simu.
Katika mazungumzo hayo aliwapa mtihani mgumu wa kupendekeza jinsi gani ya kuziba pengo la sh bilioni 178 ambazo zitapotea katika bajeti iwapo kodi hiyo itafutwa.
Wakati Rais Kikwete akisema kodi hiyo haiwezi kufutwa moja kwa moja bila kutafuta njia nyingine za kupata fedha za kujaza pengo hilo la sh bilioni 178 zilizolengwa kupatikana, hoja kadhaa zimeibuliwa kwa serikali na CCM.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi wameweka bayana kuwa kauli ya Rais Kikwete inaonesha serikali haikuwa tayari kuifuta kodi hiyo licha ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wananchi.
Wakati mjadala wa tozo hizo ukiwa mkali, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge, ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi kupitia CCM, alisema licha ya idadi kubwa ya watu kupinga tozo hiyo hawakubahatisha kutoa pendekezo hilo, bali walifanya utafiti wa kina na kujiridhisha kuwa ni sahihi likaanzishwa.
Bunge kupitia Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Chenge lilitaka kuwapo kwa kodi hiyo ili kusaidia shughuli za bajeti ya serikali kuu.
Malalamiko hayo yaliendelea hadi kwa wananchi na baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliotaka posho za wabunge zipunguzwe ili kuziba pengo hilo badala ya kuwabebesha wananchi mzigo.
Inadaiwa kwamba msimamo wa Chenge unaungwa mkono na Spika wa Bunge, Anne Makinda, jambo lililosababisha kutojadiliwa kwa hoja binafsi ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) iliyohusu kodi hiyo katika mkutano wa Bunge lililopita kwa kisingizio cha kukosekana kwa muda wa kufanya hivyo.
Hata hivyo, takwimu zilizotolewa na kampuni za simu zinaonesha kuwa miongoni mwa wamiliki wa laini za simu milioni 22; milioni nane wanatumia chini ya sh 1,000 kwa mwezi.
No comments:
Post a Comment