Katibu mkuu wa Chadema Dk. Wilbrord Slaa amewataka wananchi wasikubali kuburuzwa na baadhi ya vyama vya siasa vinavyopinga mabadiliko yanayoendela katika rasimu ya katiba na kama wanadhani hata Chadema hakitendi haki kuwaongoza wana haki ya kukikataa.
Dk. Slaa alisema hayo jana, kwenye mikutano yake ya hadhara iliyolenga kupata maoni kupitia baraza la kitaasisi aliyoifanya katika miji ya Itigi wilayani Manyoni, makao makuu ya wilaya ya Ikungi, Kiomboi wilayani Iramba na Singida mjini, kwa kutumia usafiri wa helikopita.
Alisema baadhi ya vyama vinawapotosha wananchi ili waendelee kuwa na katiba mbovu inayokumbatia uwepo wa utawala unaoinyonya jamii, kuendelea kuwepo kwa ufisadi na uvunjivu wa wazi wa sheria, jambo ambalo Chadema wanapingana nayo.
Hata hivyo, Dk. Slaa alisema sehemu kubwa ya rasimu ya katiba inayotolewa maoni hivi sasa na wananchi kama chama wanaikubali isipokuwa baadhi ya marekebesho ambayo wanadhani mbele ya safari yatafanyiwa kazi na tume ya mabadiliko ya katiba nchini, chini ya Mwenyekiti Jaji Joseph Warioba.
Baadhi ya maoni yaliyotolewa na wananchi ni serikali iwe na wizara 16 bila uwapo wa manaibu waziri, Rais akiwa madarakani ashitakiwa iwapo atavunja sheria, tume ya uchaguzi itokane na mapendekezo ya bunge na Rais athibitishe tu na iwe ya kuajiriwa hadi ngazi ya chini.
Mapendekezo mengine ni Wakuu wa mikoa na wilaya wafutwe katika katiba mpya, Tanzania igawanywe kanda kumi za kimajimbo, pawepo na haki za wajane hasa suala la umiliki wa ardhi, haki ya watoto wadogo ikiwamo mimba na mkuu wa polisi(IGP) apendekezwe na bunge na Rais athibitishe tu.
Aidha Dk. Slaa alisema kuwa akiwa kama katibu wa chama kikuu cha upinzania (CHADEMA), ataendelea kukemea maovu na ufisadi unaofanyika nchini ikiwamo biashara ya meno ya tembo inayofanywa hata na baadhi ya viongozi wakubwa wa vyama vya siasa.
“Slaa ataendelea kupiga kelele ...meno ya tembo yanakamatwa mengi katika nchi za nje, ukisema unaambiwa Watazania tusivunje amani, wacha nisema kama nikupigwa risasi acha iwe hivyo, lakini sisi tuendelee kuhubiri amani na haki kamwe haitapotea,”alisema Dk. Slaa.
Katika hatua nyingine, katibu huyo alimfagilia mkuu wa polisi wilaya Singida kwa madai kuwa amepeleka askari kwenye mkutano huo ambao hawakuvaa mavazi ya kuwatisha wananchi, tofauti na maeneo mengine ambayo hali hutisha.
Kutokana na hali hiyo alimwomba mkuu huyo wa polisi kuendelea kuwaelimisha wenzake wa wilaya zingine ili waige mfano wa kuacha tabia ya kuwatisha wananchi kwa kuvalia mavazi ambayo utadhani wanasafiri anga za juu kwenda mwezini.
Mapema akimkaribisha Dk. Slaa, mwanasheria wa chama hicho wakili Mabere Marando alisema serikali tatu ni nafuu zaidi kugharamia kuliko serikali mbili zilizopo sasa zenye kuwa na wabunge 438, wakati ile ya serikali tatui itakuwa na wabunge 314 tu.
Leo Jumapili Dk. Slaa ataendelea na mikutano yake ya mabaraza ya katiba kitaasisi katika makao makuu ya tarafa ya Sepuka wilayani Ikungi na Mtinko katika wilaya ya Singida, na baadaye mchana ataelekea Kondoa mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment