Sunday, August 4, 2013

Sumaye amshukia Warioba

Amtaka asiingilie hoja za mabaraza ya Katiba
Awashauri vijana kuchukia rushwa na ufisadi
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameionya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, kutoingilia maoni ya wananchi wanaojadili rasimu ya Katiba hiyo.
Sumaye amesema tume ya Jaji Warioba haipaswi kuwa na msimamo wake kuhusu maoni yaliyotolewa na wananchi maana wamekwisha yaweka katika rasimu.
Mchakato wa kutungwa Katiba Mpya umefikia hatua ya kujadiliwa na mabaraza katika ngazi za wilaya, kata na asasi za kijamii ambapo maoni yanaendelea kutolewa.
Sumaye alitoa karipio hilo wakati akifunga mkutano wa baraza la Katiba katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, kampasi ya Mbeya ulioandaliwa na Chama cha Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Tahliso).
kumekuwapo na kauli kadhaa zinazotolewa na vyama vya siasa, asasi za kiaraia na tume hiyo, zikitafsiriwa kama kuingilia mchakato wa majadiliano ya umma kuhusu Katiba Mpya.
“Wao (tume), wamekwisha toa rasimu ya maoni, basi wayaachie mabaraza ya Katiba wajadili rasimu hiyo, badala ya kuonekana tume nayo ina msimamo wake ambao inataka upitishwe,” alisema.
Hata hivyo, Sumaye alisema tume hiyo haipaswi kulaumiwa kutokana na maoni yaliyojitokeza kwenye rasimu inayojadiliwa sasa.
“Ili mradi kazi ya tume ilikuwa ni kuratibu maoni ya wananchi, basi tume haipaswi kulaumiwa kwa maoni yaliyotolewa, isipokuwa kama tume imetoa rasimu isiyowakilisha maoni na wananchi walivyoyatoa,” alisema.
Wakati wa kutoa maoni yao bila shaka wapo Watanzania waliotaka serikali moja, wapo waliotaka serikali mbili, waliotaka serikali tatu, waliotaka serikali nne labda wapo waliotaka serikali ya mkataba na inawezekana labda wapo waliotaka tuachane na Muungano.
Kwa mujibu wa Sumaye, siyo sahihi mtu au kundi la watu kukejeli au hata kutukana mtu au kundi lingine lililotoa maoni yanayotofautiana na yake au ya kundi lake.
Alisema, Watanzania wanapaswa kujifunza ustahimilivu na kuheshimu maoni au mawazo ya watu wengine, na kama hatukubaliani nayo, wayapinge kwa nguvu ya hoja na siyo hoja ya nguvu.
Sumaye alimkariri mwanazuoni, marehemu Wole Soyinka, aliyewahi kusema, the greatest threat to freedom is the absence of criticism, akimaanisha tishio kubwa kwa demokrasia ni kutokuwapo kwa ukosoaji.
Sumaye alisisitiza kuwa matatizo yaliyopo nchini, mathalani maisha magumu na maendeleo duni, hayawezi kutatuliwa kutokana na kuwapo kwa Katiba Mpya.
Kauli kama hiyo, iliwahi kutolewa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuizindua Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Sumaye alisema, anaamini kwamba hata Katiba iliyopo sasa bado ni nzuri, akitumia kigezo cha kutumika kwake kwa kipindi cha miaka 50 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, kutokana na changamoto na mabadiliko yanayojitokeza, Katiba hiyo ingehitaji marekebisho.


USHIRIKI WA TAHLISO
Sumaye alisema ushiriki wa TAHLISO katika baraza la Katiba, una umuhimu wa pekee kutokana na sababu tofauti.
Alizitaja baadhi yake kuwa ni TAHLISO kuwawakilisha vijana wasomi wenye uelewa, ambao mchango wao utatoa upeo wa hali ya juu katika Katiba hiyo.
Pia alisema vijana wana umuhimu wa pekee katika mchakato wa Katiba hiyo, kwa vile watapenda kuwa na chombo hicho (katiba) kitakachoitengeneza Tanzania inayofaa.
“Kijana utakuwa mtu wa ajabu sana kama utataka kuishi kwa miaka hamsini ijayo katika nchi ya shida isiyo na maendeleo, iliyojaa rushwa, na isiyo na matumaini,” alisema.
Aliongeza, “vijana wa Tanzania wakiongozwa na ninyi wasomi, lazima mshiriki kutengeneza Katiba itakayoweka, kwa miaka mingi ijayo, mazingira ya nchi yetu ya salama na amani na pia ya maendeleo kwa wote bila kujali rangi, dini, jinsia au ukundi wowote.”
RASIMU YA KATIBA MPYA
Sumaye alisema kuna vipengele vingi katika rasimu hiyo, akiivita kuwa ‘vigumu’ na ‘vyepesi’.
Kuhusu ‘sakata la Muungano’, Sumaye alisema idadi ya serikali zitakazoundwa si jambo kubwa kwake, bali hoja zinazowiana na muundo huo.
Alizitaja hoja hizo kuwa ni sababu za kufikia uamuzi huo, ikiwa serikali tatu itatoa jawabu la kuyatatua matatizo yaliyopo na kuubaini muundo utakaoutikisa Muungano.
Alizitaja hoja nyingine zinazohitaji majawabu kuwa ni uwezekano wa kugharamia serikali tatu na vyombo vyake.
“Ni dhahiri kuna maswali yanayotaka majibu au kama majibu hayapatikani, basi tukae chini tuyatafakari kwa makini zaidi,” alisema.
Alisema yapo matatizo makubwa manne ambayo hayajatatuliwa chini ya mfumo wa serikali mbili, na kwamba serikali tatu itayafanya kuwa magumu zaidi.
Aliyataja kuwa ni mvutano wa madaraka na wa utaifa, mgawanyo wa rasilimali, gharama za uendeshaji na changamoto zinazotokana na jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama.
AUZUNGUMZIA UADILIFU
Sumaye alisema Katiba Mpya pekee si mwarobaini wa matatizo ya jamii, bali inahitaji kusimamiwa na serikali adilifu, inayojali maslahi ya umma.
Pia alisema Rais wa nchi anapaswa kuwa mchapakazi na anayejali maslahi ya umma mpana na siyo maslahi yake binafsi, ya watoto wake au ya marafiki zake.
“Yeye mwenyewe (Rais) awe na uadilifu usiotiliwa mashaka ya aina yoyote na apigane vita vya wazi dhidi ya rushwa, ufisadi, dawa za kulevya na maovu mengineyo katika jamii,” alisema.

No comments:

Post a Comment