Tuesday, August 6, 2013

Jaji Warioba atwishwa lawama

MJUMBE wa Halmashauri Kuu (NEC) taifa, ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Evodius Mmanda, ameituhumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, akidai kuwa inafanya kazi ya kuwashawishi wananchi kukubaliana na mfumo wa serikali tatu iliyoupendekeza kwenye rasimu.
Mmanda alitoa madai hayo jana wakati akitoa mada katika kongamano la vijana wa CCM Mkoa wa Vyuo Vikuu lililojadili rasilimali za taifa.
Alisema anapata shaka kuona tume ya kukusanya maoni ikiwa inajitetea kila wakati baada ya kutoa rasimu yake hadharani, aliyoelezea kuwa inapaswa kujadiliwa na wananchi.
“Mimi ni shahidi, nimesikia na kuona ‘live’ kule mkoani Kilimanjaro maofisa wa tume wakiwalazimisha watu kuwa na serikali tatu, sasa ninapata shaka juu ya hili,” alisema.
Mmanda ambaye kitaaluma ni mwanasheria na wakili wa kujitegemea, alisema wajumbe wa tume hiyo hawakupewa kazi ya kuandika Katiba mpya bali jukumu lao linaishia kukusanya maoni na kuyarejesha kwa wananachi yakiwa katika mfumo wa kisheria.
Kuhusu rasimu ya Katiba mpya, alisema kama Watanzania watakubaliana na pendekezo la serikali tatu watakuwa wamefanya makosa kwa kile alichoeleza kuwa fursa nyingi zilizopo katika mfumo wa serikali mbili zitakuwa hazipatikani.
Alisema rasimu imependekeza mambo ya muungano kuwa saba pasipo kutaja vitu vya msingi vitakavyoshughulikiwa na muungano huo huku akitahadharisha rasimu hiyo kutokutaja mipaka ya Tanzania kiufasaha.
Aliongeza kuwa katika sehemu ya rasimu hiyo ibara ya pili, inaeleza mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari.
Alisema ibara hiyo imeacha kutaja mito na maziwa, hali inayohalalisha madai ya Rais wa Malawi, Joyce Banda, juu ya umiliki wa Ziwa Tanganyika.
Naye Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, aliwataka vijana wasomi kujiamini na kuingia katika kuwania nafasi za uongozi sehemu mbalimbali.

1 comment:

  1. Hao ndo CCM chama kwanza Taifa badae. hawatwambie je ni halali Zanzibar kupata yote kwa ajiri yao tu huku bara ikitawaliwa na zanzibar hata kwa mambo yasiyo ya muungano au kuanzia sasa no mzanzibar kutawala bara na je nani. Kaamuru bara itawaliwe na serikali ya muungano ambao nao ni tatizo kama upo kweli kama serikali moja ya zenj ipo bara hakuna? Au ndo kutafuta cheo kwa kujipendekeza kwa watawala baada ya kutokubalika kwa wapinyani?
    m

    ReplyDelete