Baadhi ya Wawakilishi wa Mabaraza ya kata 14 katika Manispaa ya Ilala, wamependekeza kufutwa kwa kipengele kinachoruhusu nafasi ya mgombea binafsi, kwa kuwa wagombea wanaweza kutumia itikadi za kidini itakayosababisha migogoro katika jamii.
Waliyasema hayo mbele ya Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika Kongamano la kutathimini rasimu ya katiba, lililofanyika jana, jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, alisema kwa kuwa mgombea huru hatokuwa na chama anaweza kutumia nafasi hiyo kupitia itikadi ya kidini, jambo ambalo linaweza kuwa na madhara makubwa baadaye.
"Jambo la mgombea kutokuwa na chama linaweza kuchochea suala la udini, kwakuwa anaweza kutumia dini yake katika masuala ya kisiasa zaidi, hivyo ni bora katiba ikaondoa kipengele hicho, "alisema Charles mjumbe kutoka kata ya Buguruni.
Naye, Mwakilishi toka kata ya Kivukoni, Ester Liwa, alisema suala la nafasi ya mgombea huru yapaswa iangaliwe kwa umakini kwa kuzingatia hoja tatu yaani unyeti wa nafasi yenyewe, maoni ya wananchi wengi pia suala la uwezekano wa kukosa udhamini.
Kuhusu suala la sifa za mgombea urais, alisema umri wa mgombea uwe kuanzia miaka 45 na elimu kuanzia Shahada mmoja.
Mwakilishi Stephan Chambo alisema kuna haja ya kuifanyia marekebisho suala la wajibu wa raia katika ibara ya 48 na kuongeza kifungu cha raia kujitolea bure katika mambo ya maendeleo mfano masuala ya ujenzi wa mifereji na makaburi.
No comments:
Post a Comment