CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeshauriwa kuwa na mikakati kabambe ya kuimarisha uongozi ngazi za chini ili kasi yake iende sambamba na ile ya ngazi ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Deusdedit Katto, ambaye ni Mwenyekiti wa Tawi la Sokoine, Gongo la Mboto (Chadeama) jana, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumzia kuhusu uhai wa chama hicho katika ngazi ya shina, tawi, kata, jimbo, wilaya na mkoa.
Katto alisema kuwa viongozi wa kitaifa wanafanya kazi kubwa, nzuri na iliyotukuka lakini katika ngazi za chini mambo hayako sawa, utendaji wa viongozi bado unalegalega, hivyo kuutaka uongozi wa juu kumlika pia ngazi za chini.
Aidha, alishauri katika ngazi ya mashina pia kuwe na mabalozi wa CHADEMA ambao watatoa huduma kwa wanachama wao kuliko kazi hiyo kuachiwa mabalozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee, wakati hata wao sheria ya vyama vingi inaruhusu kuwa na wa kwao.
Kiongozi huyo wa CHADEMA na mwanaharakati mahiri, alishauri kuwa ingefaa katika ngazi zote za chama kuwe na orodha kamili ya majina katika rejesta za wanachama ili iwe rahisi kufahamu idadi sahihi ya wanachama waliopo kuliko ilivyo sasa.
“Mimi napendekeza kuwe na kumbukumbu kamili katika rejesta za wanachama wa CHADEMA tangu ngazi ya shina hadi taifa ili tunapotaka kufahamu idadi kamili ya wanachama wetu iwe rahisi kuliko ilivyo sasa ambapo kumbukumbu zetu bado zina dosari, si kamilifu,” alisema Katto.
Vilevile Katto amewataka viongozi wa chama hicho wanapopewa nafasi za kuongoza wawe tayari kuwatumikia wananchi kama walivyoahidi kuliko kuangalia masilahi yao binafsi na kushindwa kuwapa mwongozo wa kujiletea maendeleo wale waliowachagua.
Amewataka pia viongozi wa chama hicho katika ngazi mbalimbali kubuni mikakati mahususi ya kuwawezesha wanachama na wananchi kwa ujumla kuwa na mipango madhubuti ya kujiongezea kipato wakiwa katika vikundi au mtu mmoja mmoja ili kukabiliana na umaskini uliokithiri.
Katto pia amewataka viongozi wa chama hicho kuwa na mikakati maalumu ya kuwasaidia wakulima wa vijijini, kwa kuwawezesha kupata pembejeo za kilimo za bei nafuu kama matrekta madogo ‘Power Tiller’ ili waweze kuzalisha kwa wingi na kuepukana na matatizo ya fedha na chakula yaliyoota mizizi nchini mwetu.
No comments:
Post a Comment