Wednesday, August 7, 2013

Msajili asifiwa, aonywa

SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Jaji Francis Mutungi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa akirithi mikoba ya John Tendwa, baadhi ya wasomi wamemsifu na kumpa angalizo.
Wakizungumza na gazeti hili jana, wasomi hao wabobezi katika taaluma ya sheria, walisema kuwa Jaji Mutungi licha ya umahili wake katika utendaji, anatakiwa kuwa makini ili kujiepusha na upendeleo wa wazi kwa vyama kama alivyokuwa mtangulizi wake.
Wakili wa Mahakama Kuu ambaye pia ni mwanasiasa wa siku nyingi, Mabere Marando, alisema amemfahamu Jaji Mutungi kwa muda mfupi akiwa jaji, kwamba hana rekodi ndefu ya kuwa Mahakama Kuu.
“Lakini tunajua akiwa jaji amekuwa mtu anayesimamia haki, kazi yake kwa muda mrefu alifanya kama hakimu kiongozi wa Mahakama ya Kisutu na ana rekodi nzuri katika kazi hiyo,” alisema.
Marando alisema kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama hahihitaji sana mwanasheria au jaji, bali inahitaji mtawala mwenye uwezo wa kuongea vizuri na viongozi wa vyama, akishauriwa kisheria na wasaidizi wake.
Aliongeza kuwa changamoto kubwa atakayokumbana nayo Jaji Mutungi kwa sasa ni ugomvi wa wanasiasa, kwa sababu msajili aliyepita alitekeleza maagizo na maelekezo kadiri CCM watakavyo.
“CCM walisema CHADEMA ni magaidi na kweli msajili akaingia katika mtego huo kusema hayo, lakini watekelezaji wakubwa wa ugaidi ni CCM wenyewe na hayo yalifanyika kuwapendeza CCM,” alisema.
Naye Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Padri Charles Kitima, alisema kwa kuwa Mutungi ni jaji, wanatumaini alisimamia haki vizuri hadi akakidhi vigezo vya kupata hadhi hiyo.
Dk. Kitima ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alitaja changamoto atakazokumbana nazo msajili huyo kuwa ni kuleta fikra mpya inayoonesha kwamba vyama vyote vipo sawa.
Alisema kuwa Jaji Mutungi hapaswi kuvionea vyama vya upinzani na kuibeba CCM.
“Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, vyama vya upinzani vilinyanyaswa sana, huku CCM ikibebwa, sasa tunatarajia jaji huyu alete usawa wa vyama vyote, na yule aliyestaafu tunamtakia kila la heri, mchango wake tumeuona,” alisema.

No comments:

Post a Comment