John Tendwa alipaswa kuwa ameondoka kwenye Ofisi ya Msajili
wa Vyama vya Siasa, tangu mwaka 2008, alipofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu
wa sheria. Aliendelea kufanya kazi zake hata baada ya muda wa mkataba wake
alioongezewa kuwa umefikia mwisho, hivyo alikuwa anakalia ofisi hiyo ya umma,
kinyume cha sheria.
Ametumia muda huo wa miezi kadhaa, aliokuwa anakalia ofisi
ya umma kinyume cha sheria, kuropoka na kuharibu demokrasia, kwa manufaa ya
mamlaka iliyomteua na CCM. Kutokana na mwenendo (maneno na matendo) wake mbovu,
CHADEMA ilitangaza kutokumpatia ushirikiano wowote, yeye kama Tendwa.
Ikamtangaza kuwa adui wa demokrasia nchini.
Kwa muda wote huo, CHADEMA ilikuwa ikitoa ushirikiano kwa
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Badala ya kuifuta CHADEMA na kufanikisha
dhamira ovu ya kuharibu amani ya nchi, ameondoka yeye.
Kuondoka kwa Tendwa hakuzuii kutekelezwa kwa
mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, iliyomkuta na hatia ya
kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Sensa, hivyo akasababisha
kutokea kwa mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Nyololo, Iringa.
Hivyo CHADEMA, kupitia Kurugenzi ya Habari na Uenezi,
inataka kauli ya Rais Jakaya Kikwete juu ya utekelezaji wa mapendekezo
hayo kwa Tendwa watu wengine, akiwemo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa, Michael Kamuhanda na wote waliotajwa katika ripoti hiyo ya chombo cha
serikali, kuwa walivunja sheria za nchi na kusababisha mauaji ya mwandishi,
raia asiyekuwa na hatia.
Tunamkaribisha 'with benefit of doubt', msajili mpya, Jaji
Francis Mutungi, kwenye kazi na majukumu yake mapya. Wapenda demokrasia
na maendeleo nchini, wanamtarajia atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia haki,
sheria na utawala bora, asije akapita njia ya Tendwa.
Kupitia mchakato wa Katiba Mpya unaojadiliwa sasa hivi,
CHADEMA tunapendekeza Ofisi ya Msajili ipewe uhuru zaidi na uteuzi wake, usiwe
suala la Rais kuamka tu na kuamua kuteua bila wahusika kuomba, kuchujwa na
kuthibitishwa na mamlaka nyingine tofauti na iliyoteua.
Tunatambua kuwa msajili mpya aliwahi kuwa Msajili wa
Mahakama ya Rufani, kwa muda mfupi, kisha akateuliwa kuwa Jaji na akateuliwa
pia nafasi zingine. Na sasa mwaka mmoja baada ya kutumikia nafasi hizo,
ameteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Jaji Mutungi, anapaswa kuonesha kwa maneno na vitendo kwamba
hatakuwa kama Tendwa, kwa kuanza kushughulikia matendo ya kiharamia
yaliyofanywa na Green Guards wa CCM kwenye chaguzi za madiwani, zilizomalizika
karibuni, ambazo si tu yalikuwa kinyume na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai, ambayo Jeshi la Polisi wanatakiwa kuchukua hatua, bali pia yalikuwa
kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa. Hivyo yako kwenye mamlaka yake.
Jaji Mutungi, amshauri Rais Jakaya Kikwete kushughulikia
mapendekezo ya Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, juu ya
uvunjifu wa sheria wa wazi uliofanywa na askari polisi na John Tendwa, hivyo
kusababisha mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012,
huko Nyololo, Iringa.
Aidha, Jaji Mutungi anapaswa kumshauri Rais Kikwete kujibu
na kufanyia kazi barua mbili alizoandikiwa na CHADEMA juu ya kuunda Tume Huru
ya Kimahakama/Kijaji, kuchunguza mauaji yaliyofanyika kwenye shughuli halali za
kisiasa za CHADEMA.
Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya mauaji mfululizo mkoani
Morogoro na Iringa, CHADEMA ilimwandikia barua Rais Kikwete kumtaka aunde Tume
ya Kimahakama kuchunguza utata wa vifo hivyo na vingine kadhaa vilivyotokea
kwenye shughuli halali za kisiasa, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, ili
ukweli ujulikane, haki itendeke na wahusika wachukuliwe hatua, hadi sasa rais
hajafanya hivyo.
Itakumbukwa pia kuwa baada ya mlipuko wa bomu la Arusha,
kwenye mkutano wa kampeni, CHADEMA pia ilimtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka
yake kuunda Tume Huru ya Kimahakama, ili ushahidi juu ya tukio hilo
uwasilishwe, hadi sasa pia rais yuko kimya. Hivyo kwa nafasi yake, msajili mpya
atoe ushauri kwa rais kuchukua hatua hizo, ili vyama vitimize wajibu wa
kikatiba kufanya kazi zake kwa haki, uhuru na sheria za nchi zinazosimamia
shughuli za vyama vya siasa nchini.
Imetolewa leo, Jumatatu, 5 Agosti, 2013 na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari, CHADEMA
No comments:
Post a Comment